Habari za Punde

DKT. CHAULA ATAKA UBUNIFU UENDESHAJI MAKAZI YA WAZEE

 

Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dkt. Zainab Chaula akizungumza na Wazee wanahudumiwa katika Makazi ya Wazee Sukamahela Wilayani Manyoni mkoani Singida alipotembelea Makazi hayo Agosti 4, 2022.

Na  WMJJWM Manyoni Singida 


Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dkt. Zainab Chaula amewataka Maafisa Wafawidhi wa Makazi ya Wazee yanayohudumiwa na Serikali kuwa wabunifu katika uendeshaji wa Makazi hayo kwa kuwa na miradi mbalimbali itakayowezesha Wazee kupata huduma bora zaidi.


Dkt. Chaula ameyasema hayo  aipotembelea na kukagua huduma zinazitolewa katika Makazi ya Wazee Sukamahela Wilayani Manyoni mkoani Singida Agosti 4, 2022.


Dkt. Chaula amesema kuwa Serikali kupitia Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum inahudumia jumla ya Makazi 14 yaliyopo katika Mikoa ya Tanzania Bara kwa kutoa huduma za Msingi kwa Wazee hao zikiwemo chakula na matibabu.


Ameongeza kuwa lengo la Serikali ni kutoa huduma kwa wazee hasa wasiojiweza hivyo wasimamizi wa Makazi hayo wakiwa wabunifu itasaidia kuwa na Makazi bora zaidi kwani kutakuwa na utoaji huduma bora kwa wazee hao.


Akitoa taarifa ya Makazi ya Wazee Sukamahela Wilayani Manyoni mkoani Singida Afisa Mfawidhi wa Makazi hayo Yolanda Komba alisema Makazi hayo mbali na kupokea fedha za huduma ya Chakula kutoka Serikalini pia wameanzisha miradi mbalimbali ikiwemo ufuguaji wa mbuzi na bustani za mbogamboga inayosaidia kuboresha huduma katika Makazi hayo.


Ameongeza kuwa Makazi hayo yanahudumia jumla ya Wazee 16 wanaopata huduma za Chakula na matibabu katika eneo lenye ukubwa wa ekari 80 lenye nyumba 50 za kuishi.


Naye Mwenyekiti wa Wazee katika Makazi ya Wazee Sukamahela Wilayani Manyoni mkoani Singida Mzee Andrea Yohana ameiomba Serikali kuendelea kuwapatia huduma Wazee kwa kuwatunza na kuwalinda dhidi ya vitendo vya ukatili dhidi yao huku akiomba utoaji wa elimu kwa jamii kuwatunza Wazee 


Mwenyekiti wa Baraza la Wazee Taifa na Mwenyekiti wa Baraza la Wazee Singida Yustina Ngaiza aishukuru Serikali kwa kuendesha na kusimamia Makazi ya Wazee kwani yamekuwa msaada mkubwa kwa Wazee wasiojiweza na wasiokuwa na ndugu kupata huduma muhimu zikiwemo chakula na matibabu.


Akizungumza katika ziara hiyo Afisa kutoka Ofisi ya Rais TAMISEMI Ziada Nkinda  alisema Ofisi hiyo itashirikiana na Wizara ya kisekta katika kuhakikisha Wazee wanapata huduma bora hasa huduma za Afya na kuhakikisha Yale ambayo yamepangwa katika kuwahudumia Wazee yanatekelezwa kwa ufanisi mkubwa.


Wakati huo huo Katibu Mkuu Dkt. Chaula ametoa vifaa vya kuendeleza mradi wa bustani za mbogamboga na kuwawezesha vijana wanaofanya kazi za kujitokeza katika Makazi hayo kupata mradi wa kufuga kuku zaidi ya mia Moja.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.