Habari za Punde

Serikali: Bima ni Biashara Huria.

Naibu Waziri, Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhe. Mhandisi Kundo Methew (Mb) akijibu swali bungeni jijini Dododma kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) kuhusu biashara huria ya makampuni ya bima.

Na. Eva Ngowi, WFM, Dodoma

Serikali imesema biashara ya bima nchini ni huria inayoendeshwa na kampuni za bima zipatazo thelathini na moja ikiwemo Shirika la Bima la Zanzibar (ZIC) ambapo kwa mujibu wa Sheria ya Bima namba 10 ya mwaka 2009, kampuni yoyote ya Bima, iliyosajiliwa, ina haki ya kuweka kinga ya bima kwenye miradi mikubwa.

Hayo yameelezwa bungeni jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhe. Mhandisi Kundo Methew (Mb) kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Gando Mheshimiwa Mussa Omar Salim, aliyetaka kujua kama kuna mwongozo wowote unaoeleza kuwa Shirika la Bima la Zanzibar haliruhusiwi kushiriki kukata bima za miradi mikubwa.

“Shirika la Bima la Zanzibar (Zanzibar Insurance Corporation- ZIC) limesajiliwa na kupewa leseni ya biashara namba 00000821 na Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania –TIRA, chini ya Sheria ya Bima Na. 10 ya mwaka 2009. ZIC inafanya biashara za bima sehemu zote Tanzania Bara na Zanzibar.” Alisema Mhe. Kundo

Mheshimiwa Kundo alisema kuwa Hakuna mwongozo wowote unaokataza Zanzibar Insurance Corporation (ZIC) kushiriki katika biashara ya kukata bima za miradi mikubwa nchini.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.