Habari za Punde

Waziri Dkt.Khalid Awataka Wajumbe wa Kamati ya Kuratibu Masahihisho ya Changamoto za Hoja za Ukaguzi Kuwajibika Katika Jukumu Walilokabidhiwa

 
Wajumbe wa Kamati ya kitaifa kuratibu ya utekelezaji wa mpango wa kurekebisha hoja za ukaguzi wa Shirika la kimataifa la bahari Duniani (IMO) wametakiwa kuwajibika vyema katika jukumu walilokabidhiwa ili kufanikisha lengo lililokusudiwa.

Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi Dk. Khalid Salum Mohamed ametoa agizo hilo wakati akizungumza na wajumbe hao kupitia kikao cha mashauriano kilichofanyika katika ukumbi wa Wizara hiyo Kisauni.

Mhe. Waziri amesema Wizara kwa kutambua umuhimu wa hitajio la kuimarisha sekta ya usafiri baharini imeamua kuunda kamati hiyo ambayo imeshirikisha mjumbe mmoja kutoka kila taasisi husika.

Amefafanua kuwa, suala la utekelezaji wa mpango kazi wa masahihisho ni miongoni mwa juhudi zinazochukuliwa na Serikali zote mbili katika kutimiza wajibu na majukumu ya Nchi kwa Jumuiya za kimataifa katika kutatua changamoto hizo.

“Kuundwa kwa kamati hii, pamoja na mambo mengine kumelenga kusaidia utekelezaji wa mpango kazi wa masahihisho kwa lengo la kuimarisha usalama wa baharini na ulinzi wa mazingira ya bahari ya nchi yetu na ulimwenguni kwa ujumla” Alisema Dk. Khalid

Waziri Dk. Khalid ameeleza kwamba Uongozi wa Wizara una imani kubwa na watendaji waliochaguliwa katika kamati hiyo kutokana na weledi na ujuzi hivyo wataifanikisha kazi hiyo kwa moyo wa kizalendo.

Aidha, Dk. Khalid amesema hoja hizo zimegawanyika  katika makundi sita (6) ikijumuisha sharia na kanuni, mafunzo na utalaamu, mifumo na miongozo ya kazi, vifaa na vitendea kazi, sera, mipango na mikakati pamoja na tathmini na ufutiliaji wa utendaji.

Mhe. Waziri amewataka wajumbe wa kamati hiyo  kuhakikisha ifikapo mwezi Disemba mwaka huu wawe wamekamilisha ripoti maalum itakayo kuwa na mpango kazi pamoja na  bajeti ya utekelezaji wake. 

Nae, Mkurugenzi wa Mamlaka ya Usafiri baharini Ndugu Sheikha Ahmed Mohamed amesema kupitia kamati hiyo ya watalamu ilioundwa mamlaka inakusudia kurekebisha changamoto zote zilizojitokeza ili muda ukifika kwa ajili ya ukaguzi zoezi likamilike kwa ufanisi.

Imetolewa na Kitengo cha Habari (WUMU)

Agosti 22, 2022.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.