Habari za Punde

Timu ya KMKM Kupata Uenyeji Nchini Norway.

Mwenyekiti wa Klabu ya KMKM, Capt. Khatibu Khamis Mwadini akimkabidhi hati ya mapendekezo ya makubaliano Mratibu wa Kampuni ya Kimataifa ya JHIL Enterprises, Ismail Shah.
Mratibu wa Kampuni ya Kimataifa ya JHIL Enterprises, Ismail Shah, akizungumza na uongozi wa Klabu ya KMKM katika hafla ya kuzungumza juu ya makubaliyano ya kuisaidia klabu ya KMKM iliyofanyika Makao Makuu, Kibweni.

Katibu wa klabu ya KMKM, Sheha Mohamed Aliakiwakaribisha na kuwatembeza wageni wao kutoka Norway katika Klabu hiyo Maisara walipofika kuona mazingira ya klabu hiyo.

Na Makame Mshenga

Kampuni ya kimataifa ya JHIL inayojenga uwanja wa Kimataifa wa Cricket na michezo mingine katika kijiji cha Fumba Zanzibar, inakusudia kuisaidia Klabu ya KMKM, kubadilishana uzoefu na kuwatafutia soko la Ulaya wachezaji wake.

 

Mratibu wa Kampuni hiyo Ismail Shah alisema kwa kuwa mradi wa viwanja vya michezo Fumba utajumuisha pia uwanja wa soka hivyo ni vyema kuanza taratibu mapema ili kabla ya viwanja kujengwa programu mbali mbali za kuimarisha soka ziwe zimeanza.

 

Alisema wameichagua KMKM kwa vile klabu hiyo imejipanga vyema katika michezo mingi ikiwemo mchezo wa soka. 

 

Mwenyekiti wa Bodi ya Kampuni ya JPM Sports na Mtendaji Mkuu wa Klabu ya Viking FC ya Norway, Eirik Henningsen alisema kupitia makubaliano na KMKM watakuwa na utaratibu wa kubadilishana uzoefu ambapo wachezaji, makocha na wataalamu wa KMKM watakwenda Norway kujifunza na wale wa Norway watakuja Zanzibar.

 

Mwenyekiti wa Klabu ya KMKM Capt. Khatibu Khamis Mwadini, aliushukuru ugeni huo na kusema kuwa umekuja muda muafaka wakati klabu ya KMKM ambayo ni bingwa wa ligi kuu ya Zanzibar ikijiandaa kwa michezo ya kimataifa.

 

Alimshukuru  Rais wa Zanzibar Dk. Hussein Mwinyi kwa kusaidia kupatikana wataalamu hao ambao watasaidia kuleta mabadiliko katika sekta ya michezo nchini.

 

Katibu wa klabu ya KMKM, Sheha Mohamed Ali, alisema ana matumaini makubwa kuwa wataalamu hao watakuwa chachu ya mabadiliko ya michezo mingi nchini jambo ambalo litaing’arisha Zanzibar katika medani ya michezo.

 

Aidha alisema watatoa kila aina ya ushirikiano unaohitajika kuhakikisha malengo yaliyopangwa yanaweza kutimia kwa wakati.

 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.