Na Kijakazi Abdalla. Maelezo Zanzibar. 24/03/2022
SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar imesema itachukua hatua za makusudi ili kukinusuru kisiwa cha Mnemba kisiendelee kuchukuliwa na bahari li kiendelee kuleta haiba kwa watalii.
Haya ameyasema Waziri wa Uchumi wa Bluu na Uvuvi Suleiman Masoud Makame wakati alipofanya ziara katika kisiwa hicho na kuona jinsi mabadiliko ya tabia ya nchi yalivyokiathiri kisiwa hicho.
Ameema ikiwa serikali haitachukua jitihada hizo basi kisiwa hicho kitaendelea kupotea na kupoteza haiba ya nchi hasa historia ambayo imedumu kwa muda mrefu.
Aidha amesema kisiwa hicho kina historia ndefu ya utalii na eneo moja lenye manufaa katika kukuza pato la serikali na eneo la hifadhi ya mazingira ya baharini.
Vilevile amesema tayari eneo hilo limeshaathiriwa kwa kiasi kikubwa na maji na tayari bahari imeshachukua mita 30 hadi 40 ya kisiwa hicho.
Hata hivyo alisema atashirikiana na serikali ikiwemo Mamlaka ya Mazingira, Uchumi wa Bluu na Uvuvi na Idara ya Misitu kuona wanakinusuru kisiwa hicho.
Naye, Meneja wa mradi wa kisiwa cha Mnemba, Jonathan Braack, alisema eneo la upande wa kulia la bahari ambalo lilikuwa ni nchi kavu hivi sasa limeshavamiwa na maji ya bahari.
Alisema, takriban mita 50 ambazo zilikuwa bangaloo wanazoishi watu tayari zimeshavamiwa na maji ya bahari hivyo ni vyema kwa serikali kuchukua jitihada za kukinusuru kisiwa hicho kisiendelee kuathiriwa na maji ya bahari.
No comments:
Post a Comment