Habari za Punde

Spika Dkt. Tulia Awataka Wabunge Kumsaidia Rais Samia Kutekeleza Vipaumbele Vyake.

Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Tulia Ackson (Mb), amefungua semina ya mafunzo ya kuwajengea uwezo Wajumbe wa Kamati ya Uongozi, Makamu Wenyeviti wa kamati na Tume ya Utumishi wa Bunge ambayo inafanyika katika Ofisi ndogo za Bunge zilizopo Tunguu Zanzibar.

Akizungumza kwenye semina hiyo, Mhe. Spika Dkt. Tulia amewataka Wabunge, kupitia mafunzo hayo wafahamu ya kwamba wanalo jukumu kubwa na muhimu la kumsaidia Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan katika kutekeleza vipaumbele vyake alivyoviahidi kwa Wananchi.

“Ninyi nyote ni mashahidi kwamba Serikali yetu ya sasa inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan ilishasema vipaumbele vyake wakati alipokuja Bungeni, vile vipaumbele alivyovieleza basi sisi kama Wabunge ni kazi yetu kuhakikisha mambo yanayoletwa kwenye kamati zetu yanazingatia vipaumbele vyake.” Alisema Mhe. Spika

“Mheshimiwa Rais hawezi kuwa kila siku anajua kwamba kila sekta fulani imeleta jambo gani Bungeni lakini sisi Wabunge kama wawakilishi wa Wananchi ndio tuliahidiwa kwa yale aliyoyasema katika hotuba yake, sasa ili tuhakikishe Serikali inayafanya yale ambayo Mheshimiwa Rais aliyasema kwamba ndio vipaumbele vyake basi Serikali inayatekeleza na ndio maana tupo hapa kwenye hii semina.”alisema Spika Dkt. Tulia

Amesisitiza “Mtakumbuka siku mliponipa heshima ya mimi kuwa Spika nilisema kwamba Bunge letu ni daraja kati ya Wananchi na Serikali na naamini mafunzo haya yatatujengea uwezo wa kufanya kazi vizuri kama Bunge ikiwa ni pamoja na kuwafanya wale tunao waongoza sisi kama daraja baina yao na Serikali” Mhe. Spika

Pamoja na hayo yote, Mheshimiwa Spika, amewataka washiriki wote kuhakikisha wanatumia nafasi hiyo ya mafunzo vizuri ikiwa ni pamoja na kujenga mahusiano bora baina yao na watumishi wengine wa taasisi mbalimbali ikiwemo Bunge na Serikali.

“Tunaamini kila mmoja wenu baada ya kumaliza mafunzo haya ataweza kusimamia kikamilifu sheria, kanuni na taratibu za Bunge na mtakuwa kioo kuzingatia miiko ya uongozi na utawala bora, tunaamini watu watajifunza mengi kutoka kwenu” Spika Dkt. Tulia

Kwa upande wake Spika wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar Mhe. Zuber Ali Maulid, amemueleza Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Tulia Ackson ya kwamba Baraza lake litahakikisha linashirikiana vyema na Bunge lake katika Nyanja mbalimbali za kiutendaji ili kufanikisha adhma ya Serikali ya Tanzania.

Imetolewa na Ofisi ya Bunge

21.02.2022

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.