Habari za Punde

Dk. Mwinyi Ameushukuru Mfuko wa Misaada wa Sheikh Zayed Bin Sultan Al Nahyan kwa Kuiunga Mkono Zanzibar.

 

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi (katikati) akishuhudia utiaji saini Ujenzi miradi mitatu ya maendeleo baina ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na Taasisi ya Misaada ya Sheikh Zayed Al Nahyan kutoka Nchi za Jumuiya ya Falme za Kiarabu (UAE)hafla iliyofanyika Ikulu Jijini Zanzibar,wanaotia saini  (kulia) Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango Dkt.Juma Malik Akili na Katibu Mkuu wa Jumuiya hiyo Nd,Hamad Bin Kurdous Al-Amry (kushoto)

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi ameushukuru Mfuko wa Misaada wa Sheikh Zayed bin Sultan Al Nahyan kwa kuiunga mkono Zanzibar katika kuimarisha sekta ya afya, elimu pamoja na ustawi wa Jamii.

Rais Dk. Mwinyi alitoa shukurani hizo leo Ikulu Zanzibar mara baada ya kushuhudia utiaji saini kati ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar pamoja na Mfuko wa Misaada ya Sheikh Zayed bin Sultan Al Nahyan kutoka nchi za Jumuiya ya Falme za Kiarabu (UAE), ambapo mfuko huo utasaidia katika sekta ya elimu, afya na ustawi wa Jamii.

Akitoa shukurani hizo, Rais Dk. Mwinyi alisema kwamba Mfuko huo umechukua uwamuzi stahikli wa kuisaidia Zanzibar katika maendeleo yake ikiwa ni pamoja na azma ya kujenga skuli mbili, kituo cha wazee cha kisasa pamoja na Hospitali.

Aliongeza kuwa hatua hiyo itasaidia kwa kiasi kikubwa kuunga mkono juhudi za Serikali katika kuendeleza ujenzi wa miradi ya maendeleo unaotekelezwa hivi sasa.

Rais Dk. Mwinyi alitumia fursa hiyo kutoa shukurani kwa Rais wa nchi za Jumuiya ya Kiarabu (UAE) Sheikh Mohamed bin Zayed Al Nahyan kwa kuendelea kuiunga mkono Zanzibar katika kuimarisha miradi mbali mbali ya maendeleo.

Nae Waziri wa Fedha na Mipango Saada Mkuya Salum alieleza kuwa Mfuko huo wa Misaada wa Sheikh Zayed bin Sultan Al Nahyan una azma ya kujenga skuli mbili ikiwemo ya Muembeladu na Mtopepo, kituo cha kisasa cha wazee kitakachokuwa na nyumba za watendaji wake pamoja na kujenga hospitali. kisasa.

Waziri Mkuya alisema kuwa nchi za Jumuiya ya Kiarabu (UAE), zimekuwa na mahusiano mazuri na Zanzibar hivyo hatua hiyo itasaidia  utekelezaji wa mikakati katika maeneo aliyoyapa kipaumbe Rais Dk. Mwinyi.

Hivyo, aliahidi kwamba Wizara yake itahakikisha inatoa ushirikiano mkubwa kwa Taasisi hiyo ili iweze kufikia malengo iliyojiwekea.

Mapema Mkuu wa Taasisi hiyo ya Misaada ya Sheikh Zayed bin Sultan Al Nahyan,  Sheikh Hamad Salem bin Kardous Al Amer aalisema kwamba Jumuiya ya nchi za Falme za Kiarabu (UAE) ina uhusiano Mwema na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ikiwenmo Zanzibar.

Alisema kuwa misaada hiyo ni hatua za kiongozi mkuu wa nchi hiyo katika kuiunga mkono Zanzibar kwani anatambua uhusiano na ushirikiano uliokuwepo ambao kuna haja ya kuendelezwa na kudumishwa.

Aidha, kiongozi huyo alitumia fursa hiyo kumpongeza Rais Dk. Mwinyi kwa hatua zake za kuendeleza mahusiano na mashirikiano mema yalipo kati ya Zanzibar na (UAE) sambamba na ukarimu mkubwa alionao kwa nchi za Umoja huo.

Aliongeza kuwa hatua hiyo pia itasaidia kuanzisha ziara kati ya pande mbili hizo zitakazosaidia kuimarisha uhusiano na ushirikiano mkubwa uliopo huku akimuomba Mwenyezi Mungu kuipa Zanzibar maendeleo makubwa yenye amani ndani yake.

Zoezi hilo la utiaji saini lililoshuhudiwa na Rais Dk. Mwinyi lilifanyika kati ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Mfuko wa Misaada wa Sheikh Zayed bin Sultan Al Nahyan ambapo kwa upande wa Serikali alietia saini ni Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Fedha na Mipango Dk. Juma Malik Akil na kwa upande wa Mfuko huoa alietia saini ni Sheikh Hamad Salem bin Kardous Al Amer.

Viongozi mbali mbali walihudhuria akiwemo Spika wa Baraza la Wawakilishi Zubeir Ali Maulid, Balozi wa (UAE) nchini Tanzania Khaalifa Abdulrahman Mohamed Al Marzooqi, Mawaziri, Makatibu Wakuu, Wakuu wa Vikosi vya Ulinzi na Usalama, Mufti Mkuu wa Zanzibar Sheikh Saleh Omar Kabi, Kadhi Mkuu wa Zanzibar Sheikh Othman Ngwali, Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi Injinia Zena Ahmed Said, Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar Mwinyi Talib Haji, Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi Idrissa Kitwana Mustafa pamoja na viongozi wengine wa Serikali.

Imetayarishwa na Idara ya Mawasilaino,

Ikulu Zanzibar.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.