Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe Riziki Pembe Juma ameiomba jamii kushirikiana katika kutoa taarifa za kupatikana kwa mtuhumiwa Kheri Mkombe Abdallah anaetuhumiwa kumfanyia kitendo cha udhalilishaji mtoto wake ili kufikishwa katika vyombo vya sheria.
Akizungumza na vyombo vya habari kuhusiana na tukio hilo lililotokea hivi karibuni amesema kutokutowa taarifa hizo kwa anaezifahamu kunaashiria kuunga mkono kitendo alichokifanya ambacho kinapaswa kulaaniwa na jamii nzima.
Amesema kukithiri kwa vitendo hivyo ndani ya jamii kumepelekea kuathiri maadili ya jamii nzima hivyo wananchi wanapaswa kushirikiana na Serikali katika kuona inalaani vitendo hivyo kwa kuvifichua ili kuvikomesha na kutoendelea kuwepo.
Akizungumzia kuhusiana na kutokukidhi haja kwa sheria zilizopo sasa juu ya makosa hayo Mhe Riziki amefahamisha kuwa Wizara kwa kushirikiana na wadau wa masuala ya sheria imeanza kufanya mapitio ya sheria za sasa ili kutambua mapungufu yaliyopo na hatimae kupatikana sheria zitakazokidhi mahitaji.
Aidha ameshauri jeshi la polisi nchini kutumia saikolojia zaidi wakati wanapowahoji watoto waliofanyiwa vitendo hivyo ili kuepusha kuwatia hofu na kupelekea kutoa taarifa zenye mapungufu zinazoweza kuathiri mwenendo wa kesi katika hatua za awali.
Wakati huo huo Mhe Riziki amesema Wizara inalaani vikali juu ya tukio hilo na haitalifumbia macho, ambaoo ameahidi kuchukuliwa hatua za kisheria wakati mtuhumiwa wa tukio hilo atakapokamatwa.
Nao Maafisa Ustawi wa Wilaya mbali mbali za Unguja, wamesema pamoja na kutoa elimu ya kuihamasisha jamii kutokuficha makosa hayo yanapotokea lakini bado kumekuwa na vikwazo katika kufuatilia kesi hizo ikiwemo kukosa ushirikiano hasa kwa makosa ya udhalilishaji yanayofanyika ndani ya familia.
No comments:
Post a Comment