Habari za Punde

Wazee Wanaume Watakiwa Kukumbukwa na Serikali Kama Kundi Maalumu.


Na Hamida Kamchalla, Tanga.

IMEELEZWA kwamba moja ya malengo ya kuanzishwa kwa Chama Cha Wazee Wanaume nchini ni kutaka wapatiwe haki zao za msingi kutokana na kusahaulika katika jamii na serikali kama ilivyo kwa makundi mengine maalumu.

Kauli hiyo imetolewa na kiongozi mkuu wa chama hicho Thadei Mchena alipozungumza  kuhusu uanzishwaji wa chama na manufaa wanayopata wazee hao ndani ya chama.

Amesema malengo ya chama ni mengi ndani ya katiba yao lakini hilo ndiyo kubwa lililopelekea likaja wazo hilo kwani serikali imekuwa ikiwajali sana Wanawake, vijana na walemavu huku ikiwasahau wazee wanaume katika nyanja mbalimbali.

"Mbali na malengo kadhaa yaliyopo katika katiba yetu ya chama, pia ni kuwawezesha wazee hawa watambulike na serikali yetu kwani imewasahau na kutowatetea katika nyanja mbalimbali kama vile inavyowatambua wanawake, vijana na walemavu, serikali imewawekea makundi haya ruzuku ya mikopo lakini wazee wanaume wamesahaulika" alibainisha Mchena.

"Lakini pia chama kinawalinda na kuwajali wazee na kuhakikisha wanatendewa haki katika familia zao ikiwa ni pamoja na kuwapatia huduma muhimu kama vile afya bila malipo kama sera ya mwaka 2003 ilivyoelekeza" amesema.

Aidha Mchena amebainisha kwamba wameandaa mpango mkakati wa kuanzisha miradi mbalimbali ya ufugaji, uvuvi na kilimo vya kisasa ili kuwawezesha wazee hao kutokuwa tegemezi katika jamii ikiwa ni pamoja na kuwapatia elimu ya afya kwa kuyajua kagonjwa na jinsi ya kujikinga.

"Kutakuwa na kitengo maalumu cha kuwapa ushauri kuhusu magonjwa na namna ya kuyaepuka kama vile ukimwi, Uviko 19, kifua kikuu, kisukari pamoja na tezidume, kuanzishwa miradi mbalimbali lakini pia kuhakikisha wanakuwa na makazi yao wenyewe na siyo makambi" amesema.

Hata hivyo amefafanua kwamba wanaojiandikisha kwenye chama hicho ni wale wanaoanzia miaka 50 kwakuwa chama kinapaswa kuwa na vijana wazee wenye nguvu za kushuhulikia baadhi ya mambo kama kuanzisha miradi lakini pia kuwasimamia na kuwaongoza wazee katika shuhuli mbalimbali.

"Tumeweka wanaume kuanzia miaka 50 kwa makusudi ili kuwepo na vijana wazee wa kuweza kutumwa kazi mbalimbali na kuanzisha miradi ya uzalishaji mali katika kuwakwamua wazee ikiwa ni pamoja na kuwakilisha maoni ya wazee katika ngazi mbalimbali" amefafanua.

Hata hivyo Mchana amebainisha kwamba chama hicho makao makuu yake yako mkoani Arusha na kimeweka matawi yake katika Mikoa ya Tanga, Manyara, Singida, Dar es salaam, Mwanza, Mbeya na Iringa na kimesajiliwa na serikali tarehe 5, Octoba, 2021 kwa usajili namba S/A/ 22527.

"Chama kinaendelea kutoa huduma mbalimbali kwa wazee wanaume, hivyo wito wangu kwa wale ambao hawajajiandikisha, popote pale walipo kwenye Mikoa niliyotaja wajitokeze kujiandikisha kwenye chama hiki ili wapate haki zao za msingi" ameongeza.

2 comments:

  1. Wazee Wanaume Tanzania tutambue kwamba jambo la kujiunga pamoja na kujadili changamoto zetu za Afya, Uchumi, Makazin.k. hatujachelewa, wakati ni huu, wakati ni sasa.
    *WAZEE NI TUNU TUWATUNZE*
    Mwenyekiti CCWWT Mkoa wa Tanga.
    Ramadhani Maselle.

    ReplyDelete

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.