Katibu Mkuu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi, anayesimamia sekta ya Uvuvi, Dkt. Rashid Tamatamah (kushoto) na Meneja Mkuu, Kampuni ya ujenzi ya CHEC, Cheng Yongjian (kulia) wakisaini nyaraka za makubaliano ya ujenzi wa bandari ya uvuvi ya Kilwa katika hafla fupi ya utiaji saini iliyofanyika jijini Dodoma Jana. Katikati ni Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki. Kushoto kwa Waziri ni Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji, Mhe. Dkt. Christina Ishengoma.
Katibu Mkuu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi, anayesimamia sekta ya Uvuvi, Dkt. Rashid Tamatamah (kushoto) akipeana mkono na na Meneja Mkuu, Kampuni ya ujenzi ya CHEC, Cheng Yongjian (kulia) ikiwa ni ishara ya makubaliano baada ya kusaini nyaraka za makubaliano ya ujenzi wa bandari ya uvuvi ya Kilwa katika hafla fupi ya utiaji saini iliyofanyika jijini Dodoma.
Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki akitoa hotuba katika hafla fupi ya utiaji saini wa nyaraka za makubaliano ya ujenzi wa bandari ya uvuvi ya Kilwa baina ya serikali na Kampuni ya ujenzi ya China Habour Engineering Company (CHEC) iliyofanyika jijini Dodoma Jana. Kulia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji, Mhe. Dkt. Christina Ishengoma na kushoto ni Katibu Mkuu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi, anayesimamia sekta ya Uvuvi, Dkt. Rashid Tamatamah.
Na Mbaraka Kambona,
Serikali imeingia makubaliano ya kuanza ujenzi wa bandari ya uvuvi ya Kilwa na Kampuni ya ujenzi ya China Habour Engineering Company (CHEC) katika hafla fupi ya kusaini mkataba wa makubaliano iliyofanyika jijini Dodoma Jana.
Wakati akiongea na Uongozi wa kampuni ya ujenzi ya CHEC,
Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki alisema mradi wa ujenzi wa
bandari ya uvuvi utakaoanza hivi karibuni Wilayani Kilwa, Mkoani Lindi
utachochea ukuaji wa uchumi wa buluu na kupelekea sekta ya uvuvi kuwa na
mchango mkubwa katika pato la taifa.
Alisema kuwa anamshukuru Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan kwa
kukubali kwake kujenga bandari hiyo kwa fedha za ndani huku akiongeza kuwa
kukamilika kwa bandari hiyo kutakuwa na faida nyingi za kiuchumi kwa wavuvi,
wananchi na taifa kwa ujumla.
“Namshukuru Mhe. Rais kwa kukubali kufanya jambo hili ambalo
lilikuwa ndoto sasa kuwa kweli, amekubali kutoa jumla ya shilingi za Kitanzania
bilioni 266.79 kwa ajili ya ujenzi wa bandari hii pamoja na miundombinu mingine
ikiwemo soko la kisasa la samaki”, alisema
Aliongeza kwa kusema kuwa bandari hiyo ikikamilika itakuwa
na uwezo wa kuhifadhi tani Elfu 60 kwa mwaka za mazao ya uvuvi kutoka katika ukanda wa bahari ya hindi huku
akisisitiza kuwa bandari hiyo itakuwa kubwa kuliko zote zilizopo katika pwani
ya Afrika Mashariki.
Waziri Ndaki alifafanua kwamba uwepo wa bandari hiyo ambayo
imesubiriwa tangu nchi ipate uhuru
itasaidia kuinua uzalishaji wa mazao ya uvuvi kwa wingi kutoka katika ukanda
huo wa bahari tofauti na ilivyo sasa ambapo mazao mengi yanayotumika yanatoka
katika ukanda wa ziwa ikiwemo ziwa Viktoria na
ziwa Tanganyika.
“Uwepo wa bandari hii pia kutasaidia kuvutia wawekezaji
wengine katika nyanja mbalimbali ikiwemo viwanda vya kuchakata mazao ya samaki
na hivyo itasaidia kutoa ajira kwa wananchi na kukuza uchumi wa nchi”,aliongeza
Aidha, Waziri Ndaki aliutaka uongozi wa Kampuni ya CHEC
ambao ndio wamepewa Kandarasi ya kujenga bandari hiyo kuhakikisha ujenzi huo
unakamilika ndani ya muda uliopangwa kwa sababu pesa kwa ajili ya kufanya kazi
hiyo zipo hivyo hawatavumilia udhuru wowote utakaopelekea kuchelewesha mradi
huo.
Naye, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo,
Mifugo na Maji, Mhe. Dkt. Christina Ishengoma aliihimiza wizara kuhakikisha
wanamsimamia vyema mkandarasi aliyekabidhiwa kujenga bandari hiyo huku
akiongeza kuwa wao kama kamati watakuwa wanafuatilia kwa karibu kuhakikisha
mradi huo unakamilika kwa wakati ili watanzania waone matunda ya pesa yao.
Kwa upande wake, Meneja Mkuu, Kampuni ya ujenzi ya CHEC,
Cheng Yongjian alisema kuwa mradi huo ni muhimu kwa serikali ya Tanzania hivyo
kwa kutumia uzoefu walionao wanaimani kwamba watakamilisha ujenzi wa bandari
hiyo ndani ya muda uliopangwa.
Awali akitoa taarifa fupi kuhusu mchakato wa ujenzi wa
bandari hiyo, Katibu Mkuu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi, anayesimamia sekta ya Uvuvi, Dkt. Rashid Tamatamah alisema
kuwa kutokuwapo kwa bandari ya uvuvi kumepelekea nchi kupoteza mapato mengi
yatokanayo na sekta ya uvuvi kwa sababu Meli kubwa zinazofanya uvuvi katika
ukanda maalum wa bahari hapa nchini zimekuwa zikishusha shehena ya samaki
katika nchi jirani na hivyo kupelekea nchi hizo kunufaika zaidi kuliko
Tanzania.
No comments:
Post a Comment