Habari za Punde

SIKU YA UPANDAJI MITI KITAIFA NA SIKU YA MISITU DUNIANI KUPAMBWA NA KAULIMBIU YA MTI WANGU, TAIFA LANGU, MAZINGIRA YANGU, KAZI IENDELEE.

Na.Maliasili na Utalii Tanzania

Wizara ya Maliasili na Utalii imesema kuwa maadhimisho ya Siku ya Upandaji Miti Kitaifa na Siku ya Misitu Duniani  mwaka 2022 yatafanyika  Wilayani  Magu, Mkoani Mwanza yakiongozwa na kaulimbiu isemayo Mti wangu, Taifa langu, mazingira yangu, Kazi Iendelee.

Taarifa iliyotolewa  Wizara ya Maliasili na Utalii leo jijini Dodoma imeeleza kuwa maadhimisho  hayo ya Siku ya Upandaji Miti Kitaifa ambayo hufanyika Aprili 1 ya kila mwaka sasa yatafanyika Machi  21, 2022 yakiwa yameunganishwa.

Maadhimisho hayo yatafanyika kwa mara ya kwanza nchini Tanzania yakiwa yameongozwa na malengo makuu mawili ambayo ni kuwakumbusha na kuwahamasisha Watanzania kuhusu umuhimu wa  upandaji na utunzaji wa miti kwa ajili ya kuongeza upatikanaji wa bidhaa na huduma za misitu hapa nchini.

Pia yatajikita katika kukumbusha na kuhamasisha umma wa watanzania juu ya umuhimu wa  kuendelea kutunza na kuhifadhi misitu kwa ajili ya kizazi cha sasa na kijacho kwa kuhamasisha wananchi waendelee kupanda miti hasa katika kipindi hiki cha mvua, kuitunza, na kuihifadhi misitu  iliyo katika maeneo yao kwa faida ya kizazi cha sasa na  kijacho.

Taarifa hiyo imefafanua kuwa Sekta ya Misitu ina mchango mkubwa katika maendeleo ya kiuchumi, kijamii na kimazingira na kuongeza kuwa watanzania wanategemea nishati ya miti kwa zaidi ya asilimia 90.

Aidha, imeeleza kuwa misitu inatoa asilimia 45 ya mahitaji ya malighafi ya ujenzi, hulinda vyanzo vya maji na kuzuia mmomonyoko wa udongo. Vile vile, misitu husaidia kunyonya hewa ukaa na hivyo kuchangia katika juhudi za kukabiliana  na changamoto za mabadiliko ya tabia nchi.

Katika hatua nyingine tarifa hiyo imeeleza kuwa kwa ujumla maisha ya mwanadamu yanategemea misitu kuanzia kuzaliwa kwake hadi mwisho wa maisha yake. Hata hivyo, takwimu zinaonesha kuwa Tanzania inapoteza eneo la misitu lenye ukubwa wa hekta 469,000 kwa mwaka kutokana na sababu mbalimbali zikiwemo za ukataji wa miti usio endelevu, mioto kichaa, na upanuzi wa mashamba.  

Hivyo, ili kuziba pengo la miti na misitu inayopotea kila mwaka jamii inatakiwa kupanda miti ya kutosha, na kuhakikisha misitu inasimamiwa kiuendelevu.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.