Habari za Punde

Vijana Kuendelea Kuyatumia Mabaraza ya Vijana Kama Chemchem ya Fikra Mpya na Jukwaa Kupaza Sauti Zao.

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akihutubia katika Maadhimisho ya Kilele cha Siku ya Vijana Kimataifa, maadhimisho hayo yaliyofanyika katika ukumbi wa Sheikh.Idrisa Abdulwakil Kikwajuni Unguja Jijini Zanzibar leo 12-8-2022
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi  Dk. Hussein Ali Mwinyi amewataka Vijana kuendelea kuyatumia Mabaraza ya Vijana kama Chemchem ya fikra mpya na jukwaa la kupaza sauti zao katika masuala muhimu kwa maendeleo ya taifa.

Dk. Mwinyi ametoa wito huo katika kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani, hafla iliofanyika katika Ukumbi wa Sheikh Idrissa Abdul-wakil Kikwajuni, Jijini Zanzibar.

Amesema Serikali imeelekeza juhudi kubwa katika kuimarisha ushiriki wa Vijana katika shughuli za Ujenzi wa Taifa kupitia Baraza la Vijana Zanzibar, kwa kigezo kuwa ndio sehemu maalum itakayowawezesha kukutana na kujadili masuala mbali mbali yatakayosaidia nchi kiuchumi, kijamii na kisiasa.

Akinukuu hotuba za Rais wa Kwanza wa Zanzibar na mwasisi wa Mapinduzi Marehemu mzee Abeid Amani Karume, Dk. Mwinyi alihimiza

Umuhimu wa Vijana kujiamini, kuacha ubinafsi, kuwa  wabunifu na kuwa Wazalendo ili kutimiza malengo ya Mapinduzi ya 1964.

Alisema ni muhimu kuweka mazingatio ya mambo hayo kwa kuzingatia umuhimu wake katika kujenga mshikamano wa kweli kati yao na wananchi wote wa Zanzibar.

“Tuhakikishe mipango na matendo yetu yanazingatia maslahi mapana ya Taifa letu”, alisema.

Akigusia Ujumbe wa maadhimisho hayo usemao ‘Mshikamano baina ya Vizazi ili kujenga dunia ya rika zote’ Dk. Mwinyi alisema ujumbe huo ni muhimu kwani unahimiza umoja na mshikamano baina ya watu wa rika zote kwa miisngi ile ile iliohimizwa na waasisi wa Taifa pamoja na miongozo ya Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984.

Dk. Mwinyi alisema Serikali imeongeza juhudi katika kuwawezesha Vijana kiuchumi kwa kuwapatia mitaji, elimu ya Ujasiriamali pamoja na kuongeza fursa za masoko na kuhimiza dhana ya kuwaelimisha wajasiriamali  umuhimu wa  kuelekeza nguvu katika kutafuta masoko na kuzalisha bidhaa bora zinazohitajika katika sekta ya Utalii.

Alisema serikali imetenga kiwango kikubwa cha Fedha kupitia Mkopo wa Ahueni ya Uviko -19 kwa ajili ya kuwaendeleza wajasiriamali wanaojishughulisha na sekta za kilimo cha mwani, uvuvi, utalii, utengenezaji wa bidhaa mbali mbali pamoja na wasanii wa kazi za mikono.

Alisema dhamira ya Serikali ni kuhakikisha inatengeneza mazingira yatakayovutia zaidi vijana kupenda kujiajiri kwa kutambua maendeleo ya sekta binafsi ndio msingi mkuu wa ajira katika Taifa lolote lile.

Alisema serikali inaendelea kupanga na kutekeleza miradi mikubwa katika ujenzi wa miundo mbinu, kuendeleza uchumi wa Buluu, kuimarisha utalii, uwekezaji na biashara ili kutanua wigo wa upatikanaji wa fursa kwa vijana na kukuza uchumi wa Taifa.

Aliwataka vijana hao kuendeleza mafanikio makubwa yaliofikiwa  na kusema Serikali inathamini sana juhudi hizo, hususan katika kuendeleza na kukuza sanaa, utamaduni na michezo.

Dk. Mwinyi alitumia fursa hiyo kuipongeza Timu ya Riverside ya Jang’ombe kwa kutwaa Ubingwa wa Ligi ya Vijana pamoja na kuzipongeza Timu za KMKM kwa kutwaa Ubingwa wa Ligi Kuu ya Zanzibar pamoja na Timu ya Jeshi ya Kipanga  kwa kubeba Taji la FA Cup.

Aidha, alizipongeza na kuzitakia  mafanikio mema timu za Jamhuri na Chipukizi kutoka Pemba kwa kupanda Daraja na kuingia Ligi Kuu ya Zanzibar  pamoja na Timu za Kundemba ya Mjini Unguja na Dulla Boys ya Jambiani kwa upande wa Zanzibar.

Katika hatua nyengine, aliwataka vijana kuwa wabunifu, wajasiri na walio na utayari katika kufanya mambo mapya.

Aliwataka kuhakikisha wanatekeleza vyema jukumu la kulinda na kuendeleza amani pamoja na kuimarisha umoja na mshikamano miongoni mwa makundi yote ndani ya jamii.

Katika hafla hiyo Dk. Mwinyi alipata fursa ya kukabidhi Mfano wa Hundi ya Shilingi Milioni 15 kutoka Shirika linaloshughulikia changamoto za Vijana (IRI) kwa ajili ya Vijana tisa  pamoja na mfano wa Hundi ya shilingi Milioni 50 kutoka Youth Challenge International Tanzania kw aajili ya vijana 18 baada  ya kupata mafunzo.

Mapema, Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Tabia Maulid Mwita alisema Wizara hiyo inaendelea kuwajengea mazingira bora vijana kisera na miundombinu wezeshi pamoja na mambo mbali mbali ili kukuza ushiriki na ushirikishwaji.

Alisema Wizara hiyo ina mipango ya kujenga vituo vya Mafunzo  kwa  Vijana katika maeneo ya Bweleo Mkoa Mjini Magharibi  na Weni Kisiwani Pemba katika nyanja za ushoni, ujasiriamali, stadi za maisha ikiwa ni hatua ya kusaidia utoaji nasaha na kuwawezesha kumudu maisha.

Aidha, alisema Wizara ina azma ya kujenga Vituo vya ufugaji kupitia fedha za Ahueni ya mfuko wa Uviko 19 katika maeneo ya Pangeni Unguja pamoja na Ole kisiiwani Pemba.  

Nae, Mwenyekiti wa Baraza la Vijana Zanzibar Yunus Juma Ali alimhakikishia Rais Dk. Mwinyi kuwa Baraza hilo litaendelea na kazi za kuwahamasisha wananchi katika Mikoa yote ya Unguja kushiriki kikamilifu katika zoezi la sensa linalotarajiwa kufanyika Agosti 23, mwaka huu.

Alitumia fursa hiyo  kumpongeza Dk. Mwinyi kwa kuimarisha uchumi wa Zanzibar pamoja na Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mama Samia Suliuhu Hassan kwa kazi kubwa ya kuiongoza Tanzania.

Aidha, aliwasilisha ombi la Baraza hilo kwa Rais Dk. Mwinyi la kumuomba kushirki  katika maadhimisho ya siku ya Vijana Duniani, kila mwaka katika kipindi chote cha uongozi wake.

Maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani hufanyika kila ifikapo Agosti 12 ya kila mwaka, ikiwa ni hatua ya kufanya tathmin ya mafanikio ya vijana katika juhudi zao za ujenzi wa Taifa pamoja na kuzitafutia ufumbuzi changamoto mbali mbali zinazowakabili.

Imetayarishwa na Idaya ya Mawasiliano

Ikulu Zanzibar.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.