Habari za Punde

Ujenzi wa viwanda kuongeza fursa za ajira nchini


 NAIBU Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dk.Abdulla Juma Mabodi akionyeshwa mchoro wa eneo litakalojengwa Viwanda katika Kijiji cha Panga tupu Mkoa wa Kaskazini Unguja.

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimesema ujenzi wa Viwanda nchini utasaidia kuongeza fursa za ajira kwa wananchi wa makundi yote.

Kauli hiyo imetolewa na Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dk.Abdulla Juma Mabodi kwa niaba ya Katibu Mkuu wa CCM Taifa Ndg. Daniel Chongolo, huko Panga Tupu wakati akiangalia eneo lililotengwa kwa ajili ya viwanda ikiwa ni mwendelezo wa ziara ya Wajumbe wa Sekretariet ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa katika Mkoa wa Kaskazini Unguja.

Dk.Mabodi amesema katika Ilani ya CCM iliahidi kuhakikisha kwa kipindio cha miaka mitano inakamilisha ajira 300,000 hivyo eneo hilo likijengwa viwanda itakuwa ni fursa kubwa ya kiuchumi kwa wananchi wa Mkoa huo na Mikoa jirani.

Alieleza kwamba mafanikio hayo ni moja ya mikakati madhubuti ya Chama Cha Mapinduzi katika kutekeleza Sera zake kwa vitendo kwa lengo la kuwainua wananchi kiuchumi na kujiajiri wenyewe.

Katika maelezo yake Dk.Mabodi, alifafanua kuwa Zanzibar imepiga hatua kubwa kimaendeleo na kutoa wito kwa wawekezaji mbalimbali kujitokeza kuwekeza viwanda wakiwemo wazawa.

“Wana CCM na Wananchi kwa ujumla tulipita nyumba kwa nyumba tukiomba kura na kunadi Sera zetu tukiomba mtupe ridhaa ya uongozi na hatimaye mkatuamini na kutuweka madarakani, sasa tunaendelea kutekeleza yale tuliyowaahidi kwa kufungua milango ya uweekezaji mkubwa katika Sekta ya Viwanda.”, alisema Dk.Mabodi.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa Kaskazini Unguja, Ayoub Mohamed Mahmoud, akizungumzia fursa zitakazopatikana katika eneo la Viwanda alisema patajengwa na barabara ya lami yenye urefu wa Kilomita nane  ili kurahisha huduma za usafiri.

Wakati huo huo Dk.Mabodi, amekagua maendeleo ya mradi wa ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Kaskazini ‘’A’’ inayogharimu Sh.Bilioni 4.4 zikiwa ni fedha za mfuko wa UVIKO-19.

Akikagua mradi huo Naibu Katibu Mkuu huyo alieleza kuwa ameridhishwa na huduma za kitabibu zitakazotolewa katika Hospitali hiyo kwani zinaendana na mahitaji ya wananchi wa maeneo hayo,ambayo imeanza kujengwa mwezi januari na itakamilika mwezi juzi mwaka  huu.

Alisema ikikamilika itapunguza masafa ya kufuata huduma za Afya katika Hospitali ya Mnazi Mmoja na kesi nyingi zitashughulikiwa katika hospitali hiyo itakayokuwa na vifaa tiba ya kisasa.

Pamoja na hayo katika maelezo yake amesisitiza dhana ya wananchi kujitolea katika ujenzi wa miradi mbalimbali ya maendeleo na kuwataka Vijana wote nchini kuendeleza utamaduni huo ulioasisiwa na waliokuwa Vijana wa ASP na TANU na sasa ni Chama Cha Mapinduzi.

“ Tunaenda kuwa na Hospitali za Kisasa katika Wilaya zote Zanzibar,nasaha zangu kwa wananchi tuendelee kuziamini Serikali zetu na Viongozi wetu wakuu ambao ni Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Hussein Ali Mwinyi na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan kwamba wana dhamira njema ya kuleta Mapinduzi ya kimaendeleo”, alieleza Dk.Mabodi.

Akizungumzia dhana ya Uchumi wa bluu Dk.Mabodi, alisema Serikali inajenga bandari za kisasa katika maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Kaskazini Unguja kwa lengo la kutoa huduma muhimu zikiwemo masuala ya mafuta,gesi,mizigo na uvuvi wa kisasa.

Naibu Katibu Mkuu huyo alisema lengo la ziara hiyo ya Sekretariet ni kukagua utekelezaji wa Ilani ya CCM, kuangalia uhai wa Chama pamoja na kuzungumza na Wana CCM kwa ngazi za Mashina.

Dk.Mabodi,aliyefuatana na Wajumbe mbalimbali wa Sekretariet alitembelea na kukagua mradi wa upanuzi wa gati bandari ya Mkokotoni,mradi wa maboresho ya bandari Bumbwini na Pangatupu na mradi wa kilimo cha umwagiliaji.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.