Habari za Punde

Mafunzo ya utengenezaji wa Video za Utalii na Utamaduni wa Zanzibar yafanyika Karume

Mratibu wa Program ya Wafanyakazi wa kujitolea KOICA Pauline Mushi akizungumza katika Ufunguzi wa Program ya Mafunzo ya utengenezaji wa Video za Utalii na Utamaduni wa Zanzibar, katika Ukumbi wa Mkutano wa Dkt. Idrissa Muslim Hijja Mbweni Zanzibar.
Mkurugenzi wa Taasisi ya Karume ya Sayansi na Teknolojia (KIST), Dkt. Mahmoud Abdulwahab, akikabidhiwa Vifaa vitakavyotumika katika Program ya Mafunzo ya utengenezaji wa Video za Utalii na Utamaduni wa Zanzibar na Mratibu wa Program ya Wafanyakazi wa kujitolea KOICA Pauline Mushi, katika Ukumbi wa Mkutano wa Dkt. Idrissa Muslim Hijja Mbweni Zanzibar.
Mkurugenzi wa Taasisi ya Karume ya Sayansi na Teknolojia (KIST), Dkt. Mahmoud Abdulwahab, akifunguwa Program ya Mafunzo ya utengenezaji wa Video za Utalii na Utamaduni wa Zanzibar, katika Ukumbi wa Mkutano wa Dkt. Idrissa Muslim Hijja Mbweni Zanzibar.

Mkurugenzi wa Taasisi ya Karume ya Sayansi na Teknolojia (KIST), Dkt. Mahmoud Abdulwahab, akiwa katika Picha ya pamoja na Washiriki mbalimbali waliyohudhuria katika Ufunguzi wa Program ya Mafunzo ya utengenezaji wa Video za Utalii na Utamaduni wa Zanzibar.

IMETOLEWA NA KITENGO CHA HABARI NA MAWASILIANO (KIST).

Taasisi ya Karume ya Sayansi na Teknolojia Zanzibar (KIST) imelipongeza Shirika la Maendeleo la Korea (KOICA), kwa kuendelea kushirikiana na Tasisi ya Karume katika kutoa mafunzo yatakayowawezesha Vijana kujitengenezea fursa za ajira  Nchini.

Pongezi hizo zimetolewa na Mkurugenzi wa Taasisi ya Karume ya Sayansi na Teknolojia (KIST), Dkt. Mahmoud Abdulwahab, wakati akifungua rasmi program ya Mafunzo ya utengenezaji wa Video za Utalii na Utamaduni wa Zanzibar, katika Ukumbi wa Mkutano wa Dkt.Idrissa Muslim Hijja Mbweni Mjini Zanzibar.

Alisema uamuzi uliochukuliwa na Shirika la Maendeleo la Korea la kutoa Mafunzo ya utengenezaji wa Video kwa  Vijana, ni uamuzi sahihi ambao utawawezesha Vijana kuajiriwa na kujiajiri wenyewe pindi watakapomaliza Mafunzo hayo.

Akielezea umuhimu wa Mafunzo hayo katika Sekta ya Utalii, alisema bado Serikali  ya Zanzibar inaendelea kuupa kipaumbele Utalii kutokana na faida kubwa inayopatikanwa katika Sekta hiyo, hivyo  utengenezwaji wa Video za Utalii na Utamaduni wa Zanzibar zitasaidia katika kuutangaza Utalii katika Mataifa mbalimbali Duniani ikiwemo Korea.

Aidha alitumia fursa hiyo kuwaagiza Viongozi wanaosimamia zoezi hilo katika Taasisi ya Karume kuhakikisha lengo la Mafunzo hayo linafikiwa kwa asilimia mia, na kuhakikisha mafunzo hayo yanakuwa endelevu katika Taasisi ya Karume, na yanakwenda sambamba na uanzishwaji wa kozi mpya ya Digital Design and Development.

“Mafunzo haya yana umuhimu mkubwa kwa Zanzibar na kwa Taasisi yetu, wenzetu kutoka Korea wametumia fedha nyingi katika Mafunzo haya ni lazima yawe endelevu katika Taasisi yetu” alisema Mkurugenzi.

Katika hatua nyingine Dkt. Mahmoud aliwaasa Wanafunzi watakaoshiriki katika Mafunzo hayo kuitumia vyema  fursa hiyo kwani ni fursa muhimu na ni adimu kuipata.

Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi wa KOICA, Mratibu wa Program ya Wafanyakazi wa kujitolea KOICA Pauline Mushi amesema KOICA imeamua kuanzisha mashindano hayo ili  kuona Utamaduni  na Utalii wa Zanzibar unatangazwa kwa njia mbalimbali ikiwemo Video za Mitandaoni, hivyo Shirika hilo limeamuwa kushirikiana na Taasisi ya Karume katika kuandaa mashindano hayo.

Alisema Shirika la Maendeleo la Korea limetumia takriban dola 10,000 za Kimarekani kwa ajili ya kununua vifaa na kualika Wataalamu wa kuwafundisha Wanafunzi ujuzi wa uchukuaji picha na video.

“Ni matumaini yetu kuwa sisi KOICA kupitia programu na mashindano haya Vijana wataweza kupata ujuzi ambao utakuwa chachu ya maendeleo kwenye Sekta ya Utalii na Utamaduni.” Alisema Mratibu huyo.

Aidha alitumia fursa hiyo kuupongeza Uongozi wa Taasisi ya Karume  kwa ushirikiano mkubwa waliouonesha katika kufanikisha mashindano hayo, na kuendelea na kazi ya kutoa elimu na kujenga uwezo kwa Vijana Nchini.


 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.