Habari za Punde

MAAFISA UGANI WATAKIWA KUWA KARIBU NA WAFUGAJI

Afisa Mifugo Mkuu, Idara ya Uendelezaji wa Maeneo ya Malisho na Rasilimali za Vyakula vya Mifugo, Bw. Israel Kilonzo (kushoto) akitoa elimu kwa wafugaji wa Kanda ya Kaskazini kuhusu umuhimu wa kustawisha malisho ya mifugo alipokutana na wafugaji hao waliotembelea Banda la Wizara ya Mifugo na Uvuvi lililopo kwenye maonesho ya Wakulima NaneNane Kanda ya Kaskazini yanayoendelea Mkoani Arusha Agosti 4, 2022.

Na Mbaraka Kambona, Arusha

Wafugaji wanaofanya shughuli zao Kanda ya Kaskazini wameiomba Serikali kuhakikisha Maafisa Ugani wanawafikia Wafugaji kwa urahisi ili kuwapatia huduma stahiki wakati wote ili ufugaji wao uwe bora na wenye tija.

Wakiongea kwa nyakati tofauti katika Maonesho ya Wakulima NaneNane Kanda ya Kaskazini yanayofanyika Mkoani Arusha Agosti 4, 2022, Wafugaji hao walisema ni muhimu maafisa ugani kuwatembelea wafugaji kila wakati na kutatua changamoto zinazowakabili kwani kufanya hivyo kutasaidia kuboresha ufugaji wao na manufaa ya kazi hiyo yataonekana.

Mfugaji kutoka Arusha, Bw. Desderi Kimario alisema kuwa wanahitaji maafisa ugani wa kilimo na mifugo wote kwa pamoja wawe wanafanya kazi karibu na wafugaji ili wafugaji hao waweze kufanya shughuli zao kwa kuzingatia ushauri wa Wataalamu hao na kufanya ufugaji wao uwe na tija kubwa kwao  na nchi kwa ujumla.

"Tunaomba maafisa ugani wawe wanatutembelea mara kwa mara sisi wafugaji wadogowadogo katika maeneo yetu huku kwenye Kata na Vijijini ili kujua matatizo yetu na sio mpaka tufike kwenye maonesho kama hivi, kwa sababu maonesho huwa ni mara moja kwa kila mwaka", alisema Kimario

Bw. Lawrence Kimambi, Mfugaji kutoka Mkoa wa Kilimanjaro alisema  kwa sasa ardhi imekuwa finyu hivyo ni muhimu wafugaji wakaendelea kupatiwa elimu ya kulima malisho ya mifugo ili kuokoa changamoto ya malisho na kuleta manufaa zaidi kwa jamii za wafugaji na nchi kwa ujumla.

Naye Kevin Manase kutoka Arusha alisema kuwa kama wafugaji wataendelea kuelimishwa vizuri kuhusu umuhimu wa ulimaji wa malisho ya mifugo basi sio muda mrefu migogoro kati ya wakulima na wafugaji itakwisha.

Kwa Upande wake, Afisa Mifugo Mkuu kutoka Wizara ya Mifugo, Bw. Israel Kilonzo aliwashauri wafugaji hao kuanza kujifunza namna ya  kustawisha malisho ya mifugo na kuachana na tabia ya kutegemea malisho ya asili peke yake  kwani kufanya hivyo kutasaidia kupunguza migogoro ya ardhi.

"Kama tunavyojua watu wanaongezeka na mifugo pia inaongezeka na ardhi iliyopo haitoshi kufanya ufugaji wa kuhamahama, ni lazima tujifunze kustawisha malisho  katika maeneo yetu na tujifunze kuyatumia vizuri ikiwemo kuwa na mifugo tutakayoimudu kuihudumia", alisema Kilonzo

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.