Habari za Punde

Kituo cha Kusaidia Sekta ya Utalii Kwa Wananchi

Serikali itaendendelea kushirikiana na taasisi binafsi katika kuwaletea wananchi maendeleo pamoja na kukuza Uchumi wake.

Kauli hiyo imetolewa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla wakati wa ufunguzi wa kituo cha kukuza ujuzi kwenye sekta ya Utalii (ZENJ CENTER OF EXCELLENCE FOR TOURISM- AND HOSPITALITY) kilichopo Michamvi Kae Mkoa wa Kusini Unguja.

Amesema kuwepo kwa kituo hicho kitasaidia kukuza sekta ya utalii kwa wananchi wa maeneo hayo na maeneo jirani watakao fika kujifunza.

Amesema kuwepo kwa taassisi hii Zanzibar ni ishara ya taasisi binafsi kuiunga mkono serikali ya awamu ya nane inayoongozwa na dkt Husein Ali Mwinyi kwenye sera ya uchumi wa bluu kwani sera hii inahitaji ushirikiano baina ya serikali kuu na sekta binafsi.

Mhe. Hemed ameeleza kuwa taasisi hii itawasaidia wananchi wa Zanzibar kupata ajira za muda mrefu zitakazowasaidia  kufanya shughuli zao kupitia sekta ya kitalii na kupelekea kukuza uchumi kwa kupitia wageni wanaoingia na kutoka nchini.

Aidha makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar ameeleza kuwa serikali itaendelea kuwakaribisha wawekezaji kuekeza Zanzibar hasa katika sekta ya utalii kwa maslahi ya wazanzibari.

Aidha Mhe. Hemed amewataka wanafunzi wa kituo  hicho kuutumia ujuzi na taaluma watakaopatiwa ili kuendana na soko la utalii duniani.

Amesema kuwa Zanzibar ni nchi pekee ulimwenguni iliyobarikiwa kuwa na vivutio vingi vya kihistoria, hali ya hewa nzuri fukwe za kuvutia hivyo ni vyema kuvitumia vitu hivyo ili kuweza kujiajiri na kuvitangaza kukuza soko.

Nae waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Mhe.Leila Mohammed Mussa amesema kuwa serikali tayari imeshatoa kibali kwa kituo hicho kuanzisha masomo kwani kinaendana na Sera ya Serikali kuwainua vijana kimaendeleo.

Mhe Leila amewaomba wamiliki wa kituo hicho kuhakikisha hatua zilizobaki ili kuweza kufanya mitihani ya mazunzo Amali (VTA) na Kuwataka kuanzisha vituo kama hivyo katika kisiwa cha Pemba kwa lengo la kuwakomboa vijana kutoka kwenye utegemezi na kuweza kujiajiri pindi wamalizapo masomo yao.

Kwa upande wake mwenyekiti wa kituo hicho Ndugu.Toufiq Turky amesema malengo makuu ya kituo hicho ni kuiunga mkono serikali kuu kwa kuwapatia mafunzo ya amali vijana hasa katika sekta ya utalii ili kuweza kujiajiri.

Amesema kuwa idadi ya wanafunzi 27 kutoka Unguja na Pemba wameshaanza kupatiwa mafunzo ya utalii na tayari mahoteli mbali mbali nchini tayari yameshajitokeza kutaka kuwaajiri vijana hao pindi watakapomaliza mafunzo yao.

OFISI YA MAKAMU WA PILI WA RAIS

27/08/2022

Ali Moh’d

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.