Habari za Punde

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Mwinyi Amekutana na Kuzungumza na Waziri Mkuu Mstaafu wa Uingereza Bw. Tony Blair Ikulu Zanzibar.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Hussein Ali Mwinyi (katikati) akisalimiana na Waziri Mkuu Mstaafu wa Uingereza Mhe.Tony Blair alipofika Ikulu Jijini Zanzibar leo kwa mazungumzo akiwa na ujumbe wake.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Hussein Ali Mwinyi (katikati) akisisitiza jambo leo wakati alipokuwa na mazungumzo na   Waziri Mkuu Mstaafu wa Uingereza Mhe.Tony Blair alipofika Ikulu Jijini Zanzibar  kwa mazungumzo akiwa na ujumbe wake.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Hussein Ali Mwinyi (kuliai) akiaagana na mgeni wake   Waziri Mkuu Mstaafu wa Uingereza Mhe.Tony Blair baada ya mazungumzo yao leo alipofika Ikulu Jijini Zanzibar  akiwa na ujumbe wake.
[Picha na Ikulu] 05/07/2022.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi amefanya mazungumzo na Waziri Mkuu wa zamani wa Uingereza Tony Charles Blair ambapo kiongozi huyo ameahidi kuendelea kuiunga mkono Zanzibar.

Mazungumzo hayo yamefanyika leo Ikulu Zanzibar ambapo Rais Dk. Mwinyi alimpongeza Waziri Mkuu huyo wa zamani wa Uingereza ambaye yuko Zanzibar kwa ziara maalum ya siku moja kwa utayari wake wa kuendelea kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Katika mazungumzo hayo, Rais Dk. Mwinyi alieeleza kwamba ujio wa kiongozi huyo kwa mara nyengine tena hapa Zanzibar unaonesha ni kwa jinsi gani ana azma ya kuisaidia Zanzibar sambamba na kuonesha ushirikiano wake mkubwa.

Aidha, Rais Dk. Mwinyi alimueleza kiongozi huyo mipango mikubwa iliyofikiwa katika kuanzisha Kitengo cha ufuatiliaji na tathmini.

Aidha, Rais Dk. Mwinyi aliendelea kuipongeza taasisi ya Tony Blair ya Mabadiliko Ulimwenguni (Tony Blair Institute for Global Change),kwa kuendelea kushirikiana vyema na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuhakikisha inaimarisha vipaumbele vyake katika sekta kadhaa ikiwemo uchumi wa buluu, utalii, na miundombinu.

Pamoja na hayo, Rais Dk. Mwinyi alimuhakikishia kiongozi huyo kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaedelea kufanya kazi pamoja na timu ya taasisi yake ili kufikia lengo lililokusudiwa katika kuiletea maendeleo Zanzibar.

Kwa upande wake Waziri Mkuu huyo wa zamani wa Uingreza Tony Charles Blair amemuhakikishia Rais Dk. Mwinyi kwa taasisi yake itaendelea kushirikiana na Zanzibar kwani inaziona juhudi za Rais Dk. Mwinyi anazozichukua katika kuijenga Zanzibar pamoja na watu wake.

Waziri Mkuu huyo mstaafu alimueleza Rais Dk. Mwinyi kwamba taasisi yake itahakikisha kwamba program zote zilizokusudiwa zinatekelezwa tena kwa ufanisi mkubwa.

Kiongozi huyo alieleza azma ya taasisi yake ya kuunga mkono juhudi za kukiimarisha kitengo cha ufuatiliaji na tathmini ili kuweza kuleta manufaa katika vipaumbele vilivyowekwa.

Mapema kiongozi huyo akiwa na ujumbe wake alifanya mazungumzo na Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi Muhandisi Zena Ahmed Said ambapo katika mazungumzo hayo Waziri Mkuu huyo wa zamani wa Uingereza aliahidi ushirikiano katika kutayarisha na kuanzisha Kitengo cha ufuatiliaji na tathmini.

Sambamba na hayo, Mhandisi Zena alieleza hatua zilizofikiwa katika uanzishwaji wa kitengo hicho cha ufuatiliaji na tathmini huku akieleza matumaini yake kwamba lengo lililokusudiwa litafikiwa hasa kwa kuzingatiwa kwamba ndani ya Serikali ushiriki wa kila mmoja unahitajika.

Imetayarishwa na Idara ya Mawasiliano,

Ikulu Zanzibar.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.