Habari za Punde

Amani ni Tunda la Imani Alhaj Othman.

 

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Alhaj Othman Masoud Othman akizungumza na kuwasalimia Waumini wa Masjid Rahmaan Mtoni Marine Wilaya ya Magharibi A Unguja baada ya kumalizika kwa Sala ya Ijumaa iliyofanyika katika Masjid hiyo leo 11-3-2022.

Wananchi wa Mtoni wakimsikiliza Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Alhaj Othman Masoud Othman akizungumza na kuwasalimia baada ya kumalizika kwa Sala ya Ijumaa iliyofanyika katika Masjid Rahmaan Mtoni Marine.

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mheshimiwa Alhaj Othman Masoud Othman, amesema amani ni tunda la imani ambalo misingi yake ni muhimu kwa ustawi bora wa jamii na ujenzi wa Taifa la watu wenye maadili.

Alhaj Othman ameyasema hayo, wakati akitoa salamu zake kwa waumini, mara baada ya kujumuika katika Ibada ya Swala ya Ijumaa, Masjid Rahmaan, Msikiti uliopo Mtoni Marine, Wilaya ya Magharibi A, kisiwani Unguja, sambamba na ziara yake katika Chuo cha Wanawake cha Al-salaam.

Mheshimiwa Alhaj Othman, amesema kati ya uwekezaji bora kwa ngazi zote za jamii, ni pamoja na kuwekeza katika mbegu ya imani, ambayo ni njia kuelekea uzalishaji na upatikanaji wa raia wema, wafuasi wema, na hatimaye viongozi wema.

Alhaj Othman ameeleza kuwa kumjenga, kumkuza na kumuendeleza mwanamke, ikiwemo kumpatia taaluma sahihi na mbinu za ujasiriamali, ni sawa na kuikuza jamii, nchi na kulijenga Taifa kwa ujumla chini ya misingi ya maendeleo na maadili.

Mheshimiwa Alhaj Othman pamoja na kupongeza juhudi zinazochukuliwa na Jumuiya ya Al-salaam, ambayo amesema imetoa changamoto na kuonyesha mfano wa kuigwa katika kuhamasisha ustawi bora wa jamii na maendeleo ya nchi, pia ametoa wito kwa Misikiti isiishie na kamati pekee, bali iweke mkazo katika malezi mema ya watoto.

Akitoa khutba mbili kabla ya Swala ya Ijumaa hii, Khatib Sheikh Khamis Ibnu Khamis ameeleza umuhimu wa ‘infaaq’, kutoa sadaka na kuwasaidia wanyonge, kwa kutarajia kheri na malipo mema kutoka kwa Mwenyezi Mungu, hasa ndani ya msimu wa Miezi hii Mitukufu.

Katika salamu zake mbele ya hadhira ya Mheshimiwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Viongozi na Wanachuo, Katibu wa Jumuiya ya Al-salaam Sheikh Hassan Rashid Mohamed amesema hatua ya mafunzo ya imani na ujasiriamali kwa akinamama chuoni hapo imelenga katika ukombozi wa kweli wa mwanamke na kwa nyanja zote za maisha ya jamii, ndani na nje ya Zanzibar.

Chuo hicho kinachosimamiwa na Jumuiya ya Al-salaam, kilichopo pia jirani na Mitaa ya Mtoni Marine, kinachowajumuisha wanafunzi wanawake kutoka Unguja na Pemba, Tanzania Bara na Nchi za jirani, kimekuwa kikiendesha mafunzo mbali mbali yakiwemo ya Dini ya Kiislamu na fani kadhaa za ujasiriamali.

Kitengo cha Habari,
Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanziabr,
Tarehe 11/03/2022.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.