Habari za Punde

Watumishi wa Umma Kufanyakazi kwa Kuzingatia Haki na Uadilifu kwa Kutambua Dhima kubwa Waliyonayo kwa Mwenyezi Mungu.- Alhaj Dk. Mwinyi.

                                                                      

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk. Hussein Ali Mwinyi akizungumza na kuwasailimia Waumini wa Dini ya Kiislam baada ya kumalizika kwa Sala ya Ijumaa iliyofanyika katika Masjid Qudus Kijitoupele Wilaya ya Magharibi “A” Unguja.(Picha na Ikulu)

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa    Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk. Hussein Ali Mwinyi amewataka watumishi wa umma kufanya kazi kwa kuzingatia haki na uadilifu kwa kutambua dhima kubwa waliyonayo kwa Mwenyezi Mungu.

Alhaj Dk Mwinyi amesema hayo kwa waumini wa Dini ya kiislamu baada ya kukamilika kwa sala ya Ijumaa iliofanyika Masjid Al - Qudus uliopo Kijitoupele Jijini Zanzibar.

Alisema watumishi wa  umma wana wajibu wa kufanya kazi  kwa kuzingatia uadilifu na kutambua nafasi walizokabidhiwa ni dhima kubwa kwa Mwenyezi Mungu, hivyo wanapaswa kufanya haki na kuondokana na dhulma.

Aliwataka watumishi hao kuondokana na dhana iliojengeka miongoni mwao kuwa mali ya Serikali haina mwenyewe.

Alisema Serikali inahitaji fedha kwa ajili ya kuendeleza kazi za maendeleo, hivyo akatowa wito kwa wafanyakazi wa Serikali pamoja na wafanyabiashara kuwa waadilifu, hususan katika suala la ulipaji wa kodi.

“Wafanyakazi wa Serikali na wafanyabiashara  sote tufanye kazi ya kuisaidia Serikali “, alisema.

Aidha, aliwataka wananchi kufahamu kuwa shughuli mbali mbali za maendeleo zinazoendelea kufanyika katika maeneo mbali mbali ya nchi pamoja na hatua za kuwajibisha  Watendaji wa Serikali, zinafanyika kwa nia njema ili kuleta ustawi mwema wa taifa.

Alhaj Rais Dk. Mwinyi alishangazwa na mitazamo ya baadhi ya wananchi kuhusiana na uzungushwaji wa mabati katika maeneo ya miradi mbali mbali inayoendelezwa na kusema hayo yanafanyika kwa nia njema kwa lengo la kuliletea Taifa maendeleo, kupitia sekta mbali mbali, ikiwemo elimu na afya.

“Nia na dhamira ya Serikali ni njema,……. ni kujenga nchi”, alisema.

Alhaj Dk. Mwinyi alirejea kauli yake ya kuwaomba Wazanzibari kuendelea kumuombea dua ili aweze kutekeleza yale yote aliyoyaahidi pamoja na kutenda haki katika utekelezaji wa majukumu yake.

Nae, Katibu wa Mufti wa Zanzibar Sheikh Khalid Ali Mfaume amewataka wananachi kwa ujumla kuwa na imani na Viongozi wao wakati huu wakitekeleza ahadi, sambamba na kusisitiza umuhimu wa kumuombea dua Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Alhaj Dk. Hussein Mwinyi..

Mapema Khatibu wa Sala hiyo ya Ijumaa, Sheikh Idd Hussein  aliwataka waislamu kujikita katika kutafuta uchamungu kwa kufanya mambo mema na kubainisha mambo manane muhimu, ikiwemo la  suala la uadilifu katika dhamana wanazokabidhiwa.   

Imetayarishwa na Kitengo cha Habari,

Ikulu Zanzibar.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.