Habari za Punde

AFYA YAZIDI KUIMARIKA ZANZIBAR

Waziri wa Afya Zanzibar Mhe. Nassor Ahmed Mazrui akizungumza na  Ujumbe kutoka Kampuni ya Badea kuhusu mradi wa ujenzi wa Hospitali ya  Rufaa Mnazimmoja pamoja na ukarabati wa Jengo kongwe la Hospitali hiyo wakati walipofika Ofisini  kwake kujadili maendeleo ya mradi huo utakaogharimu jumla ya dola milioni 48 kutoka kwa  Serikali ya Mapinduzi Zanzibar wakishirikiana na Badea,mfuko wa misaada wa Kuweit na Saudiarabia.

Mwakilishi wa Badea Sameh Azzuz akizungumza na Waziri wa Afya Zanzibar Mhe. Nassor Ahmed Mazrui (hayumo Pichani)  wakati alipofika Ofisini kwake kujadili maenedeleo ya mradi wa ujenzi wa Hospitali ya rufaa Mnazimmoja pamoja na ukarabati wa Jengo kongwe la Hospitali hiyo  utakaogharimu jumla ya dola milioni 48 kutoka kwa  Serikali ya Mapinduzi Zanzibar wakishirikiana na Badea,mfuko wa misaada wa Kuweit na Saudiarabia.

Picha na Fauzia Mussa  –Maelezo  Zanzibar.

Na.Rahima Mohammed - Maelezo Zanzibar. 28.06.2022

Wizara ya afya inatarajia kujenga majengo mapya katika hospitali ya Rufaa Mnazimmoja pamoja na  kuifanyia matengenezo jengo kongwe katika  hospitali hiyo ili kuboresha zaidi huduma za Afya kwa Wananchi.

 

Hayo amesema Waziri wa Afya Mhe. Ahmed Mazrui wakati akizungumza na ugeni kutoka shirika la Badea huko ofisini kwake Mnazimmoja mjni Unguja walipofika kwa ajili ya kujadili maendeleo ya mradi wa ujenzi wa majengo mapya na kulifanyia ukarabati jengo kongwe.


Amesema mradi  huo utasaidia kuweka mazingira mazuri  zaidi ya hospitali hiyo kwani unaenda kuongeza idadi ya vyumba vya upasuaji,wodi za kulazia wagonjwa pamoja na sehemu za kutibia wagonjwa.

 

Aidha amesema mradi huo utasaidia kuongezeka upatikanaji tiba na kutaleta mageuzi makubwa katika sekta ya Afya   kwa kutoa huduma bora kwa jamii.

 

" Hospitali kuu ya Mnazi Mmoja itakuwa mpya yenye huduma zote muhimu za kuweza kuwahudumia wazanzibar "Alisema Waziri huyo.

 

Waziri Mazrui amesema kukamilika kwa ujenzi huo kutaimarisha  upatikanaji wa   huduma nyingi za afya , kupunguza vifo vya mama na mtoto pamoja na kupunguza wimbi la wagonjwa kwenda kutibiwa nje ya nchi.

 

Vilevile amesema kupitia mradi huo wataifanyia   ukarabati mkubwa hospitali ya wazazi Mwembeladu kwa kuweka mazingira mazuri , kuweka vifaa vya kisasa pamoja na ujenzi mdogo katika hospitali ya wagonjwa wa akili kidongo chekundu utakaosaidia kuongeza matibabu hospitalini hapo.

 

Nae Sameh Azzuz mwakilishi kutoka shirika la Badea amesema shirika lake liko tayari kushirikiana na wizara hiyo ili kuhakikisha afya za wazanzibar zinaimarika.

 

Mwakilishi huyo ameahidi kukamilika mradi huo kwa wakati licha ya kusimama kwa muda mrefu kutokana na changamoto ya maradhi ya UVIKO 19.

 

Mradi huo unafadhiliwa na serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kushirikiana na Shirika la Badea,na mfuko wa Quwait na Saudia Arabia ambapo jumla ya dola milioni 48 za kimarekani zitatumika kukamilisha ujenzi huo.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.