Habari za Punde

Mnazi Haupopolewi.

 

Na.Adeladius Makwega-DODOMA

Mikoa mingi ya pwani ya Tanzania huwa inastawi minazi ambayo hutumiwa kama kiungo kikubwa cha mboga na chakula. Mapishi ya nazi yana raha yake hasa hasa ukipikiwa na mjuzi na isitoshe hata anayekula kama awe anafahamu utamu wa mapishi hayo.

Inawezekana mwanakwetu wewe umezoea kuungiwa chakula chako kwa kutumia ufuta, samli, karanga, mbegu za maboga, mbegu za ubuyu, kweme na kadhalika, mambo ya nazi yana hekima zake.

Leo mwanakwetu nakupa hekima moja tu ya nazi hasa hasa namna inavyoanguliwa kutoka katika mti wa mnazi.

Nazi huwa inanguliwa kwa njia mbili moja halali na nyengine haramu.

Njia halali ni nazo zipo mbili, kwanza mkwezi huukwea mnazi kwa kutumia kamba maalumu ambayo hujivisha miguuni, anausogelea mnazi na kuukamata kwa mikono yake miwili na kuanza kuukwea hadi juu na kuangua nazi zilizokomaa. Kamba ya miguuni inamsaidia mkwezi aweze kupumzika akiwa anaukwea mnazi huo hasa hasa ukiwa na wenye kona nyingi.

Halali ya pili ya kuukwea mnazi ni kwa kutumia ngazi ambazo huwa zimechimbwa na kitu chenye ncha kali na mkwezi anaukwea kwa kupachika miguu yake katika eneo hilo hadi kileleni nakuangusha nazi anazotaka.

Kwa desturi ya maisha ya pwani kazi ya ukwezi angalabu hufanywa na wanaume, kama mwanamke anaangu nazi basi kwa minazi mifupi na minazi ya kisasa. Hapo hufuata kazi ya kuifua nazi kwa matumizi ya mekoni.

Uvunaji haramu nao upo kwa kuipopoa, zoezi hilo hufanywa na wezi ambao huwa hawana mashamba ya minazi kwa kurusha kota (kipande cha mti) na kuzigonga nazi, madafu na vidaka kuanguka chini.

Mara nyingi wezi hutumia mtindo huo maana kuupanda mnazi watakamatwa kiurahisi

Msomaji wangu unaweza kujiuliza kwani mwanakwetu leo ana nini?

Siku ya leo nimekuwa naulinganisha mfumo wa elimu ya Tanzania wa chekechea miaka 2-3, msingi miaka 7, sekondari miaka 4, sekondari ya juu miaka 2, shahada ya kwanza miaka 3-4 na shahada ya uzamili miaka 2-3 na shahada ya uzamivu miaka 3-4 na mkwezi wa nazi, hasa hasa njia halali ya kutumia kamba na ngazi .

Mtoto wa kitanzania anaposoma kwa mfumo wa elimu yetu anafuata hatua zote hadi tunakuja kumpata mtaalamu wetu katik fani mbalimbali.

Binafsi ninaona wazi kuwa hoja ya darasa la saba kupatiwa kibali cha kusoma shahada za vyuo vikuuu ni kuangua nazi kwa kuzipopoa kwa kota. Kota hilo linaangusha hata vidaka ambavyo kwa hakika havipaswa kuanguliwa wakati huo.

Shabaha ya kota ni kupiga matunda ya mnazi lolote lile kwa kubahatisha likianguka dafu sawa, ikianguka nazi sawa na hata kikianguka kidaka twende kazini.

Mwanakwetu ukikiangusha kidaka unakwenda kufanyia nini? Kazi pekee ya kidaka kikidondoka ni kwa watoto wanatumia kuchezea mdako na  kuandikia maandishi katika kuta za nyumba za wazazi wao hasa hasa wale wanaonza darasa la kwanza tu.

Huo ni uharibifu mkubwa tunapopanda minazi nia yetu tupate nazi ili tuweze kuungia vyakula vyetu na siyo kupata vidaka.

Mwanakwetu kwa leo pia naendelea kupigia chapuo suala la taasisi zote zinazosimamia elimu yetu kuendelea kuheshimu mifumo yetu ya elimu na kuitetea bila woga mbele ya Watanzania na dunia kwani tangu uhuru mfumo huu wa elimu umewanufaisha wengi na taifa letu pia.

Natambua kuwa zipo hoja juu ya wagunduzi kadhaa, hilo nakubaliana nalo lakini ifahamike wazi kuwa sayansi huendana na kanuni zake ni wajibu wa mgunduzi kuifuata msingi ya sayansi. Misingi hiyo ndiyo tunaipata katika elimu zetu za msingi na sekondari.

Binafsi naendelea kukipongeza sana Chuo Kikuu Dar es Salaam kwa kuheshimu hilo na ni jukumu la Wizara yetu ya Elimu chini ya Profesa Adolf Mkenda kulisimamia hilo kwa nguvu zote kama mkulima wa minazo anavyoheshimu minazi yake inayompatia nazi bora.

Naiweka kalamu yangu chini kwa kusema kuwa unapotaka kuvuna nazi sharti lake ni kuukwea mnazi kwa kamba au kwa ngazi na siyo kuupopoa.

 Mwanakwetu mnazi haupopolewi.

makwadeladius@gmail.com

 0717649257

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.