Habari za Punde

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Dkt.Philip Mpango Akabidhi Gari kwa TANAPA

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa  Dkt. Philip Mpango akimkabidhi mfano wa funguo ya gari Waziri wa Maliasili mna Utalii Balozi Dkt. Pindi Chana kuashiria kukabidhi rasmi Malori maalum yatakayotumika na TANAPA katika kuboresha Miundombinu ya Utalii yaliotolewa na Mradi wa Kuboresha Usimamizi wa Maliasili na Utalii Kusini mwa Tanzania (REGROW) katika hafla iliofanyika katika viwanja vya Hifadhi ya Taifa ya Mikumi mkoani Morogoro leo tarehe 17 Agosti 2022.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango leo tarehe 17 Agosti 2022 amezindua na kukabidhi Malori maalum 44 yenye thamani ya Shillingi billioni 14.77 kwa Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA) yalionunuliwa kupitia Mradi wa Kuboresha Usimamizi wa Maliasili na Kukuza Utalii Kusini mwa Tanzania (REGROW). Hafla hiyo imefanyika katika viwanja vya Hifadhi ya Taifa ya Mikumi mkoani Morogoro.

Akihutubia Viongozi, Maafisa, Askari na wananchi mbalimbali waliojitokeza katika hafla hiyo, Makamu wa Rais amesema serikali imedhamiria kuimarisha miundombinu ya vivutio vya utalii vilivyopo Ukanda wa Kusini hususan ujenzi wa barabara na viwanja vya ndege ndani ya Hifadhi pamoja na kutangaza ipasavyo eneo hilo ili kuendeleza utalii katika Ukanda huo.

Ameongeza kwamba mradi huo ukitekelezwa ipasavyo utasaidia kuongeza fursa kwa mwananchi, kwani unalenga kutoa ajira zaidi ya 40,000 kwa wakulima na wananchi wanaoishi jirani na hifadhi za ukanda wa Kusini,kuhamasisha kilimo cha kisasa na kuchochea sekta nyingine ambazo zinachangia ukuaji wa uchumi.

Makamu wa Rais ameitaka Wizara ya Maliasili na Utalii na wadau wote wa utalii kwa ujumla, kuwa wabunifu katika kutangaza vivutio vilivyopo nchini Tanzania. Amewasihi kuhakikisha wanaongeza maeneo ya kitalii ambayo yana ladha mbalimbali za kitalii na kuvitangaza. Amewaasa watoa huduma wa sekta binafsi kutumia fursa ya uwepo wa idadi kubwa ya watalii nchini kuwekeza katika kujenga hoteli katika hifadhi.

Aidha Makamu wa Rais ameagiza Wizara ya Ardhi, Wizara ya Maliasili na Utalii pamoja na TAMISEMI kwa kushirikiana na wadau wengine kuhakikisha maeneo yanayopimwa kwa ajili ya mashamba, miradi au makazi yasiwe njia za wanyama pori. Amesema kumekuepo ongezeko la malalamiko kuhusu watu kupewa mashamba na viwanja kwenye mapito ya wanyama na hivyo kusababisha migogoro ya ardhi na hasara kubwa.

Pia amewaagiza Wakuu wa Mikoa ,TANAPA na TAWIRI kuchukua hatua kali za kisheria dhidi ya yeyote atakaebainika kuingiza mifugo katika maeneo ya hifadhi na mapori tengefu.

Kwa upande wake Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana amesema mradi wa REGROW unatekelezwa katika vijiji 61 ambavyo vipo Jirani na hifadhi za kipaumbele  ikiwa lengo kuu ni kuwapa faida ya uhifadhi wa maliasili muhimu kwa nchi hasa katika kuchangia katika uchumi wa nchi kwa ujumla na mtu mmoja mmoja

Amesema Miongoni mwa faida watakazopata wakazi hao ni pamoja na ajira zitakazotokana na miradi watakayopendekeza wao wenyewe na pia mradi utatoa ufadhili wa masomo kwa vijana kutoka vijiji hivyo kuanzia vyuo vya ngazi ya kati kama VETA, Chuo cha Utalii (NCT), Chuo cha Ufugaji Nyuki (BTI) na Chuo cha Mafunzo ya Wanyamapori Pasiansi (PWTI) na Vyuo vya Elimu ya Juu kama vile Chuo Kikuu cha Sokoine pamoja na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Awali akitoa taarifa ya mkoa, Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Fatma Mwasa ameiomba serikali kurudisha mpango wa ujenzi wa barabara iliolenga kupita nje ya hifadhi ili kusaidia kupunguza vifo vya wanyama vitokanavyo na ajali, kupunguza takataka zinazotokana na watumiaji wa barabara hiyo pamoja na uwepo wa geti la udhibiti litakalotumika kudhibiti wanaoendesha mwendokasi hifadhini.

Amesema mkoa unaendelea na juhudi za kutangaza utalii ikiwa pamoja na kuwaomba wadau wa utalii kuwekeza katika miundombinu ya malazi ili kuboresha sekta hiyo. 

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa  Dkt. Philip Mpango akikata utepe kuashiria kuzindua Malori maalum yatakayotumika na TANAPA katika kuboresha Miundombinu ya Utalii yaliotolewa na Mradi wa Kuboresha Usimamizi wa Maliasili na Utalii Kusini mwa Tanzania (REGROW) katika hafla iliofanyika katika viwanja vya Hifadhi ya Taifa ya Mikumi mkoani Morogoro leo

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa  Dkt. Philip Mpango akihutubia Viongozi, ,Maafisa , Askari na Wananchi mbalimbali  katika viwanja vya Hifadhi ya Taifa ya Mikumi mkoani Morogoro  wakati wa Hafla ya kukabidhi Malori maalum kwa TANAPA yatakayotumika katika kuboresha Miundombinu ya Utalii yaliotolewa na Mradi wa Kuboresha Usimamizi wa Maliasili na Utalii Kusini mwa Tanzania (REGROW). tarehe 17 Agosti 2022

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa  Dkt. Philip Mpango akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya wakuu wa uhifadhi na mwenyeviti wa bodi kutoka TANAPA, TAWA na Mamlaka ya Uhifadhi Ngorongoro. Kushoto ni  Waziri wa Maliasili na Utalii Balozi Dkt. Pindi Chana, na Katibu Mkuu wa Wizara  hiyo Prof. Ealiaman Sedoyeka na kulia ni Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Fatma Mwasa na Mwenyekiti wa CCM wa Mkoa huo Doroth Mwamsiku.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa  Dkt. Philip Mpango akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya wakazi wa wilaya ya Kilosa eneo la Mikumi waliojitokeza katika Hafla ya kukabidhi Malori maalum kwa TANAPA yatakayotumika katika kuboresha Miundombinu ya Utalii yaliotolewa na Mradi wa Kuboresha Usimamizi wa Maliasili na Utalii Kusini mwa Tanzania (REGROW). tarehe 17 Agosti 2022.

 

 


No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.