RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akimsikiliza Waziri wa Habari,Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Tanzania Mhe. Nape Moses Nnauye, alipofika Ikulu Zanzibar kwa mazungumzo na kujitambulisha na Ujumbe wake, mazungumzo hayo yaliyofanyika katika ukumbi wa Ikulu Jijini Zanzibar.(Picha na Ikulu)
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akizungumza na Ujumbe wa Wizara ya Habari,Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Tanzania ukiongozwa na Waziri wa wizara hiyo Mhe.Nape Moses Mnauye.(kulia kwa Rais) na (kushoto kwa Rais ) Katibu Mkuu Kiongozi na Katibu wa Baraza la Mapinduzi Mhandisi Zena Ahmed Said.(Picha na Ikulu)
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akizungumza na Waziri wa Habari,Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Tanzania Mhe.Nape Moses Nnauye, baada ya kumaliza mazungumzo yao alipofika Ikulu Jijini Zanzibar kwa mazungumzo na kujitambulisha leo 20-1-2022.(Picha na Ikulu)
STATE HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
Zanzibar 20.01.2022

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali
Mwinyi ameeleza matumaini yake makubwa katika kuimarisha mashirikiano kati ya pande mbili za Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania ikiwa ni pamoja na kukuza sekta ya mawasiliano.
Rais Dk. Mwinyi aliyasema hayo leo
wakati alipofanya mazungumzo na Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya
Habari Nape Moses Nnauye Ikulu Zanzibar akiwa amefuatana na ujumbe wake.
Katika mazungumzo hayo Rais Dk. Mwinyi
alimpongeza Waziri Nape kwa kupata wadhifa huo na kuahaidi kwamba Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar itaendeleza ushirikiano uliopo ili kuweza kufanikisha
kuwapatia wananchi wote mawasiliano sambamba na kushirikiana katika nyanja
nyengine muhimu zilizokuwemo katika Wizara hiyo ili pande mbili hizo ziweze
kwenda kwa pamoja katika maendeleo.
Alieleza kwamba kuweko kwa mradi wa
kusambaza minara ambao itawekwa minara ipatayo 42 katika Shehia zipatazo 38 Unguja
na Pemba kutasaidia kwa kiasi kikubwa kuweza kuwapatia mawasiliano bora
wananchi, mradi utakao simamiwa na Mfuko wa Mawasilano kwa wote (UCSAF)
ulioanzishwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Nae Waziri wa Habari, Mawasiliano na
Teknolojia ya Habari Nape Moses Nnauye kwa upande wake aliahidi kutekeleza
majukumu yake ipasavyo na kueleza kwamba ushirikiano uliopo kati ya Mfuko wa
Mawasiliano na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ni mzuri.
Alisema kwamba mradi huo utafanyika kwa
kiasi ya TZS Bilioni 6.9, ambao pia, umezingatia Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha
Mapinduzi (CCM), pamoja na maelekezo aliyoyatoa katika ziara zake alizozifanya
katika mikoa ya Zanzibar ambapo iligundulika kwamba kuna baadhi ya maeneo
katika visiwa vya Unguja na Pemba hawapati mawasiliano bora ya simu.
Sambamba na hayo, Waziri Nape
alimuhakikishia Rais Dk. Mwinyi kwamba Wizara anayoiongoza itatoa mashirikiano
ya kutosha hasa kwa kutambua kwamba ni Wizara ya Muungano.
No comments:
Post a Comment