Habari za Punde

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk.Hussein Ali Mwinyi Ameongoza Wananchi Katika Kisomo cha Dua na Hitma kumuombea Rais wa Kwanza na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Zanzibar Hayati Sheikh.Abeid Amani Karume.

 

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk. Hussein Ali Mwinyi ameongoza hitma ya kumuombea dua Rais wa Kwanza wa Zanzibar Marehemu Sheikh Abeid Amani Karume, iliyofanyika Afisi Kuu ya CCM Kisiwandui Zanzibar.

Hitma hiyo, pia ilihudhuriwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan pamoja na viongozi mbali mbali wa Serikali akiwemo Rais Mstaafu wa Zanzibar wa Awamu ya Sita Dk. Amani Abeid Karume, Makamo wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Philip Mpango.

Wengine ni Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Majaliwa Kassim Majaliwa, Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Othman Masoud Othman, Makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar Hemed Suleiman Abdulla, viongozi wa vyama vya siasa pamoja na viongozi wa dini.

 

Hitma hiyo ya kumuombea dua Marehemu Sheikh Abeid Amani Karume ambapo pia ni miongoni mwa maadhimisho ya Siku ya Mashujaa ilitanguliwa na dua ya ufunguzi kutoka kwa Sheikh wa Mkoa wa Dar es Salaam Sheikh Alhad Mussa Salum na Qur-an tukufu, iliyosomwa na Ustadh Abdulrahim Twalib na kuhitimishwa na Sheikh Salim Juma Faki.

 

Mara baada ya hitma hiyo, Sheikh Khamis Abdulrahman, Mjumbe wa Baraza la Maulamaa Zanzibar alitoa mawaidha na kumuelezea marehemu mzee Abeid Amani Karume kuwa ni kiongozi aliyepigania maendeleo ya wananchi wa Zanzibar na kumuombea MwenyeziMungu ampe makaazi mema Peponi. Amin.

 

Aidha, Sheikh Khamis alieleza kwamba kumuombea dua mtu aliyetangulia mbele ya haki ni wajibu kwa kila Muislamu.

 

Aliongeza kuwa miongoni mwa mambo mengi mazuri aliyoyafanya Marehemu Sheikh Abeid Amani Karume pia, ameweka misingi mizuri ya taalum kwa kujenga na kuweka jiwe la msingi la Chuo Cha Kiislamu kiliopo Mazizini Zanzibar mnamo mwaka 1972, chuo ambacho kimetoa wataalamu pamoja na  Maulamaa mbali mbali ambao wengine hivi sasa wako ndani na nje ya Tanzania wakitoa elimu waliyoipata chuoni hapo.

 

Aidha, tukio lililofuata ni uwekaji wa mashada ya mauwa ambapo walioweka maua  katika kaburi la Marehemu Sheikh Abeid Amani Karume ni Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk. Hussein Ali Mwinyi, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan, Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi ya Tanzania Venance Salvatory Mabeyo kwa niaba ya wakuu wa vikosi vya Ulinzi Tanzania.

 

Wengine ni Balozi mdogo wa  India anayefanya kazi zake hapa Zanzibar  Bhagwant Singh aliyewawakilisha Mabalozi wenzake wa hapa nchini, Balozi Ali Karume aliyewakilisha familia ya Marehemu Sheikh Abeid Amani Karume pamoja na Mzee Ramadhan Nzori aliyeweka shada la maua akiwawakilisha wazee.

 

Pia, katika tukio hilo kulisomwa dua na sala vilivyoongozwa na viongozi wa dini katika kaburi la Marehemu Sheikh Abeid Karume lililopo pembezoni mwa Afisi hiyo ya CCM Kisiwandui  ambapo Mufti Mkuu wa Zanzibar Sheikh Omar Kabhi alisoma kwa niaba ya Waislamu, Padri Stanley Nikolas Lichinga Katibu wa Dayosisi ya Anglikana Zanzibar alisoma kwa niaba ya Wakristo pamoja na Nikhil Mahraja Joshi Kandka aliyesoma kwa niaba ya Wahindu.

 

Aidha, wake wa viongozi wakiongozwa na Mama Mariam Mwinyi walihudhuria katika hitma hiyo ambapo pia, Mjane wa Marehemu Sheikh Abeid Karume Mama Fatma Karume na viongozi wengine wanawake wa kitaifa wakiwemo Mawaziri, Wabunge, Wawakilishini pamoja na wake wa viongozi wastaafu na wananchi kutoka sehemu mbali mbali za Zanzibar na Tanzania Bara.

 

April 7, 1972 ndiyo siku aliyouawa Rais wa Kwanza wa Zanzibar marehemu Mzee Abeid Amani Karume na wapinga maendeleo nchini ambapo hivi leo imetimia miaka 50 tokea utokee msiba huo.


Imetayarishwa na Kitengo cha Habari,

Ikulu Zanzibar.ILITY

 

 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.