Habari za Punde

Tanzania na Saudi Arabia Zaahidi Ushirikiano Katika Elimu.

Balozi wa Saudi Arabia nchini, Mhe. Abdullah Ali Alsheryan akizungumza na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam
Mazungumzo baina ya Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk na Balozi wa Saudi Arabia nchini, Mhe. Abdullah Ali Alsheryan katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk akipokea zawadi kutoka kwa Balozi wa Saudi Arabia nchini, Mhe. Abdullah Ali Alsheryan katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk katika picha ya pamoja na Balozi wa Saudi Arabia nchini, Mhe. Abdullah Ali Alsheryan pamoja na maafisa kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki na Ubalozi wa Saudi Arabia hapa nchini

Na Mwandishi Wetu, Dar

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Ufalme wa Saudi Arabia zimeahidi kuendelea kushirikiana na kukuza sekta elimu kwa manufaa ya mataifa yote mawili.

Ahadi hiyo imetolewa na Balozi wa Saudi Arabia nchini, Mhe. Abdullah Ali Alsheryan alipokutana kwa mazungumzo na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk (Mb) leo katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam 

Balozi Alsheryan amemhakikishia Balozi Mbarouk kuwa Saudi Arabia itaendelea kushirikiana na Tanzania katika kukuza na kuendeleza sekta ya elimu ambapo kwa mwaka 2022 Saudi Arabia imetoa fursa za ufadhili wa masomo kwa wanafunzi 80 wa kada mbalimbali. 

“Serikali yetu kwa kutambua mchango wa elimu, imetoa ufadhili wa masomo kwa wanafunzi 80 wa kitanzania, hivyo ni rai yangu kwa watanzania kuchangamkia fursa hizo pindi zitakapotangazwa,” alisema Balozi Alsheryan

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk ameahidi kuwa Tanzania itaendelea kushirikiana na Saudi Arabia katika kukuza na kuendeleza ushirikiano imara baina ya mataifa hayo uliodumu kwa muda mrefu. 

“Uhusiano wa Tanzania na Saudi Arabia umezidi kuimarika, pia tumefurahishwa na fursa za ufadhili wa masomo kwa wanafunzi wetu na tunaahidi kutumia fursa hiyo kwa maendeleo ya taifa letu” amesema Balozi Mbarouk.

Ushirikiano wa Tanzania na Saudia Arabia ni wa muda mrefu ambapo mataifa hayo yamekuwa yakishirikiana katika Nyanja za nishati na gesi, madini, utalii na kilimo, afya, elimu na kiutamaduni.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.