Habari za Punde

MAPISHI YA MWIKO MKUBWA

 
Na.Adeladius Makwega- BUJORA-MWANZA

Siku moja nilibanwa sana na njaa, kwa hiyo nilitafuta mboga yangu na kuichemsha haraka haraka mekoni, ilipoiva sikuiunga, niliichukua kama ilivyo nakuiweka kando ya jiko langu. Nikachukua sufuria na kuiweka maji mekoni, mara baada ya dakika kadhaa, maji haya yalichemka nakuweka unga katika sufuria hiyo iliyokuwa mekoni ili niusonge ugali.

Wakati nimeshaweka unga kwenye maji yalichemka nikaangalia mwiko wa kupikia ugali wangu sikuuona kabisa, tafuta huku na kule mwiko siuoni, nikasema leo mwanakwettu ninapika kwa kutumia nini? Kijiko na upawa wa chuma vinashika moto na pia haviwezi kuukamata ugali vizuri.

Ninafanyaje?

Akili yangu ilijiuliza mno, ahh gafla kwa mbele yangu kwenye kona na pahala ninapopika nikauona mwiko mkubwa, huku chini yake kukiwa na sufuria kubwa kadhaa za mapishi katika shughuli.

Nikauvuta huku ukipiga kelele,

Kwaaaaaaaaa!

Nilipoutoa tu nikauosha haraka haraka na kuanza kuusonga ugali wangu.

Kwa kuwa mwiko huu ulikuwa mkubwa na ugali uliokuwa wangu mwenyewe basi mwiko huu wa kupikia sufuri la watu kama mia uliukamata ugali vizuri na kuugeuza bila tabu na hata nilipokuwa nautumia kuusagasaga ugali ili kuondoa mabonge mabonge yenye unga ulifanya kazi hiyo vizuri sana.

Wakati naendelea kuusonga ugali huu, nikawa ninajiuliza huu mwiko wangu mdogo umekwenda wapi? Huu mwiko mkubwa ulifikajefikaje hapa?

Nilipata majibu kuwa mwiko mdogo pengine nimeutupa na uchafu na mwiko mkubwa kuwepo hapa nyumbani kwangu nikakumbuka nikiwa kijana sana bibi yangu mzaa baba anayeitwa Hedwiki Omari Binti Mkomangi aliniambiwa kuwa katika nyumba yako yoyote ile hakikisha unakuwa na mikeka mingi, sufuria kubwa na mifuniko yake na miko ya mikubwa kwa maana msiba, sherehe, ugonjwa na hata ugeni mkubwa ni nyumbani kwako ni dharura,

Kimoyomoyo nikasema hapa akija mtu akanikuta ninavyousonga ugali wa mtu mmoja kwa mwiko wakupikia watu mia atasema, “Katekista Makwega mbona unafanya israfu?”

Kwa hiyo ili somo la dharura la Binti Omari lilisababisha ninunue mwiko huo. Kumbuka nipo napika ugali msomaji wangu. Nikautenga ugali wangu nakuula polepole, bila tabu na ulikuwa ugali mtamu sana. Kwa hiyo tangu siku hiyo nikawa napikia ugali wangu kwa mwiko mkubwa hadi leo hii.

Ugali wangu ninaopika kwa mwiko mkubwa huwa una sifa kubwa tano kwanza lazima uive, pili huwa hauna mabonge mabonge, tatu chungu chake ninachopikia hakiungui hata wale mabingwa wa kula ukoko wanajinoma na tano na mwisho atayaeuonja tu lazima ale tangu tonge la kwanza hadi mwisho.

Huo ndiyo ugali wangu, ninaopika kwa kutumia mwiko mkubwa. Je yupo anayediriki kushinda na mimi kupika kwa kutumia mwiko wake mdogo?

Ha ha ha ha ha ha ha, nicheke mwanakwetu, hayupo.

Labda, tena labda mwanafunzi wangu hodari ambaye darasa hili la leo atafuzu, anaweza kushindana nami. Hata hivyo huyo mwanafunzi wangu hodari (yeye) atabaki kuwa mwanafunzi tu na mimi kubaki kuwa mwalimu wake.

Mwanakwetu upo?

Nakutakia siku njema.

makwadeladius@gmail.com

0717649257

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.