Habari za Punde

DKT. CHAULA AKABIDHIWA OFISI RASMI NA DKT JINGU

Na WMJJWM Dodoma

Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dkt. Zainabu Chaula amekabidhiwa rasmi Ofisi ya Wizara na aliyekuwa Katibu Mkuu Wizara ya Afya Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii ambaye kwasasa ni Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Dkt. John Jingu.

 

Makabidhiano hayo yamefanyika katika Ofisi za Wizara jijini Dodoma baada ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan,  kuiunda Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum.

 

Akizungumza katika hafla ya makabidhiano hayo, Katibu Mkuu wa Wizara Dkt. Zainabu Chaula, amewataka watumishi wa Wizara hiyo kutimiza majukumu yao kwa ufanisi na kujituma katika kutekeleza majukumu yao.

 

"Kila mmoja hapa ana karama yake, sasa tuunganishe hayo Maarifa ya mtu mmoja mmoja tutembee pamoja" Dkt. Chaula

 

Ameongeza kuwa, kiongozi ni wasifu katika eneo analofanya kazi na kuleta matokeo chanya kwenye eneno la utekelezaji wa majukumu yao hivyo, ni vyema kuhakikisha wanatumia vipawa vyao kusadia kutatua changamoto zilizopo katika jamii.

 

"Tutumie ujuzi na uwezo wote tulionao kuhakikisha tunasaidiana katika kutekeleza majukumu yetu kwa ufanisi na ufasaha ili kuleta matokeo chanya" alisema Dkt. Zainabu Chaula.

 

Kwa upande wake, aliyekuwa Katibu Mkuu Wizara ya Afya Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii ambaye ni Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Dkt. John Jingu amewashukuru Watumishi wa Wizara hiyo mpya kwa ushirikiano waliompa wakati akitekeleza majukumu yake na kuwaasa kuendelea kuwapa ushirikiano viongozi wapya katika utekelezaji wa majukumu waliyopewa na Rais.

 

"Nawaahidi nitaendelea kuwapa ushirikiano katika utekelezaji wa majukumu yenu tuendelee kutekeleza majukumu yetu kwa ufanisi ili  kumsaidia Rais katika kutatua changamoto za kimaendeleo " alisema Dkt. Jingu

 

Akizungumza katika hafla hiyo, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Amon Mpanju, amewaasa watumishi kupendana na kushirikiana kwa pamoja katika majukumu yao ili kuwasaidia Viongozi kuendeleza jukumu la Maendeleo.

 

Mapema Januari 8, 2022, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Samia Suluhu Hassan, aliunda Wizara mpya ya Maendeleo ya Jamii Jinsia Wanawake na Makundi Maalum na kisha kuteuwa Viongozi wa kuingoza Wizara hiyo.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.