Habari za Punde

Tuendeleze Umoja wa Kidiplomasia Kukuza Fursa za Maendeleo - Mhe Othman Masoud.

 

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe.Othman Masoud Othman akizungumza na Balozi wa Jamhuri ya Kenya anayemaliza muda wake Nchini Tanzania Mhe.Dan Kazungu, alipofika Ofisini kwake kwa mazungumzo na kuaga baada ya kumaliza muda wake Nchini. 
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Othman Masoud Othma  akizungumza na Balozi wa Saudi Arabia Nchini Tanzania Sheikh.Abdullah bin Aliy Al Sheryan, alipofika Ofisini kwake Migombani kwa mazungumzo yaliofanyika leo. 


Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mheshimiwa Othman Masoud Othman, ameitaka Saudi Arabia kuendeleza umoja wa asili uliopo kati yake na Zanzibar, ili kukuza fursa za maendeleo baina ya pande mbili hizo.
Mheshimiwa Othman ameyasema hayo leo Ofisini kwake Migombani, Jijini hapa akiongea na Balozi wa Saudi Arabia nchini Tanzania, Sheikh Abdullah bin Aliy Alsheryan, aliyewasili hapo ili kujitambulisha.
Amesema Saudi Arabia na Zanzibar, zimekuwa na fungamano na udugu wa asili katika nyanja zote za maisha zikiwemo elimu, utamaduni na maisha ya jamii ambapo ni vigumu hata kubaini zama ambazo mahusiano hayo yalianza.

“Ni vigumu kuelewa ni lini mahusiano haya yalipoanza, kwani hakuna mtaa ambao utakosa mtu aliyefungamana na Saudia, na pia ni vigumu kuona msikiti ambao anakosekana mtu ambaye kasomea katika Nchi hiyo”, amesema Mheshimiwa Othman.

Mheshimiwa Othman amebainisha njia ambazo fungamano hilo linaweza kuendelezwa, na hivyo kufanikisha maendeleo kati ya watu wa pande mbili hizo, zikiwemo fursa za kuhamasisha huduma za kijamii ambazo ni pamoja na usimamizi wa mali za wakfu, sekta ambayo Zanzibar iliianzisha miaka mingi iliyopita.

Aidha Mheshimiwa Othman ameihakikishia Saudi Arabia akisema kwamba milango ya Zanzibar iko wazi katika kusaidiana na kushikamana, ili kukuza mahusiano mema na udugu wa asili baina ya pande mbili hizo muhimu.

Naye Balozi wa Saudi Arabia nchini Tanzania, Sheikh Abdullah Alsheryan, amesema kuwa azma ya nchi yake ni kuendelea kuiungamkono Zanzibar na Tanzania kwa ujumla ili kuhamasisha na kusaidia maendeleo ya watu wake katika sekta mbali mbali.

Amesema sekta hizo ni pamoja na kusaidia upatikanaji wa fursa za kitaaluma na nafasi za masomo katika ngazi mbali mbali, ili kuongeza kiwango cha wahitimu wa Nchi hii, wanaofadhiliwa na Taifa hilo.
Katika ujumbe wake, Balozi Alsheryan aliongozana na watendaji wake mbali mbali akiwemo Mkuu wao wa Itifaki, Sheikh Muhamed Alzabin.
Wakati huo huo, Mheshimiwa Othman amekutana na Balozi wa Jamhuri ya Kenya anayemaliza muda wake nchini, Mheshimiwa Dan Kazungu, aliyefika ofisini hapo kwaajili ya kuaga.
Katika kikao chake na Balozi huyo, Mheshimiwa Othman amesema kuwa pamoja na changamoto nyingi Nchi mbili hizo zinazozipitia, bado zipo fursa kadhaa za maendeleo baina yao zikiwemo za biashara, kilimo na utalii ambazo kupitia mashirikiano mema zinaweza kuchangia kujikwamua kiuchumi.
Pamoja na salamu zake kwa watu wa Kenya, Mheshimiwa Othman amemtakia dua Balozi Kazungu, huku akimtaka aendelee kuyakumbuka mema yote aliyoyapata alipokuwa katika kipindi cha utumishi wake hapa nchini.
Akitoa shukran zake, Balozi Kazungu ameeleza kuwa pamoja na mafanikio mengine, Zanzibar imeionyesha njia Jamhuri ya Watu wa Kenya katika kujenga amani, utulivu, umoja na mshikamano, kupitia maridhiano ya kisiasa.
Balozi Kazungu ambaye ameishi na kukulia katika Ukanda wa Pwani ya Kenya amesifia mazingira ya sasa ya Zanzibar na Tanzania kwa ujumla, ambayo amesema yanatoa fursa kwa wananchi wake, na hata kutoka majirani wa Afrika ya Mashariki, kushikamana na kujiletea maendeleo.
Kitengo cha Habari
Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar.
23/02/2022

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.