Habari za Punde

Wenye Nyumba Zinazohitaji Kufanyiwa Matengenezo Jijini Tanga Wapewa Miezi Mitatu Kuzirekebisha.

Na Hamida Kamchalla, Tanga.

MEYA wa jiji la Tanga Abdulrahman Shillow ametoa miezi mitatu kwa wananchi wakazi wenye majengo machakavu, machafu ndani ya  jiji hilo kuyafanyia ukarabati au kutumia njia yoyote ili kuyaondoa kwani maeneo yote yanatakiwa kuletahadhi ya jiji.

Shillow ameyasema hayo  kwenye baraza la madiwani robo ya pili kwa maka wa fedha 2021/22 ambapo alitoa taarifa kwa umma na wasafirishaji wote ndani ya jiji la Tanga.

"Wasafirishaji wote ni lazima waanze na kumalizia safari zao kwa kupita stendi kubwa ya Kange na kwa wale wenye stendi ndogo ambao wamekidhi vigezo ni lazima wapitie Kange kwa dakika 15 kabla ya muda wa kuondoka na ni lazima wakirudi wapitie pale" alisema.

"Aidha majengo mabovu, machafu, au yaliyochoka ambayo yapo katikati ya jiji yanayoharibu taswira ya jiji yanapewa miezi mitatu aidha yafanyiwe uwekezaji, yauzwe au yarekebishwe ili yaendane na hadhi ya jiji letu" alisisitiza Shillow.

Hata hivyo ameiomba ofisi ya Mkurugenzi wa jiji hilo kufanya tathmini ya miradi ambayo ni viporo kwani baraza lake limedhamiria kumaliza miradi hiyo kwa wakati na kuepuka kuendelea kulaza miradi kwa mwaka mwingine.

"Ndugu Mkurugenzi, baraza hili lina nia ya dhati kumaliza miradi yote viporo, kwasababu hiyo basi, nikuombe kwa niaba ya baraza ufanye tathmini ya miradi yote viporo katika kata zote na tupewe tathmini ya kila mradi na jumla ya thamani ya miradi yote ili tuweke mpango kazi y umalizia miradi hiyo kwa wakati" alieleza.

Aidha Shillow amebainisha kwamba jiji la Tanga kwa mwaka wa fedha 2021/2022 imelenga kuboresha vyanzo vya mapato vilivyopo na kuanzisha vingine ili kuzidi kuongoza katika ukusanyaji wa mapato yake ya ndani kwa kipindi cha robo ya tatu ya mwaka inayokuja.

Awali kabla ya baraza hilo, Meya aliongea kuhusu taarifa iliyotolewa January 28,2022 na Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) katika kipindi cha mwezi julai hadi Disemba, 2021 ambapo jiji hilo limeshika namba moja katika ukusanyaji wake wa mapato ya ndani ikivuka lengo lake la asilimia 50 na kufikia asilimia 56.

"Lengo letu ni kuboresha vyanzo vya mapato vilivyopo ili tukusanye vizuri lakini pia tumejipanga kuanzisha vyanzo vingine vya mapato vilivyopo Moja wapo ni jengo la kitega uchumi lililopo kwenye stand kuu ya mabasi , kuanzisha machinjio ya Kisasa, kujenga soko kubwa na la kisasa  katika eneo la kata ya Pongwe ambalo litakuwalinauza mazao ya jumla" alisema Shillow.

"Tuna mipango ya muda mrefu ikiwa ni pamoja na kuboresha masoko yetu yaliyopo  ili kuepuka ile mianya ya upotevu wa fedha za halmashauri yetu ya jiji la Tanga, lengo letu ni kujiwekea katika nafasi nzuri na kuwa namba Moja katika ukusanyaji wa mapato ya ndani" aliongeza.

Aidha Halmashauri ya jiji la Tanga kuwa miaka mitano imejiwekea malengo ya kukusanya shilingi bilioni 20 kutoka shilingi bilioni 15 inazozikusanya kwa sasa ikiwa ni sawa na kiasi ya shilingi bilioni moja kila mwaka ili kuzidi kutatua changamoto kwa jamii.

Mstahiki Meya huyo ameongeza kuwa kwa kuzingatia dhamira ya Jiji hilo kuzidi kuboresha upatikanaji wa huduma kwa jamii wafanyabiashara wanatakiwa  kutoa ushirikiano kwa kulipa kodi kupitia mifumo iliyoelekezwa na serikali.

"Maendeleo ya mahali popote hayapatikani isipokuwa kwa kupitia kodi sisi kama halmashauri tunaendeleza kuto elimu kuwa wananchi wafahamu umuhimu wa kulipa kodi , niwaombe Wananchi na wafanyabiashara walipe kodi bila shuruti wasikubali kununua au kuuza bidhaa bila ya kupewa risiti tena kwa mifumo iliyoelekezwa na serikali"

Hata hivyo halmashauri hiyo kwa mwaka wa fedha 2021/2022 imeomba kuongezewa bajeti kutoka bilioni 15. inazozikusanya kwa sasa na kuifikia shilingi bilioni 16.

"Ni matarajio ya Baraza letu la madiwani kuwa ndani ya miaka mitano mpaka ifikia 2025  ni kufika bilioni 20 katika ukusanyaji wa mapato yetu ya ndani kutoka shilingi bilioni 15 tunazokusanya kwa sasa na inawezekana maana sasa hivi jiji letu linakuwa" alisema mstahiki Meya.

Halmashauri ya jiji la Tanga katika kipindi cha robo ya pili ya mwaka wa fedha wa kutoka mwezi july hadi december 2021 iliibuka namba Moja kwa ukusanyaji wa mapato ya ndani ikiyashinda majiji ya Dar es salaam, Mwanza, Dodoma, Arusha na Mbeya.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.