Habari za Punde

Askari wa Uhifadhi Waliodanganya Kuvuna Mamba Buchosa Kuchukuliwa Hatua za Kinidhamu.

Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mary Masanja (Mb) akijibu swali bungeni jijini Dodoma leo Mei 13,2022. 

Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mary Masanja (Mb) amemuelekeza Katibu Mkuu, Wizara ya Maliasili na Utalii kuwachukulia hatua za kinidhamu Askari wa Uhifadhi watakaothibitika kuidanganya Serikali kwamba wameshiriki katika zoezi la kuvuna mamba wawili Wilayani Buchosa Mkoani Mwanza.

 

Ameyasema hayo leo Bungeni jijini Dodoma alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Buchosa, Mhe. Eric James Shigongo kuhusu mikakati ya Serikali ya kuzuia mamba wanaoua watu Jimboni Buchosa.

 

Amefafanua kuwa Serikali katika kukabiliana na changamoto hizo, inaendelea kutekeleza Mkakati wa Kitaifa wa Kusimamia Migongano baina ya Binadamu na Wanyama wakali na waharibifu.

 

Awali akijibu swali la msingi Mhe. Masanja alisema kuwa Serikali imevuna jumla ya mamba wawili katika wilaya hiyo.

 

“Kuanzia kipindi cha Julai, 2021 hadi Aprili, 2022 jumla ya mamba wawili (2) wamevunwa katika Kata ya Maisome Wilayani Buchosa, watu 992 wamepewa elimu kuhusu namna ya kuepuka madhara ya wanyama wakali na waharibifu na kikosi cha Askari wa Uhifadhi watatu (3) wapo uwandani wanaendelea na doria za kudhibiti mamba katika Wilaya ya Buchosa” Mhe. Masanja amesisitiza.

 

Aidha, amezishauri Mamlaka ya Serikali za Mtaa (Halmashauri) kuandaa mpango madhubuti wa kutenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa vizimba na Wizara ya Maliasili na Utalii itatoa utaalam.


Akifafanua kuhusu mikakati ya Serikali ya kukuza utalii wa fukwe Mhe. Masanja amesema kuwa Serikali imebaini maeneo mapya ya fukwe za Bahari ya Hindi yanayofaa kwa ajili ya uwekezaji wa shughuli za utalii katika Mikoa ya Dar es Salaam, Tanga, Pwani, Lindi na Mtwara.

 

Aidha, Mhe. Masanja amesema Serikali imeweka utaratibu wa kusajili maeneo ya fukwe yanayofaa kwa shughuli za Utalii kama maeneo maalum ya Uwekezaji wa Shughuli za Utalii (Tourism Special Economic Zone).

 

Pia, Serikali imeendelea kuwahamasisha wamiliki wa maeneo ya fukwe nchini ili kusajili maeneo ya fukwe wanayoyamiliki chini ya utaratibu wa Maeneo Maalum ya Uwekezaji wa Shughuli za Utalii kwa lengo la kuiwezesha Serikali kushirikiana na wamiliki hao kuhimiza uwekezaji wa utalii wa fukwe.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.