Habari za Punde

Mashirikiano yatasaidia kutatua changamoto za wakulima wa Viungo, Mbogamboga na Matunda

Baadhi ya washiriki wakiendelea na mkutano huo.

Mwakilishi wa Umoja wa Ulaya EU.Bi. Anna Costantin akizungumza wakati wa mkutano wa kikundi kazi cha kiufundi kwa taasisi zinazotekeleza mradi wa kilimo cha viungo, mbogamboga na matunda chini ya mpango wa Agri-Connect Tanzania uliofanyika mkoani Iringa. 

TAASISI zinazotekeleza miradi ya mazao ya viungo, mboga mboga na matunda (Agri-connect) zimetakiwa kuongeza mashirikiano katika utekelezaji wa kazi zao ili kutatua changamoto zinazowakabili wakulima Tanzania Bara na Zanzibar.

Wito huo umetolewa na mwakilishi wa Umoja wa Ulaya, Anna Costantini kwenye mkutano wa kikundi kazi cha kiufundi kwa taasisi zinazotekeleza mradi wa kilimo cha viungo, mbogamboga na matunda chini ya mpango wa Agri-Connect Tanzania uliofanyika mkoani Iringa. Kikundi kazi hicho kinahusisha wataalamu pia kutoka Wizara za Fedha na Kilimo kutoka Tanzania Bara na Zanzibar pamoja na wawakilishi kutoka Shirika la chakula na kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO).  

Bibi Anna alieleza kwamba changamoto nyingi zinazowakabili wakulima katika maeneo mbalimbali zinafanana, ni muhimu watekelezaji hao kufanya kazi kwa karibu katika kila hatua wakati wa kuzitatua changamoto hizo, ili kupata matokeo ya pamoja.

Mradi wa Agri-Connect unatekelezwa na taasisi tofauti zikiwemo People’s Development Forum (PDF) kwa kushirikiana na Community Forests Pemba (CFP) na Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania, Zanzibar (TAMWA-ZNZ). Taasisi nyingine ni pamoja na Tanzania Horticultural Association (TAHA), TRIAS, HELVETAS, RIKOLTO na SOLIDARIDAD chini ya ufadhili wa Umoja wa Ulaya (EU). 

Alifahamisha kwamba moja ya changamoto inayohitaji ushirikiano wa karibu ni suala la masoko kwa mazao hayo ambapo wakulima bado wanashindwa kupata taarifa sahihi.

Bibi Anna aliwashauri  watekelezaji wote wa mradi kushirikiana hasa kwa kufanya tafiti za masoko ili kuwasaidia wakulima kujua mahitaji sahihi ya soko.

Nae Bibi Upendo Mndeme, Afisa lishe kutoka Wizara ya Kilimo Tanzania Bara aliwaomba watekelezaji wa mradi huo kushirikiana kuunda mfumo wa kidigitali wa kilimo utakaowasaidia wakulima kupata taarifa zote za kilimo kwa wakati.

Alisema mfumo huo ukifanikiwa kufanya kazi ipasavyo, utawasaidia wakulima wengi kupata fursa ya kufikiwa na pia kupata taarifa  sahihi zinazohusu uzalishaji wa mazao yao katika kila hatua wanayofikia.

Kwa upande wa mradi wa VIUNGO Zanzibar, mmoja wa watekelezaji; meneja wa mradi, Bi Amina Ussi, alieleza kuwa katika kuhakikisha wakulima wanazalisha kwa kufuata mbinu bora za kisasa, mradi umetayarisha miongozo mitatu kwa ajili ya wakulima ikiwemo Mwongozo wa hali ya hewa, usalama wa chakula na lishe na muongozo wa kilimo cha bustani za nyumbani.

Gaspary Charles

Afisa Mawasiliano, TAMWA  ZNZ.

 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.