Habari za Punde

CHATI YA LATRA ILIYOCHUJUKA

 
Na.Adeladius Makwega-DODOMA

Kwa muda wa majuma mawili nimekuwa nikishuhudia kutupiana kwa maneno baina ya makondakta na abiria katika vyombo vya usafiri jijini Dodoma. Jambo hilo limekuwa si jema huku abiria wengi wanakuwa wanyonge wanapopanda vyombo vya usafiri vinavyotoa huduma mkoani humo.

Binafsi niliamua kulifuatilia jambo hilo ndani ya majuma yote mawili mkazo ulikuwa kwa siku nne mfululizo Mei 15, 16, 17 na 18, 2022.

Katika kipindi hicho nilibahatika kulipanda mara nyingi kwa bahati tu basi yenye usajiri wa T 178 DQU inayofanya kazi kati ya Sabasaba na Chamwino Ikulu. Katika siku hizo nne za majuma mawili nilifanya safari nane yaani nne za kwenda na nne kurudi, T 178 DQU nilipanda mara saba. Safari mbili za Sabasaba Chamwino Ikulu na tano za Mtumba Chamwino Ikulu.

Mwanakwetu nilibaini kuwa nauli kati ya Chamwino Ikulu hadi Sabasaba kwa sasa ni shilingi 1600/-na kabla ya kupanda bei za mafuta nauli ilikuwa shilingi 1400/- .Nauli kati ya Sabasaba na hadi Mtumba ni shilingi 1000/- na nauli kati ya Chamwino Ikulu hadi Mtumba ni shilingi 1000/-.huku nauli ya kituo na kituo ni shilingi 500/-

Mei 18, 2022 nilipotoka nyumbani kwangu nilielekea kituo cha basi nikiwa upande wa pili wa barabara basi lilinipita na hata nilipojaribu kutoa ishara halikusimama.

Likaeendelea kwa mwendo kidogo nilivuka barabara na kusimama kituoni kungoja basi lingine nikiamini kuwa basi hilo nimelikosa. Nikiwa hapo alitokea kijana mmoja wa bodaboda akaniambia kuwa mzee mbona basi limekuacha njoo upande nikuwaishe ukalipande mbele kwa kuwa na mimi naelekea uelekeo huohuo.

Nikamwambia mbona wale wameniona nikiwa navuka barabara mbona hawakusimama? Kijana huyu akasema kuwa mzee twende tu. Nikaipanda bodaboda hiyo na kulivuka basi hilo ambalo lilikuwa linapakia abiria. Nikashuka kituo cha mbele na kumshukuru sana huyu bodaboda huyu.

Kweli basi hilo lilikaribia nilipo na kusimama na nilipolitazama nikabaini ni lile lile T 178 DQU nilipanda nakuanza safari kwenda Mtumba.Safari iliendelea vizuri na kondakta alianza kuchukua nauli zake.

Kwa kuwa basi lilikuwa na abiria wengi, abiria mmoja aliyekuwa amekaa jirani na dereva alipotakiwa kutoa nauli alitoa pesa pungufu, jambo hilo likaleta mzozo kidogo na kondakta, kuondoa utata alifungua pahala ambapo panapachikwa runinga ya basi hilo na kuonesha chati iliyobandikwa hapo, nadhania runinga hiyo ilikuwa mbovu ambayo ilifanana fika na umbo la kompyuta mpakato.

Kondakta alipopewa nauli yake alikuwa mpole sana na kusahau kuifunga runinga yake ili chati hiyo isionekana.

Swali ambalo nilikuwa nalo mara saba zote nilipopanda basi hilo nilijiuliza kwa nini chati hii isibandikwe sehemu ya wazi?

Nakala ya chati hiyo ilikuwa ni kivuli kilichofifia mno hata mimi kwa mbali sikuweza kusoma maneno mengi bali ni neno LATRA tu na mchujuko wake ulikuwa mkubwa. Nilistajabu dereva aliangalia nyuma kidogo na kupafunga vizuri pale palipokuwa na chati hii na kuendelea na safari.

Mwanakwetu nilishuka Mtumba, na hapo nilijiulizwa maswali mengi kwanini chati hiyo ifichwe kama uchawi?

Nikasema kuwa hoja ya uhalali wa nauli inatakiwa kujibiwa kwa wepesi sana kwani kama chati ikibandikwa katika kila basi, katika kila kituo na hata kuwekwa maeneo ya wazi jambo hilo linaweza kuondoa maneno na kutuhumiana baina ya abiria na makondakta.

Mkurugenzi Mkuu LATRA anawajibu wa kutoa maelekezo hayo nchini nzima katika kila pahala penye mkusanyiko wa abiria, kwani kutoa fotokopi gharama si kubwa na LATRA jambo hilo wanaliweza.Binafsi nina amini kazi hiyo inaweza kufanywa na LATRA vizuri sana chini ya Mkurugenzi wake Mkuu ndugu Gilliard Ngewe.

Katika kila wilaya kuna wenyeviti wa kamati za ulinzi za wilaya jambo hilo wanaweza kulisimamia vizuri na wale wanaongeza nauli wachukuliwe hatua. Kwa hakika Chamwino Ikulu ni eneo ambalo lipo jirani na Ikulu ya Rais wetu Samia Suluhu Hassan kwa hiyo ni vizuri Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya hii ajitahidi angalau kulitatua hilo.

makwadeladius@gmail.com

0717649257

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.