Habari za Punde

Kamati Ya Kudumu Ya Viwanda, Biashara Na Mazingira Ya Bunge La Jamhuri Ya Muungano Wa Tanzania

Mkurugenzi wa Kitengo cha Ununuzi na Ugavi kutoka Ofisi ya Makamo wa Rais Bi Juliana Mkalimoto akiangalia mradi wa majiko sanifu yenye kutumia kuni kidogo kwenye nyumba ya Bi Tatu Zaja Haji wa Kijiji cha Matemwe ukiwa ni mradi wa kuhimili mabadiliko ya tabia nchi kwa kutumia ekolojia (EBA) unaosimamiwa na Ofisi ya Makamo wa Rais Muungano na Mazingira kwa kushirikiana na Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais- Zanzibar

Mwenyekiti wa  Kamati ya Kudumu ya Viwanda, Biashara na Mazingira ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe David Mwakiposa Kihenzile akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Matemwe kutoka Shehia ya Kijini, Mbuyutende na Jugakuu Wadi ya Kijini Wilaya ya Kaskazini ‘A’ ikiwa ni ziara ya kutembelea maeneo ya mradi wa kuhimili mabadiliko ya tabia nchi kwa kutumia ekolojia (EBA) unaosimamiwa na Ofisi ya Makamo wa Rais Muungano na Mazingira kwa kushirikiana na Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais - Zanzibar         


Na RAYA HAMAD –OMKR                                                                                                           

Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Viwanda, Biashara na Mazingira ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe David Mwakiposa Kihenzile amesema wajibu wa bunge ni kushauri Serikali, kusimamia Serikali na kutunga sheria hivyo wanawajibu mkubwa kuhakikisha miradi ya wananchi inatekelezwa

Amesema ni lazima kufahamu miradi ya Serikali iliyopitishwa na kuifatilia, kuona kwa macho miradi inayotekelezwa ili maendeleo ya wananchi yaweze kufikiwa kwa wakati hivyo Kamati yao inawajibu wa kushauri, kuona changamoto za maendeleo ya miradi na kutoa mapendekezo ya hatua zinazopaswa kuchukuliwa

Mhe Mwakiposa amesema pamoja na kuwa bado hawajafanya majumuisho lakini katika miradi yote waliyoitembelea Zanzibar wameridhishwana kwa kazi nzuri iliyofikiwa na inayoendelea ya utekelezaji wa maendeleo ya miradi hio

“Ni ziara ya mafanikio na tumepata ushirikiano mzuri kutoka Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais na pia tumepata kuona hali halisi kutoka kwa wananchi wenyewe changamoto zao, mafanikio na matumaini yao juu ya Mradi huu” alisisitiza Mwakiposa  

Nae Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mhe Khamis Hamza Khamis Chilo ambae ameongozana na Kamati ya Kudumu ya Viwanda, Biashara na Mazingira ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania amesema lengo la kufanya ziara ya kuitembelea miradi ya maendeleo ni kuhakikisha kuwa miradi iinakamilika kwa wakati na wanufaika wake ni wananchi

Chilo amesema Mradi huu pia lengo lake ni kusaidia kuhimili mabadiliko ya tabianchi, kwa kurejesha uoto wa asili kwa kutumia mfuko wa ikolojia, kutoa elimu juu ya kilimo chenye kustahamili athari za mabadiliko ya tabianchi na kuwajengea uwezo wanajamii juu ya njia mbadala za kujipatia kipato ambacho hakiathiri mazingira

Nao baadhi ya wananchi waliofikiwa na mradi wa EBA akiwemo sheha wa shehia ya Mbuyutende Bw Khamis Juma Khamis wameishukuru Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na Jamhuri wa Muungano wa Tanzania kwa kuwafikishia miradi ya maendeleo katika kijiji chao jambo ambalo limewapa mwamko na kuamsha ari ya maendeleo katika kutunza na kuhifadhi mazingira kwa vile wamefahamu kuwa ni njia moja wapo ya kuwasaidia kujiinua kiuchumi kupitia uhifadhi wa mazingira

“Awali hatukuwa tukifahamu umuhimu wa miti hii inayotuzunguka hapa kijijini kwetu tuliikata na kufanyia shughuli nyengine za kijamii ambazo ziliharibu mazingira yetu lakini sasa baada mradi kutufikia na kupata elimu tumeelewa na kufahamu umuhimu wake kwani kipato kinaongezeka” alisema Bi Fatma Omar Juma wa Kikundi cha utengenezaji wa sabuni na vipodozi Matemwe Kijini

Kamati iliyotembelea kiwanda cha kampuni ya Green kilichopewa dhamana ya kutengeneza boti za mradi kilichopo Fumba, kuangalia na kupata maelezo ya kazi za vikundi vya utengenezaji sabuni na vipodozi visivyotumia kemikali ikiwemo liwa, mafuta ya kujipaka kwa kutumia majani ya mchaichai, mkaratusi, karafuu na miti mengine ya asili kilichopo Kijiji cha Matemwe pamoja na kuona majiko sanifu la kuni kidogo kijijini hapo

Kwa upandea wa Ofisi wa Makamu wa Rais ziara hio imeongozwa na Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais Dkt Omar D. Shajak, Mkurugenzi Mkuu Mamlaka ya Usimamizi wa Mazingira ndugu Sheha Mjaja na Mkurugenzi Idara ya Mazingira Bi Farhat Mbarouk na baadhi ya watendaji wa Ofisi hio.

Awali kabla ya kuanza ziara yao kamati hio walionana na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais Mhe Harusi Saidi Suleiman na kuelezea matumaini yake baada ya ziara hio pamoja na kumuomba Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mhe Khamis Hamza Khamis Chilo kupitia Ofisi yake kuendelea kutafuta miradi mengine utunzaji na uhifadhi wa mazingira kwani maeneo mengi yameharibiwa kutokana na mabadiliko ya tabianchi.

Kamati ya Kudumu ya Viwanda, Biashara na Mazingira ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imetembelea Fumba kwenye kiwanda cha kutengeneza maboti ya mradi huo kinachoitwa Fumba Marine Service kinachomilikiwa Visiwani Traders,

Aidha walifika Kijiji cha Matemwe kutoka Shehia ya Kijini, Mbuyutende na Jugakuu Wadi ya Kijini Wilaya ya Kaskazini ‘A’ ikiwa ni ziara ya kutembelea maeneo ya mradi wa kuhimili mabadiliko ya tabia nchi kwa kutumia ekolojia (EBA) unaosimamiwa na Ofisi ya Makamo wa Rais Muungano na Mazingira kwa kushirikiana na Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais – Zanzibar

Mradi wa EBA ni wa miaka mitano unatekelezwa ndani ya Mikoa mitano kwenye Wilaya tano ambapo kwa upande wa Tanzania Bara ipo kwenye mikoa minne ikiwemo Wilaya ya Simanjiro, Wilaya ya Kishapu, Wilaya ya Mpwapwana Wilaya ya Mvumero na kwa Zanzibar ni Mkoa wa Kaskazini ndani ya Wilaya ya Kaskazini “A” katika Shehia za Matemwe Kijini, Mbuyutende, na Jukakuu Wadi wa Kijini.

.

 

 

 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.