Habari za Punde

SERIKALI YA AWAMU YA SITA YAJIZATITI KUENDELEZA PROGRAMU ZA KUKUZA UJUZI: WAZIRI NDALICHAKO

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Prof. Joyce Ndalichako akizungumza wakati wa hafla ya kutunuku vyeti kwa Wanagenzi wahitimu wa mafunzo ya kurasimisha ujuzi uliopatikana nje ya mfumo rasmi wa mafunzo katika Chuo cha Ufundi Stadi VETA Njiro, Jijini Arusha 
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Prof. Joyce Ndalichako (kushoto) akikabidi orodha ya Wanufaika wote wa mafunzo kurasimisha ujuzi uliopatikana nje ya mfumo rasmi ki-Mkoa Naibu Waziri Ofisi ya Rais, TAMISEMI, Mhe. Dkt. Festo Dugange (katikati). Kulia ni Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) Mhe. Patrobas Katambi.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Prof. Joyce akikabidhi cheti kwa Bi. Rejina Panga (wenye ulemavu) mmoja wa wahitimu wa mafunzo ya kurasimisha ujuzi uliopatikana nje ya mfumo rasmi katika Chuo cha Ufundi Stadi VETA Njiro, Jijini Arusha Januari 15, 2022.

Na: Mwandishi Wetu - Arusha

Serikali ya Awamu ya Sita Inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan imeweka kipaumbele katika programu za kukuza ujuzi kwa lengo la kuwasaidia vijana ili waweze kujiajiri au kuajiriwa sambamba na kuwajengea uwezo wa kukuza na kuboresha uzalishaji katika fani mbalimbali. 

 

Hayo yamebainishwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Prof. Joyce Ndalichako wakati wa hafla ya kutunuku vyeti kwa Wanagenzi wahitimu wa mafunzo ya kurasimisha ujuzi uliopatikana nje ya mfumo rasmi wa mafunzo katika Chuo cha Ufundi Stadi VETA Njiro, Jijini Arusha Januari 15, 2022.

 

Mheshimiwa Prof. Ndalichako alieleza kuwa, Serikali inayoongozwa na Mhe. Samia Suhulu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ina dhamira ya dhati ya kuwasaidia vijana nchini na katika kutekeleza hilo Serikali kupitia Mpango wa  Tatu wa Taifa wa Maendeleo wa Miaka Mitano (2021/2022 - 2025/2026), ambao unalenga kukuza ujuzi kwa watanzania wapatao 681,000 ambapo kati yao 100,000 ni wa mafunzo ya kurasimisha ujuzi.

 

Katika utekelezaji wa programu hii hadi kufikia Juni, 2022 tutakuwa tumeweza kurasimisha ujuzi jumla kwa watanzania 24,750 na hivi karibuni tunatarajia kutangaza nafasi za mafunzo ya urasimishaji zisizopungua 4,000 ambayo yatafanyika katika kipindi cha Januari hadi Juni, 2022, hivyo Ofisi ya Waziri Mkuu itahakikisha lengo hilo linatimia,” alisema Waziri Ndalichako


Aliongeza kuwa, lengo la programu hiyo ya Taifa ya kukuza Ujuzi ni kuwezesha nguvu kazi ya Taifa kupata ujuzi na stadi za kazi stahiki zitakazosaidia kumudu ushindani katika soko la ajira la ndani na nje ya nchi kwa kuwezesha nguvukazi nchini kuwa na uwezo wa kujiajiri au kuajiriwa na waajiri mbalimbali nchini.


"Vijana wanaopatiwa vyeti kwa ujumla ni 2,537 na katika Chuo cha Ufundi stadi VETA Njiro hapa Jijini Arusha vijana 511 wamesharasimishwa katika kipindi cha Julai hadi Desemba, 2021 na Ofisi ya Waziri Mkuu ipokatika mchakato wa kurasimisha ujuzi kwa vijana 4,416 ifikapo Juni 2022,"

 

“Vyeti mnavyotunukiwa vitawawezesha kujiendeleza kielimu, kuboresha huduma wanazotoa na kutafuta ajira au kujiajiri, kufungua taasisi au kampuni za kibiashara na hivyo kufanya shughuli zao kuwa rasmi; na hatimaye kutambulika na taasisi za mikopo, kukuza biashara zao, kuongeza kipato chao na pia kuchangia katika pato la taifa. vyeti hivi pia vitamuwezesha fundi kuwa na sifa ya kuomba zabuni mbalimnbali za Serikali na Taasisi binafsi,” alieleza Waziri Ndalichako

 

Alifafanua kuwa, Utafiti wa nguvukazi uliofanyika mwaka 2020/2021 ulibainisha kuwa Tanzania ina watu 25,861,023 wenye uwezo wa kufanya kazi, kati ya kundi hilo la watu wenye ajira ni 23,536,135 sawa na asilimia 91 na wasio na ajira ni 2,324,888 ikiwa ni sawa na asilimia 9.

 

“Juhudi za Serikali kupitia programu hii ni kuhakikisha watu wasio na ajira ambao wako katika soko la ajira wanawezeshwa kwa kujengewa ujuzi ili waweze kufanya shughuli za kiuchumi na hatimaye kujiajiri au kuajiriwa.” alisema

 

“Serikali inatambua mchango wa watu waliopata ujuzi kupitia mfumo usio rasmi na ndiyo maana imechukua hatua hii muhimu ya kuhakikisha wanatambulika rasmi ili nao waweze kushiriki katika shughuli rasmi ikiwemo kufanya kazi katika miradi ya Serikali ya kimkakati,” alieleza

 

Aidha, Waziri Ndalichako alitumia fursa hiyo kuwasihi vijana na watanzania kwa ujumla wenye ujuzi katika fani mbalimbali na ambao hawana vyeti vinavyoutambulisha ujuzi wao kuchangamkia programu hiyo kwa kuwa mafunzo hayo hawalipii gharama yoyote isipokuwa muda wao wa kushiriki katika mafunzo.

 

Pia, Mheshimiwa Prof. Ndalichako alihimiza taasisi mbambali nchini kutumia kikamilifu wahitimu hao kwa kuwa wamebobea katika fani mbalimbali za ufundi.

 

Vijana hawa wameingia rasmi katika soko la ajira, hivyo ni vyema kuwasaidia kwa kuwatumia ipasavyo katika miradi mbalimbali inayotekelezwa katika maeneo mbalimbali ili waweze kujipatia kipato na kuondokana na changamoto za kijamii zinazotokana ukosefu wa ajira,”

 

Awali akizungumza Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe. Prof Adolf Mkenda alisema kuwa kupitia programu hiyo ya taifa ya kukuza ujuzi, Serikali itaweka mifumo bora ya tathimini kwa wahitimu wanaomaliza katika Vyuo vya Ufundi Stadi vilivyopo nchini ili kuwawezesha vijana hao kujiajiri, kuajiriwa na kuajiri wenzao.

 

Naye, Naibu Waziri Ofisi ya Rais, TAMISEMI, Mhe. Dkt. Festo Dugange alisema kuwa ofisi hiyo itaendelea kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu ili kuhakikisha Agizo la Mheshimiwa Waziri Mkuu alilotoa Agosti 2, 2021 kuwa Halmashauri zote ziwatambue vijana waliofaidika na mafunzo ya programu ya taifa ya kukuza ujuzi na ziwasaidie kuunda vikundi na kuwawezesha kupata mikopo kupitia asilimia 10 za mapato ya ndani zinazotengwa kwa ajili ya mikopo kwa vijana, wanawake na wenye ulemavu.

 

“Vijana hawa tayari wana ujuzi wanachokosa ni mitaji ya kuanzisha au kuendeleza shughuli zao za kiuchumi, hivyo viongozi wa Halmashauri hakikisheni vijana wanawezeshwa mikopo ya asilimia 10 za mapato ya ndani. Vijana asilimia 4%, Wanawake asilimia 4% na Watu wenye Ulemavu asilimia 2% ili wakaendeleze ujuzi walionao kupitia shughuli watakazoanzisha ama kuendeleza mara baada ya kupatiwa mikopo hiyo,” alisema Dkt. Dugange

 

Kwa Upande wake Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mhe. John Mongella alisema kuwa Mkoa huo umeendelea kuhamasisha vijana kushiriki kwenye mafunzo hayo ili waweze kupata ujuzi utakaowawezesha kushiriki katika kusukuma gurudumu la maendeleo ya taifa.

 

Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) Mhe. Patrobas Katambi alisema kuwa katika utekelezaji wa Programu ya Taifa ya Kukuza Ujuzi, Ofisi hiyo imeendelea kuchukua hatua katika kuhakikisha wenye Ulemavu wanajumishwa kwa wingi kwenye fani mbalimbali ili waweze kujiendeleza pia.

 

Naye, Mnufaika wa Mafunzo hayo fani ya Ushonaji Bi. Rejina Panga ameishukuru Serikali kwa kuendelea kujali na kutambua mchango wa vijana na kuwapatia ujuzi uliowasaidia kuondokana na changamoto za ajira na kushiriki ipasavyo katika kukuza maendeleo ya taifa.

 

Katika hafla hiyo Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Prof. Joyce Ndalichako alikabidhi orodha ya Wanufaika wote wa mafunzo hayo ya kurasimisha ujuzi uliopatikana nje ya mfumo rasmi ki-Mkoa kwa Naibu Waziri Ofisi ya Rais, TAMISEMI, Mhe. Dkt. Festo Dugange kwa lengo la kukukabidhi ili nawe ukaikabidhi Mikoa husika ili kuwezesha wanufaika hao.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.