Habari za Punde

Serikali Kununua Ndege Tano Mpya
Na. Lilian Lundo – MAELEZO

Serikali imeingia mikataba ya ununuzi wa ndege Tano mpya, ambapo ndege nne ni za abiria na ndege moja ni ya mizigo.

Waziri wa ujenzi na uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa amesema hayo jana, Machi 8, 2022 alipokuwa akitoa taarifa ya mafanikio ya mwaka mmoja wa serikali ya awamu ya sita katika stesheni ya Kwala, Mkoani Pwani.

“Serikali imeingia mikataba ya ununuzi wa ndege tano (5) mpya ambazo ni, Dash 8 Q400 ndege moja (1), Boeng B737-9 Max ndege mbili (2), Boeing B787-8 Dreamliner ndege moja (1) na Boeing 767-300F ndege moja (1) ambayo ni ya mizigo,” alifafanua.

Vilevile amesema kuwa katika kipindi cha mwaka mmoja tangu serikali ya awamu ya Sita imeingia madarakani, ndege mpya tatu (3) ambazo ni ndege aina ya Dash 8 Q400 yenye uwezo wa kubeba abiria 76 iliwasili Julai, 2021 na ndege mbili aina ya Airbus A220-300 zenye uwezo wa kubeba abiria 130 kila moja ziliwasili Oktoba 2021, ambapo imeifanya ATCL kuwa na jumla ya ndege mpya 11.

Prof. Mbarawa ametaja mafanikio mengine katika sekta ya uchukuzi kuwa ni mradi wa uboreshaji wa gati Na. 0 – 7 Bandari ya Dar es Salaam ambao ulikamilika Julai, 2021 na kuzinduliwa rasmi Desemba 2021, ambapo kutokana na maboresho hayo, uwezo wa miundombinu ya Bandari ya Dar es Salaam umeongezwa kutoka kuhudumia tani milioni 15 kwa mwaka hadi tani milioni 25.

Aidha, Bandari hiyo ya Dar es Salaam imeanza kupokea meli kubwa zaidi za magari na mizigo. Vilevile, kazi ya kuongeza kina cha lango la kuingia na kugeuka meli na kuimarisha na kuboresha gati Na. 1 na 2, kazi imekamilika kwa asilimia 35 inatarajia kukamilika Juni, 2022.

Kwa upande wa ujenzi wa reli kwa kiwango cha Standard Gauge (SGR) awamu ya kwanza kutoka Dar es Salaam hadi Mwanza umeendelea kutekelezwa kwa ufanisi, ambapo hadi kufikia Februari, 2022 ujenzi wa reli kipande cha Dar es Salaam hadi Morogoro (km 300) umekamilika kwa asilimia 95.03, kipande cha reli kutoka Morogoro hadi Makutuporo (km 422) umeendelea kutekelezwa, hadi Februari, 2022 ujenzi umekamilika kwa asilimia 79.23. Ujenzi wa kipande cha Mwanza – Isaka (km 341) unaendelea na umefikia asilimia 4.3.

Pia, wizara ya ujenzi na uchukuzi katika kipindi cha mwaka mmoja wa serikali ya awamu ya Sita imefanikiwa kukamilisha na kuanza kutumika kwa daraja jipya la Tanzanite lenye urefu wa kilomita 1.03  lililopo Jijini Dar es Salaam lililogharimu sh. Bilioni 243, kukamilisha daraja la JP Magufuli lililipo Mwanza, ujenzi wa daraja jipya la Wami lenye urefu wa mita 510 na upana wa mita 11.85 ambalo kwa sasa limefikia asilimia 75.57 na litagharimu sh. Bilioni 72.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.