Habari za Punde

Mti Ulioitika Tabia za Binadamu.

 

Na.Adeladius Makwega-IGOMA                                                                                                                                                                                                                                                  Juni 18, 2022 niliingia katika jiji la Mwanza na kufika moja kwa moja makutano ya barabara tatu Nyerere, Makongoro na Kenyatta. Kando ya makutano hayo katikati ya barabara kuna kisiki cha mti uliokatwa na kukauka vizuri.

Nilikisogelea kisiki hicho nikiwa na wenzangu kadhaa, tulikikagua kwa pamoja, huku maswali yakiibuka. Hiki kisiki mbona kimepambwa mno? Je ni kisiki halisi au kisiki bandia?

“Mti huu umekauka ndiyo uliokuwa ukitumika kunyongea watumwa waliochoka, kuumwa na baadhi ya watu walioonyesha kukaidi serikali ya Kijerumani hata ile ya Waingereza baadaye. Madhira haya ni yale ya enzi za biashara ya utumwa na wakati wa utawala wa wakoloni, wale wote waliowapinga walikatishwa uhai wao hapo kwa kunyongwa hadharani. Baadhi ya Waafrika waliokuwa wabunifu katika uhunzi, ushonaji na ususi walikatwa mikono chini ya mti huu”.

Hayo yalisimuliwa na mzee mashuhuri wa jiji la Mwanza ambaye jina lake limehifadhiwa. Pia, maelezo haya yalishadidiwa na Dkt Mnata Resani Mkurugenzi Msaidizi Lugha Wizara ya Utamaduni Sanaa na Michezo ya Tanzania ambaye pia alipata kusimuliwa hadithi ya mti huu.

“Watumwa walipofika hapa walikuwa wanapumzika, wale waliochokachoka walinyongwa ili wasibaki hai au wale waliokuwa wakisingizia ugonjwa. Hiyo ilikuwa adhabu madhubuti ili kila mtumwa ajitahidi awezavyo awe mzima hadi mwisho wa safari.”

Bila hiyana mzee huyu aliyevalia koti la Kaunda lililochujuka ambaye alionekana kuwa mtulivu sana, muelewa mno, kama aliwahi kuwa mtumishi wa umma ujanani vile, aliendelea kusema;

“Siyo kisiki halisi, bali ni kisiki bandia ambacho kilitenengezwa na kampuni moja kama kumbukumbu ya mti huo uliokuwa ukitumika kunyongea enzi za utumwa, enzi za wakoloni.”

Mzee huyu alituvuta kando ya kisiki bandia hicho kama hatua nne za mtu mzima akatuonyesha mti ambao ulikuwa unachipuka akisema kuwa mti halisi ulikuwa MKUYU huu hapa sasa umeanza kuchipua majani yake baada ya ule mti mkongwe kuanguka na kuondolewa. Aliendelea kusema;

“Tunachoshangaa kwa sasa mti huu umeanza kuchipua kidogo kidogo, kuna wakati uliota lakini ukakatwa na watu kimakosa lakini unachipua tena kupitia mizizi ya mti huo wa asili.”

Hata waliojenga hiki kisiki bandia walidhania mti huu umekufa, walifanya hisani kulinda kumbukumbu ya historia hiyo lakini la kustajabisha mti huo unachipua kwa kasi.

Baada ya maelezo haya Dkt Julieth Kabyemela ambaye ni Mkurugenzi Msaidizi anayeshugulikia Urithi wa Utamaduni na Maadili ya Taifa na Lilian Firimin Shayo Afisa Utamaduni Mwandamizi wote wa Wizara ya Utamaduni , Sanaa na Michezo na walipiga picha na mti huo kuhifadhi kumbukumbu yake ambapo sasa unachipuka kwa kasi mno ukiwa na urefu unaokaribia sentimeta 30.

Nilipotoka hapo binafsi nilitafakari mambo mengi juu ya mti huo; kwanza mti huo namna ulivyokuwa ukinyonga watumwa waliokuwa wamedhoofu kihali na kiafya safarini, halafu mti huo huo ulitumika kunyonga watu waliotazamwa kama wakorofi wakati wa utawala wa wakoloni, na wale wabunifu na wadadisi ili kurudisha na kudumaza tekinolojia ya Mwafrika.

Tafakari yangu kubwa zaidi na ya msingi ipo katika dhana ya kuwekwa kwa kisiki bandia cha mti huo, sasa mti huo ulioanguka, unachipuka, kuonyesha falsafa za wazee wetu kuwa,

“Historia huwa haizikwi”.

“Katika dunia ukifanya baya au zuri usidhani yamepotea yatarudi tu bila ya wewe kufahamu, ukiwa hai au hata kwa kizazi chako. Ule wema /ubaya utajidhihirisha wenyewe kama mti huu wa kunyongea sasa unapochipuka tena na kile kisiki bandia kinapokosa kazi.

Mwanakwetu naiweka kalamu yangu chini nikiwa hapa Igoma Mwanza kwa kusema kuwa kumbuka kuchagua ya kutenda yawe mema au mabaya yote ni mbegu. Unapoona katika familia zetu za Kiafrika tunatoa majina kwa watoto wetu kutokana na majina ya wahenga wetu wa awali, hii ni njia ya kuhifandhi historia za wazee wenye majina husika. Mti huu umeitikia tabia za binadamu.

makwadeladius@gmail.com

0717649257 .                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                 

 

J

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.