Habari za Punde

Wakati Ule Si wa Sasa.

Na.Adeladius Makwega-DODOMA

Ndugu yangu mmoja alinisimulia jambo fulani kuwa kuna taasisi moja ya umma walipokuwa wakifanya kazi waliona mambo hayaendi hivyo wakakaa kikao kujadili hali hiyo.

Katika kile kikao mjumbe mmoja alishauri kuwa jamani mmoja ambaye aliwahi kufanya nao kazi hapo anaweza kuwasaidia, lakini kwa pumzi zao taasisi imewashinda. Mjadala ulikuwa mkali sana wajumbe wakigawanyika juu ya mtu huyo kurudishwa hapo.

Mama mmoja mjumbe halali wa kikao hicho alisema kuwa ni kweli mtu huyo namfahamu na nimefanya nae kazi, anawahi kazini, anafanya kazi kwa bidii lakini shida yake tu pale mtakapomkwaza cha moto mtakiona, akashauri ndugu huyu asiende pale.

Kikao kilisahau kuwa wale ndugu uwepo wao pale ni taasisi iwe imara kwa hiyo ajenda ikahamia katika madhaifu ya mwokoa jahazi. Ushauri ulikataliwa maana yake ni heri taasisi ile ionekane hakuna kitu kuliko mwenzao kurudi. Jahazi lishazama siku nyingi, kama linaonekana basi ni pembe ya jahazi hilo zamifu katika kina cha bahari.

Kwa sehemu kubwa watu katika utumishi wa umma wanapaswa kutazama taasisi isonge mbele hiyo ndiyo iwe shabaha na siyo maslahi binafsi.

Kiukweli watu wanapofanya kazi pamoja wanatambuana uwezo na madhaifu ya kila mmoja, hakuna malaika anayefanya kazi duniani, kila mmoja ni binadamu. Kila upande unapaswa kufahamu hilo, yale madhaifu ya kila mmoja yanawekwa kando alafu wanauchukua ule uwezo wa kila mmoja na kujenga taasisi ya hiyo.

Pale unaposimamia madhaifu ya mtu na kuyaweka mbele bila ya kujua kuwa taasisi ile ni jamii nzima, jahazi linazama na mara zote jahazi linazama taratibu.Ukija kutahamaki tayari.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.