Habari za Punde

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi Amekutana na Kuzungumza na Kamati ya ya Sheria Mpya ya Makadhi

 

RAIS  wa Zanzibar  na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akizungumza na Ujumbe wa Kamati Sheria Mpya ya Makadhi Zanzibar , walipofika Ikulu Jijini Zanzibar kwa mazungumzo yaliyofanyika katika ukumbi wa Ikulu leo 12-9-2022 na (kulia kwa Rais) Jaji Mkuu wa Zanzibar Mhe. Khamis Ramadhan  Abdalla na Kadhi Mkuu wa Zanzibar Sheikh Hassan Othman Ngwali

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi amesema ana matumaini makubwa kuwa mabadiliko ya Sheria ya Makadhi yanayofanyika yataondoa utata pamoja na migongano ya kiutendaji katika mhimili wa Mahakama hapa nchini.

Dk. Mwinyi amesema hayo Ikulu Zanzibar, alipozungumza na Kamati ya Sheria mpya ya Makadhi na kupokea taarifa ya mwelekeo wa Rasimu hiyo inayoongozwa na Mwenyekiti  Wakili  Mwandamizi wa Serikali Saleh Mbaraka.

Amesema kutokana na  dhamira njema iliopo, ana imani kubwa kuwa sheria ijayo ya Makadhi itakuwa nzuri, yenye tija, isiyo na mivutano  na yenye mwelekeo wa kujenga.

Alisema pale rasimu hiyo itakapofikishwa katika ngazi ya Baraza la Mapinduzi, wajumbe wa Baraza hilo watapata fursa ya kuipitia, sambamba na Kamati ya sheria ya Baraza hilo kushauri juu ya vipengele vinavyofaa kuingizwa au kupunguzwa.

Dk. Mwinyi aliwashukuru wajumbe wa Kamati hiyo kwa dhamira ya kuja na sheria mpya ya Makadhi kutokana na mahitaji yaliopo, akibainisha  hatua  ya kuwashirikisha wadau itawezesha  kupata mchango wa maoni ya kutosha.

Nae, Jaji     Mkuu wa Zanzibar Khamis Ramadhan  Abdalla pamoja na mambo mengine alisema kuongoza mhimili wa Mahakama, ambamo ndani yake kuna Kadhi mkuu, kunahitajika busara kubwa.

Mapema, Mwenyekiti wa Kamati ya Sheria mpya ya Makadhi Wakili Mwandamizi Saleh Mbaraka, alisema lengo la sheria hiyo ni kuongeza wigo wa kutafuta haki ndani ya Mahakama za Kadhi pamoja na kuleta uharaka katika maamuzi ya kesi.

Alisema sheria hiyo inalenga kurejesha dhana ya kuwatambua masheikh wabobezi , pamoja na kuwa na utaratibu wa kuweka Hati  mbali mbali na  kuweza kutumika katika Mahakama  mbali mbali Duniani.

Aidha, alisema itatoa msukumo katika hati mbali mbali  (ikiwemo za ndoa) kuweza kukubalika katika mataifa mbali mbali.

Wakili Mbaraka alieleza kuwa kwa kipindi kirefu Serikali imekuwa ikipoteza fedha nyingi katika kuwasomesha Masheikh katika nchi mbali mbali Duniani ikiwemo Saud Arabia, kupitia fedha za Serikali au za wahisani, lakini matokeo yake pale masheikh hao wanaporerjea nchini huachwa bila kutumika.   

Alisema kupitia sheria hiyo Masheikh hao watatambuliwa ili waweze kutoa mchango wao na kubainisha hatua hiyo itatoa ajira kwao.

Imetayarishwa na Idara ya Mawasiliano

Ikulu Zanzibar.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.