Habari za Punde

Wamiliki wa Viwanda Watakiwa Kutenga Fungu la Kusaidia Utunzaji Mazingira.

 

Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Khamis Hamza Khamis akiwa katika ziara ya kikazoi ya kukagua uzingatiaji wa sheria ya mazingira katika kiwanda cha mafuta ya alizeti cha Pyxus kilichopo eneo la Kizota jijini Dodoma leo Juni 18, 2022.

Wamiliki wa viwanda watakiwa kutenga fungu la kusaidia utunzaji mazingira

Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Khamis Hamza Khamis ametoa rai kwa wamiliki wa viwanda nchini kutenga fungu kwa ajili ya shughuli za kimazingira.

Ametoa rai hiyo leo Juni 18, 2022 alipofanya ziara ya kikazi ya kujionea uzingatiaji wa sheria ya mazingira katika kiwanda cha kuzalisha mafuta ya alizeti cha Pyxus kilichopo eneo la Kizota jijini Dodoma.

Mhe. Khamis alisema kuwa mataifa mbalimbali yaliyoendelea hutoa fedha kwa nchi zinazoendelea kwa kutambua kuwa wao ndio chanzo cha uharibifu wa mazingira kutokana na hewa ya ukaa wanayozalisha.

Alisema viwanda havina budi kuchangia shughuli za mazingira na za kijamii kwa ujumla zikiwemo upandaji miti, utoaji elimu kuhusu uhifadhi na utunzaji wa mazingira.

“Nawapongeza kiwanda hiki cha Pyxus nimesiki mnafanya shughuli za kupanda miti katika eneo lenu hivyo natoa wito kwa viwanda vingine nchini viwe na utaratibu huu ili tuhakikishe tunatunza mazingira,” alisema.

Aidha, naibu waziri huyo aliagiza wamiliki wa viwanda vyote nchini viwe na mfumo mzuri wa kutibu na kudhibiti majitaka ili kuhakikisha hayatiririki na kumwagika kwenye makazi ya watu hali inayoweza kuhatarisha afya na mazingira.

Sambamba na hilo pia alielekeza viwanda vidhibiti moshi unaotokana na shughuli za viwandani usisambae katika makazi ya watu hali inayoweza kuwasababishia matatizo ya kiafya. Alielekeza pia viwanda vidhibiti kelele zinazotokana na mashine za viwandani zisiwe kero kwa wananchi kwani zinaweza kuwasbabishia matatizo ya masikio.

Kwa upande wake Meneja Rasilimaliwatu wa kiwanda cha Pyxus Bw. Gideon Mutta alisema uongozi wa kiwanda hicho umepokea maelekezo hayo na kuahidi yatashughulikwa.

Hata hivyo, alisema wana changamoto ya miundombinu ya mfumo wa majitaka ambapo kutokana na hali hiyo aliomba Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mjini Dodoma (DUWASA) kuwasaidia na kuona namna ya kuwaungasnishai na mfumo wa Jiji la Dodoma.  

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.