Habari za Punde

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi Amekutana na Kuzungumza na Mnadhimu Mkuu wa JWTZ.

 

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Hussein Ali Mwinyi (kulia) alipokuwa akizungumza na Mnadhimu  Mkuu wa  JWTZ (Chief of Stuff) Luteni Generali  Salum Haji Othman,alipofika Ikulu Jijini Zanzibar kujitambulisha leo akiwa na ujumbe aliofuatana nao .[Picha na Ikulu] 01/08/2022. 

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi amelipongeza Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), kwa kuendelea kusimamia ulinzi na usalama hapa nchini.

Rais Dk. Mwinyi aliyasema hayo leo Ikulu Zanzibar wakati alipofanya mazungumzo na Mnadhimu Mkuu wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Luteni Jenerali Salum Haji Othman, aliyefika Ikulu kwa ajili ya kujitambulisha.

Aidha, Rais Dk. Mwinyi alimueleza Mnadhimu Mkuu huyo wa (JWTZ), kwamba hali ya amani, ulinzi na usalama hapa Zanzibar imezidi kuimarika kutokana na kuwepo kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa.

Katika mazungumzo hayo, Rais Dk. Mwinyi alisema kuwa hatua za (JWTZ) ya kuendelea kusimamia ulinzi na usalama wa nchi imepelekea kupatikana kwa mafanikio makubwa.

Hivyo, Rais Dk. Mwinyi amemuhakikishia Mnadhimu Mkuu huyo wa (JWTZ), kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kushirikiana na Jeshi hilo ili mafanikio zaidi yaendelee kupatikana.

Pamoja na hayo, Rais Dk. Mwinyi alimpongeza Luteni Jenerali Othman kwa kuteuliwa kushika wadhifa huo na kumuahidi kwamba ataendelea kushirikiana nae ili aendelee kufanya kazi zake katika kulitumikia Jeshi hilo kwa ufanisi zaidi.

Pamoja na hayo, Rais Dk. Mwinyi alieleza haja ya kuendeleza ushirikiano na Chuo cha Ulinzi cha Taifa (NDC) na kusema kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendeleza ushirikiano na Chuo hicho ambacho kila mwaka wahitimu wake wamekuwa wakifika Zanzibar ikiwa ni sehemu yao ya masomo.

Mapema Mnadhimu Mkuu wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Luteni Jenerali Salum Haji Othman alimueleza Rais Dk. Mwinyi kwamba uteuzi wake katika nafasi hiyo ulifanyika tarehe 30 Juni 2022 baada ya aliyekuwa Mnadhimu Mkuu Luteni Jenerali Mathew Mkingule kupangiwa majukumu ya Ubalozi nchini Zambia.

Hivyo, alimueleza Rais Dk. Mwinyi kwamba kufuatia kuteuliwa kwake ameona ni vyema aje kumsalimia pamoja na kujitambulisha kwake na kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Mnadhimu Mkuu huyo alieleza jinsi anavyotambua mchango mkubwa wa Rais Dk. Mwinyi pamoja na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa (JWTZ).

“Mheshimiwa Rais umekuwa karibu sana na Jeshi letu, kwa ushauri na kwa nasaha zako zilizojaa hekima na busara nyingi ulizojaaliwa na Mwenyezi Mungu, JWTZ siyo Taasisi ngeni kwani kupitia Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa umeliongoza Jeshi hili kwa miaka kumi katika mazingira haya sidhani kama kuna jambo jipya nitakaloweza kukueleza ukawa hulifahamu kuhusu JWTZ na sekta nzima ya ulinzi kwa ujumla wake”, alisema Mnadhimu Mkuu huyo wa JWTZ.

Aidha, Luteni Jenerali Othman alieleza jinsi Rais Dk. Mwinyi kwa kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar anavyosaidia kwa kiasi kikubwa katika kuleta utangamano kati ya wananchi na Jeshi lao kuhusu masuala mbali mbali ikiwemo migogoro ya ardhi na kusaidia kupata ufumbuzi wa kudumu.

Luteni Jenerali Othman alitumia fursa hiyo kumpongeza Rais Dk. Mwinyi kwa kuendeleza ukaribu wake na Chuo cha Ulinzi cha Taifa (NDC), ikiwa ni pamoja na kuwakaribisha washiriki wa kozi hiyo kuja Zanzibar pamoja na kuwafanyia mhadhara hapo Ikulu.

Katika maelezo yake Mnadhimu Mkuu huyo alieleza kwamba tayari ameshanza shughuli zake za kazi na kwa mara ya kwanza ameanza kisiwani Pemba kwa kukutana na kufanya mazungumzo na viongozi pamoja na maafisa wa Jeshi hilo.

Imetayarishwa na Idara ya Mawasiliano,

Ikulu Zanzibar.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.