Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi Mhe. Rahma Kassim Ali amesema Serikali ya Mapinduzi Zanzibar inatambua na kuthamini mchango unaotolewa na ushirika wa madereva wa Taxi uwanja wa ndege katika kukuza hadhi na haiba ya uwanja wa ndege wa kimataifa wa Zanzibar.
Mkurugenzi utumishi na Uwendeshaji Dk. Shaaban Hassan Haji alieleza hayo kupitia hotuba alioisoma kwa niaba ya Waziri wa ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi katika hafla ya mkutano wa 11 wa ushirika wa madereva wa Taxi uanja wa ndege uliofanyika katika ukumbi wa mkutano wa Ushirikahuo huo uliopo kiembe samaki Jijini Zanzibar.
Aidha Mhe. Waziri aliwashauri wanaushirika wa umoja huo wa madereva kuendeleza na kuimarisha huduma zao kwa kuwa na mashirikiano ya karibu na mamlaka ya viwanja vya ndege ili kuendelee kuwahudumia na kuwahakikisha usalama wa wageni.
Kuhusiana na kupewa fursa za kutoa huduma katika viwanja vyote Mhe. Waziri ailwataka madereva hao kuwa wavumilivu na aliwahakikishia mkakati wa kuhamia jengo jipya la uanja wa ndege utakapokamilika serikali itazingatia na kutoa kipaombele kwa ushirika huo baada ya wizara kujiridhisha kwamba ushirika huo una uwezo na vigezo vya kutoa huduma bora.
“Niseme tu ni lazima ushirika ujipange zaidi ili dhamana mtakayopewa muweze kuitekeleza kwa ufanisi na viwango vinavyotakiwa”Alisema Mhe. Waziri.
Pamoja na mambo mengine, Mhe. Waziri aliwahakikishia wanaushirika hao suala la malipo ya fidia litafanyika baada ya Wizara kufanya uhakiki wa deni hilo na kijiridhisha.
Akisoma risala kwa niaba ya wanaushirika Ndg. Maryam Said Soud alimuomba Mhe. Waziri kupitia wizara anayoisimamia kuendelea kuwapa fursa na kuwaamini kwa kuwapa nafasi ya kutoa huduma katika viwanj vyote kwani uwezo walionao ni wa kuridhisha.
Sambamba na hayo, Ndg. Maryam alimuomba Mhe. Waziri kutoa msukumo wa kulipwa fedha wanazodai ambazo zilitumika kwa ajili ya ujenzi wa vyoo katika eneo la uegeshaji wa magari.
Akigusia changamoto zinazowakabili alisema ni uwelewa mdogo pamoja na ufinyu wa elimu ya ujasiliamali jambo linalosababisha kutofikiwa kwa malengo ya ushirika huo katika kuwaingizia kipato wanachama wake.
Ushirika wa madereva wa Taxi Uwanja wa ndege umeanzishwa februari 2003 na una jumla ya wanachama mia moja na hamsini na tano (155) wakiwemo wanawake Arobaini (40) na wanaume mia moja na kumi na tano (115).
No comments:
Post a Comment