Habari za Punde

Kiwanda cha Chai Mponde Chakamilika kwa Asilimia 95%

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Ajira, Vijana na Watu Wenye Ulemavu), Mhe. Profesa Joyce Ndalichako (Watatu kulia), akiangalia Chai iliyochakatwa wakati w amajaribo ya awali ya kiwanda cha Chai Mponde alipokitembeela leo Agosti 16, 2022 ili kuona maendeleo ya ukarabaki wa kiwanda hicho kinachomilikiwa kw aubia kati ya WCF na PSSSF. 

NA K-VIS BLOG/KHALFAN SAID, BUMBULI

          WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Ajira, Vijana na Watu Wenye Ulemavu), Mhe. Profesa Joyce Ndalichako ametembelea kiwanda cha Chai Mponde kilichoko Bumbuli, Wilaya ya Lushoto Mkoani Tanga na kuwahakikishia wakulima wa zao hilo kwamba kiwanda kimekamilika kwa asilimia 95%.

Mhe. Profesa Ndalichako ameyasema hayo Agosti 16, 2022, ikiwa ni siku sita tu baada ya Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Comrade Daniel Chongolo kutoa maelekezo, juu ya kiwanda hicho kwamba kitakapoanza uzalishaji wa majaribio Septemba mwaka huu, kiendelee kupokea na kuchakata Chai moja kwa moja.

Pofesa Ndalichako amesema “Kimsingi kiwanda kimekamilika kwa asilimia 95%, nimefanya ukaguzi kwenye eneo la kupokelea na kuchambua Chai, eneo la kuichakata (Processing), eneo la kuangalia viwango na ubora (Grading), eneo la Karakana, Tanuri la kufua joto(Boiler) na kote huko kumekamilika.” Alisema.

Baada ya kupokea maelekezo Waziri alisema wao kama Wizara alikaa na Katibu Mkuu pamoja na Watendaji Wakuu wa Mifuko ya Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) na Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) ambao ndio wawekezaji wakuu kwenye kiwanda hicho ili kuona namna bora ya kuanza utekelezaji mara moja.

“Kulikuwa na baadhi ya vifaa ikiwemo mabomba ya kutolea mvuke na nyavu za kukaushia chai ambavyo vilihitajika ili kukamilisha hatua za uzalishaji.” Alifafanua.

Alisema Kiwannda cha Chai Mponde kinakwenda kuwa kiwanda cha ksiasa na kitakuwa na uwezo wa kuchakata tani 5,800 na baadaye uzalishaji utafika tani elfu 16,000.

“Kwa siku wakulima watauza kilo elfu 52,000, naamini kwamba kiwanda kitaenda kuinyanyua Halmashauri yetu ya Bumbuli na kuboresha maisha ya wananchi.” Alisema.

Mhe. Profesa Ndalichako ambaye alifuatana na Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Mhe. Omary Mgumba, Mkuu wa Wilaya ya Lushoto Mhe. Kalist Lazaro, Mkurugenzi Mkuu wa WCF, Dkt. John Mduma mwakilishi wa Mkurugenzi Mkuu wa PSSSF, Bw. Marco Kapinga, Mwenyekiti wa Bodi ya Kiwanda hicho, Bw. Anselim Peter, Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Chai  na watendaji wengine wa kiwanda, alisema kiwanda hicho kitatengeneza ajira za moja kwa moja 79 na zingine 100 hadi 200 kulingana na msimu wa kilimo.

Niwahakikishie ndugu zangu wa Bumbuli, huu ni utekelezaji wa Ilani ya CCM, lakini pia ni utekelezaji wa nia njema ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan ya kuwainua wakulima.” Alisema Profesa Ndalichako.

Ameongeza kwa namna yoyote ile kiwanda hicho ni kipaumbele katika Wizara anayoisimamia na dhamira kubwa ni kuhakikisha ifikapo Septemba mwishoni kiwanda kianze kazi.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Tanga Mhe. Omary Mgumba aliwahimiza wakulima wa Chai kuanza uzalishaji wa Chai kwa wakati kwani kiwanda kinaanza kazi mapema kama ambavyo imeelekezwa.

“Sisi watu wa Tanga, watu wa Bumbuli na hasa Lushoto, uchumi wetu mkubwa unategemea Chai. Tangu kiwanda kilipofungwa mwaka 2013, uchumi umedumaa na ushahidi ni mapato ya Halmashauri ambayo si ya kuridhisha.” Alisema.

Aidha wakulima wa Chai wameonyesha matumaini makubwa kufuatia ziara ya Mhe. Waziri Profesa Ndalichako ambapo baadhi walifuatana nae kutembelea na kukagua maendeleo ya kiwanda hicho.

“Mimi sasa nina matumaini makubwa kwamba kiwanda hiki kitaanza kazi, nimeona mabadiliko makubwa yamefanyika, nimshukuru sana Mhe. Rais wetu, Mama Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa hii iliyofanyika.” Alisema Mkulima wa Chai Bumbuli Mzee Said Ngereza.

“Sisi kama wakulima tumejipanga kwenda shambani, pelekeni salamu kuwa serikali inatufungulia kiwanda nasi tuko tayari.” Alisema mkulima mwingine Bw. Shemdoe.


Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Ajira, Vijana na Watu Wenye Ulemavu), Mhe. Profesa Joyce Ndalichako (Wapili kushoto), akizungumza jambo wakati alipotembelea na kukagua kiwanda cha Chai Mponde Agosti 16, 2022. Wakwanza kulia ni Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Mhe. Omary Mgumba na katikati ya Mhe. Waziri na Mhe. Mkuu wa Mkoa ni Mkurugenzi Mkuu wa WCF, Dkt. John Mduma.No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.