Habari za Punde

WAZIRI DKT MABULA AZUIA UPANGISHAJI ARDHI MASHAMBA MATATU MONDULI

 

Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akiwasili wilayani Monduli kwa ajili ya kushughulikia mgogoro wa mashamba ya Steyn wakati wa ziara yake ya siku mbili mkoani Arusha tarehe 4 Julai 2022.

Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akizungumza na Askari wa Mamlaka ya Wanyamapori Tanzania (TAWA) katika mashamba ya Steyn  wilayani Monduli wakati wa ziara yake ya siku mbili mkoani Arusha
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akizungumza na Askari wa Mamlaka ya Wanyamapori Tanzania (TAWA) katika mashamba ya Steyn  wilayani Monduli wakati wa ziara yake ya siku mbili mkoani Arusha
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akiangalia sehemu ya mashamba ya Steyn yaliyopo wilayani Monduli mkoani Arusha wakati wa ziara yake ya siku mbili mkoani humo 

 

Na Munir Shemweta, WANMM MONDULI

 

Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula amezuia mkataba wa upangishaji ardhi wa mashamba matatu maarufu kama mashamba ya Steyn yaliyopo wilayani Monduli mkoani Arusha ulioingiwa kati ya halmashauri ya wilaya ya Monduli na kampuni ya EBN Hunting Safaris.

 

Uamuzi huo unafuatia halmashauri ya wilaya ya Monduli kuingia mkataba wa kufanya uwekezaji kwenye mashamba hayo ulioibua mkanganyiko baina ya Ofisi ya Msajili wa Hazina na halmashauri ya wilaya ya Monduli kutokana na ofisi ya Msajili kutokamilisha wala kutoa shamba hilo  kwa mtu ama mamlaka yoyote.

 

Hatua ya halmashauri kutafuta mwekezaji kwenye mashamba hayo ulitokana na ufutwaji mashamba uliofanywa na Rais wa Serikali ya Awamu ya tatu Hayati Benjamin Mkapa kupitia tangazo la serikali la mwaka 2005 kwa lengo la upanuzi wa mji wa Makuyuni.

 

Mashamba ya Steyn ni muunganiko wa mashamba matatu ya Lente estate, Amani na Loldebes yenye ukubwa wa ekari 15,163 yaliyopo wilayani Monduli ambapo katika kipindi cha miaka ya 70 raia waliomiliki mashamba hayo waliondoka nchini na kuyaacha kumilikiwa na Bw. Hermanus Steyn kupitia kampuni ya Rift Valley Seed Company Ltd.

 

Akitoa maamuzi hayo baada ya kukagua mashamba hayo akiwa katika ziara yake ya siku mbili mkoani Arusha, Dkt Mabula alisema mashamba hayo kwa mujibu wa sheria ya masuala ya utwaaji yako chini umiliki wa Msajili wa Hazina hivyo uongozi wa wilaya ya Monduli ulitakiwa kuomba kibali cha matumizi ya eneo baada ya kutwaliwa.

 

‘’kuanzia sasa halmashauri itambue eneo hili litakuwa chini ya usimamizi wa Maliasili na Utalii na wamewapa TAWA kwa ajili ya kuona namna ya kuliendesha’’ alisema Dkt Mabula

 

Alisema, mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Monduli alipaswa kujiridhisha kuhusu umuliki wa mashamba hayo kabla ya kuanza mchakato wa upangishaji uliohitimishwa na yeye pamoja na mwenyekiti wa halmashauri kusaini mkataba huo.

 

Awali Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Monduli Isack Joseph katika kikao cha ndani alimueleza Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Mabula kuwa, uamuzi wa halmashauri yake kuingia mkataba wa kukodisha mashamba hayo kwa muwekezaji ulitokana na halmashauri kutokuwa na chanzo chochote cha mapato cha uhakika.

 

‘’Ukiangalia wilaya hii hakuna sehemu yoyote tunahemea kama wilaya kwa hiyo tulipokaa na kutafakari kama baraza tukaona kuna eneo ambalo serikali kimsingi liko chini yetu kwanini tusiweke mikakati ya kutafuta muwekezaji ili tutengeneze pesa kwa ajili ya makusanyo’’ alisema Mwenyekiti wa halmashauri ya Monduli.

 

Akielezea zaidi kuhusu utata wa uingiaji mkataba huo, Dkt Mabula alisema kuwa, maombi ya awali ya kampuni ya EBN Hunting Safaris Ltd yalikuwa kupangishwa kwa kipindi cha miaka 30 lakini pamoja na muda kupumguzwa hadi miaka 18 bado hali hiyo haitoi uhalali wa mkurugenzi na mwenyekiti kusaini mkataba ulioashiria mashaka juu ya usalama wa rasilimali za taifa.

 

Mkataba kati ya halmashauri na kampuni ya EBN Hunting Safaris Ltd ulisainiwa mwezi Mei 2022 na ulikuwa wa miaka 18 ambapo malipo yalikuwa kwa mwaka ni Tsh milioni 250 na iliamuliwa katika malipo hayo asilimia 60 ilipwe halmashauri na asilimia 40 ilipwe ofisi ya Msajili wa Hazina.

 

Mashamba ya Steyn hajaendelezwa na ni mapori yenye wanyama mbalimbali kutoka ikolojia ya eneo husika kuzungukwa na maeneo ya hifadhi za Manyara, Tarangire na pori tengefu la mto wa mbu ambapo wanyama hutumia eneo hilo kama ushoroba.

 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.