Habari za Punde

MASHUJAA WA SARATANI ( JEMA FOUNDATION) KUTEMBELEA WAGONJWA WA SAATANI

Na Khadija Khamis -Maelezo. 10/ 09 /2022.

Imeelezwa kuwa Ugonjwa wa Saratani unapona iwapo ukigundulika mapema na kufanyiwa matibabu  ya haraka, hivyo ni vyema jamii iweke utamaduni wa kupima afya mara kwa mara ili kuchunguza  afya zao .

 

Akiyasema hayo  Mkurugenzi Mkuu wa Hospitali kuu ya Rufaa Mnazimmoja Dk. Marijani Msafiri Marijani alipowapokea Mashujaa wa Saratani kutoka Jema Fondation Tanzania bara kwa kuja  kuwatembelea wenzao wanaoishi na maradhi ya saratani na kuwafariji wagonjwa hao waliokuwepo katika hospitali ya rufaa mnazimmoja.

Alisema saratani ni ugonjwa sugu kwani wagonjwa wanakuwa katika maumivu makali na jambo kubwa wanalohitaji ni kupata ushirikiano kama huo kwa kuwapa moyo katika kupambana na maradhi hayo.

“Wanapowaona wenzao nao wamepitia katika mitihani kama hiyo na wameishinda hivyo huwapa matumaini ya kupambana,” alisema Dk.Marijani.  

Aidha alibainisha kuwa kwa Zanzibar saratani zinazoongoza ni saratani ya matiti, saratani ya tenzi dume na saratani ya shingo ya kizazi.

Alieleza kwamba mwaka 2021 wagonjwa wa saratani ya matiti walikuwa 57, saratani ya tenzi dume wagonjwa 40 na wagonjwa 28 wa saratani ya shingo ya kizazi.

Nao Mashujaa wa Saratani kutoka Jema Fondation Tanzania bara wamewaasa wagonjwa wenye ugonjwa huo kuhakikisha wanafuata maelekezo ya madaktari katika matibabu ili waweze kupona kabisa.

Walisema ni jambo la msingi kwa wagonjwa hao kutovunjika moyo na kutoogopa kwani watu wengi wana dhana potofu kuwa mtu ukishapata ugonjwa huo basi huwezi kupona tena .

kwa upande wa Mkuu wa Taasisi hiyo Jema Mahmoud Baruan ambae ni muathirika wa saratani ya mitoki alisema aligundulika na ugonjwa huo mwaka 2017 na kufanya tiba ambapo alipona mwaka 2018.

“Nilikuwa napitia madhila mbalimbali lakini sikukata tamaa niliendelea na tiba na nimepona hivyo na wenzetu waliokuwepo hapa waamini nao watapona,” alisema.

.Aidha alisema pamoja na kupitia chamgamoto mbali mbali za kipindi kigumu cha tiba ni kuihakikishia jamii kwamba saratani inatibika na inapona kabisa.

Alifahamisha kwamba satani ipo katika kundi la magonjwa ambayo sio ya kuambukiza hivyo ni vyema kwa wananchi kubadilisha maisha yao kwa kufanya mazoezi, kupunguza uzito, kuacha kunywa pombe kupindukia, kula vyakula vya mbogamboga na matunda na kuacha kuvuta sigara .

Mapema Muuguzi wa wodi ya Saratani hospitali ya Rufaa Mnazimmoja Ghania Amour Saleh aliipongeza taasisi hiyo kwa msaada na kujitolea kwao kwa wagonjwa waliolazwa katika hospitali hiyo.

Alisema bado katika jamii yetu kumekuwa na hofu ya kupima afya zao hivyo alitoa wito kwa jamii kujitokeza kupima afya  kwani kufanya hiyo kutasaidia kujulikana kwa tatizo mapema na kupatiwa matibabu.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.