Habari za Punde

Waziri Mhe.Ndalichako Ataka Ushirikiano wa Waajiri na Wafanyakazi Kuzuiya Ajali na Magonjwa Mahali pa Kazi.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Prof. Joyce Ndalichako akihutubia wakati hafla ya maadhimisho ya Siku ya Usalama na Afya Mahali Pa Kazi Duniani yaliyofanyika kitaifa katika eneo la Jakaya Kikwete Convention Centre, Jijini Dodoma
Sehemu ya washiriki wakifuatilia hotuba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Prof. Joyce Ndalichako (hayupo pichani) wakati wa hafla hiyo ya maadhimisho ya Siku ya Usalama na Afya Mahali Pa Kazi Duniani yaliyofanyika Jijini Dodoma.
Mtendaji Mkuu wa OSHA, Bi. Khadija Mwenda akifafanua jambo kuhusu masuala ya usalama na afya wakati wa hafla hiyo ya maadhimisho ya Siku ya Usalama na Afya Mahali Pa Kazi Duniani yaliyofanyika Jijini Dodoma.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Prof. Joyce Ndalichako akifuatilia zoezi la uokoaji kwenye moto kwa tumia vazi maalum la uokozi alipotembelea eneo la Banda la Mgodi wa Anglo Gold Ashanti (GGM) katika maadhimisho hayo ya Siku ya Usalama na Afya Mahali Pa Kazi Duniani yaliyofanyika Jijini Dodoma.

Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu.)


Na: Mwandishi Wetu – DODOMA.                                                                                                     

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Prof. Joyce Ndalichako amewataka waajiri na wafanyazi kushirikiana pamoja kujenga utamaduni bora wa kuweka mazingira yenye usalama na afya ili kuzuia vihatarishi katika maeneo ya kazi.

Hayo yameelezwa hii leo Aprili 28, 2022 katika maadhimisho ya Siku ya Usalama na Afya Mahali Pa Kazi Duniani yaliyofanyika kitaifa katika eneo la Jakaya Kikwete Convention Centre, Jijini Dodoma.

Waziri Ndalichako alieleza kuwa, Waajiri na wamiliki wa sehemu za kazi katika maeneo mengi hudhani kuweka mazingira ya kazi salama ni gharama za ziada kutokana na ukosefu wa ufahamu wa faida za kuboresha mazingira ya kazi ili waweze kutambua hasara zinazoweza kutokea hususan inapotokea ajali au ugonjwa katika sehemu ya kazi.

 “Ni utamaduni unaohitaji kuona Serikali, Waajiri na Wafanyakazi wanashiriki kikamilifu katika kuweka mazingira salama ya kufanya kazi kupitia mfumo wa haki na wajibu ulioainishwa, ambapo kanuni ya kuzuia vihatarishi inapewa kipaumbele cha juu zaidi,” alieleza Waziri Ndalichako

“Waajiri na wafanyakazi ni lazima wachukulie kwamba afya na usalama mahali pa kazi ni sehemu ya mipango ya uzalishaji au utoaji wa huduma,”

Alifafanua kuwa, katika maadhimisho ya siku hiyo wanalenga kuongeza uelewa kuhusu ukubwa na madhara ya ajali na magonjwa yatokanayo na kazi miongoni mwa waajiri na wafanyakazi; Kuhamasisha namna ya kulinda usalama na afya za Wafanyakazi wakiwa kazini hasa kwa kuzingatia kanuni za kazi Kitaifa na Kimataifa;na Kuhamasisha Wadau mbalimbali kujenga uwezo na utaalamu wa kuweka mifumo, sera na mikakati inayolenga kulinda usalama na afya za wafanyakazi wakiwa kazini.

“Wadau wa Utatu yaani Serikali, Waajiri, na Wafanyakazi wakishirikiana katika hatua zote za kufanya maamuzi ya kulinda usalama na afya za wafanyakazi itachangia kuboresha sera na mikakati ya kuwa na mazingira usalama na afya mahali pa kazi,” alisema

“Serikali kupitia Wakala wake wa Usalama na Afya mahali pa Kazi (OSHA), imeanzisha tuzo maalumu kwa Waajiri watakao kuwa wanaonyesha juhudi katika kuboresha mazingira ya kazi kwa kuweka mifumo ya afya na usalama kazini iliyo imara,” alisema

Aliongeza kuwa Serikali inathamini juhudi za Waajiri katika Sekta za Umma na Binafsi kwa kushirikiana na Wafanyakazi wanaojituma katika kuboresha mazingira ya kazi wao wenyewe bila kusukumwa. Hivyo Serikali itaendelea kushirikiana na wadau wote ili kupunguza au kuondoa kabisa vifo, ajali, magonjwa na madhara yatokanayo na kazi lengo ni kuhakikisha kuwa, mazingira ya kazi ni salama na hivyo kuongeza tija katika uzalishaji.

“Serikali kupitia Wakala wake wa Usalama na Afya mahali pa Kazi (OSHA), imeanzisha tuzo maalumu kwa Waajiri watakao kuwa wanaonyesha juhudi katika kuboresha mazingira ya kazi kwa kuweka mifumo ya afya na usalama kazini iliyo imara,” alisema

Sambamba na hayo, Profesa Ndalichako amewataka Waajiri na Wafanyakazi kuendelea kuchukua taadhari dhidi ya magonjwa mbalimbali ili kulinda afya na usalama wao

Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa OSHA, Bi. Khadija Mwenda alisema kuwa masuala ya usalama na afya masuala ya Afya na Usalama ni mtambuka,na yanagusa sekta zote za uchumi.

“kampeni ya mwaka huu imejikita zaidi katika kuhakikisha kuwa kunakuwa na ushirikishwaji katika ngazi zote zamaamuzi wakiwemo wafanyakazi ili nao wawe sehemu ya maamuzi na hivyo kujenga utamaduni wa kukinga zaidi kuliko kusubiri mambo yaharibike ndipo hatua za kuyarekebisha zichukuliwe. Utamaduni huu ukijengeka utapelekea kupunguza ajali, magojwa na vifo vinavyotokana na mazingira hatarishi ya kazi na hivyo kuongeza tija katika uzalishaji ndani ya Taifa letu,” alisema

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.