Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), Mhe. George Simbachawene wakiteta jambo na Naibu Waziri wa Elimu, Mhe. Omary Juma Kipanga baada ya kuwasilisha kauli ya Serikali kuhusu Tozo, bungeni jijini Dodoma.
Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba akiteta jambo na Mbunge wa Viti Maalum, Mhe. Juliana Masuburi, muda mchache kabla ya kuwasilisha kauli ya Serikali kuhusu Tozo, bungeni jijini Dodoma.
Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba akipongezwa na Mbunge wa Mbinga Vijijini, Mhe. Benaya Kapinga baada ya kuwasilisha kauli ya Serikali kuhusu Tozo, bungeni jijini Dodoma
Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Hamad Hassan Chande akitetea jambo na Naibu Waziri wa Ujenzi, Mhe. Mhandisi Godfrey Kasekenya, bungeni jijini Dodoma.
KAULI YA SERIKALI KUHUSU TOZO IKITOLEWA NA MHESHIMIWA DKT. MWIGULU LAMECK NCHEMBA MADELU
(MB),
WAZIRI WA FEDHA
NA MIPANGO
______________________________
Mheshimiwa
Spika, itakumbukwa
kuwa, katika mwaka wa fedha 2021/22, Sheria
ya Malipo ya Taifa, Sura na. 437 (National Payment System Act, Cap. 437)
ilifanyiwa marekebisho kupitia Sheria ya Fedha ya mwaka 2021 na kuanzisha tozo ya miamala ya kutuma
na kutoa fedha kwa njia ya simu za mikononi yaani, Mobile Money Transaction
Levy. Sambamba na tozo hii, tulipandisha tozo kwenye mafuta kwa ajili ya
kutunisha mfuko wa TARURA na Mfuko wa Elimu ya juu. Lengo la kuanzisha tozo hizi ni kuunganisha nguvu na umoja wa
Watanzania wote katika kuiwezesha Serikali kuongeza kasi ya kutekeleza miradi
hasa ile iliyokosa fedha kutokana na ufinyu wa bajeti ili kuwakwamua wananchi
dhidi ya ukosefu wa huduma za jamii-msingi kwa kuzingatia kuwa sura ya bejeti
yetu karibu kila mahitaji ni mahitaji ya lazima.Mahitaji
ya lazima yanayolindwa kwa mfano SGR, TANROADS, Bwawa la Umeme, REA, TARURA, Maji,
Elimu, Mikopo ya Elimu ya Juu, Elimu bila Ada, Mishahara, Deni la Taifa, Afya ni
takribani 27.9 trilion na makusanyo ya ndani ni takribani 28.01trilioni.
Mheshimiwa
Spika, Serikali
haina malengo ya kutoza Wananchi wake kodi/tozo kwa ajili ya kuwapa mzigo tu, bali
inalenga kuwahusisha Watanzania wote kwa umoja wetu katika juhudi za kujikwamua
kimaendeleo. Kwa mfano, tulipofanya
uamuzi huu:
a)
Tulikuwa
na hali mbaya sana ya barabara za vijijini zilizokosa matengenezo kwa ufinyu wa
bajeti, kadhalika, tulikuwa na vijiji ambavyo havijawahi kuwa na barabara ya aina
yeyote tangu nchi hii ipate uhuru, akina mama wajawazito walikuwa wakibebwa kwa
vitanda kupelekwa hospitali na wengine kupoteza maisha njiani, watoto wa shule
wakibebwa na maji kwa vijito tu kukosekana kwa madaraja;
b)
Tulikuwa
na kilio kikubwa sana cha ukosefu wa vituo vya afya vya kisasa vijijini, wagonjwa
wote walikuwa wanalazimika kutegemea hospitali za wilaya tu, maeneno mengine
hata hospitali za wilaya hazikuwepo, sehemu nyingine wananchi walilazimika kwenda
hospitali za mikoa jirani. Tulikuwa tunapoteza maisha ya watanzania kutokana na
umbali wa kufuata huduma za afya;
c)
Tulikuwa
na kilio kikubwa cha uwepo wa maboma ya madarasa na nyumba za walimu
yaliyojengwa kwa nguvu za wananchi na yaliyokaa muda mrefu bila kukamilishwa ilhali kukiwa na uhitaji mkubwa wa madarasa kutokana
na ongezeko kubwa la watoto;
d)
Tulikuwa
na kilio kikubwa cha wanafunzi waliokosa mikopo ya elimu ya juu wapatao 26,000
wakijumuisha mwaka juzi na mwaka jana. Hawa ni watoto wa kitanzania hasa hasa
wanaotoka katika familia masikini ambao ndoto zao za kufika chuo kikuu zilikuwa
zinaishia hapo; na
e)
Tulikuwa
na kilio kikubwa cha maji hasa hasa vijijini, jambo hili lilikuwa linaathiri
sana shughuli za maendeleo kwa mfano kila mtoto abebe galoni ya maji na
kuibajeti kwa siku nzima, walimu kufuata maji maeneo ya mbali, vijana wanaotaka
kujenga kuingia gharama kubwa kwa kununua maji yanayopimwa kwa ndoo pamoja na
kukosekana kwa mahitaji ya maji katika maeneo muhimu kama Hosipitalini.
Mheshimiwa
Spika, makusanyo ya tozo ya miamala
yameiwezesha Serikali kutoa huduma za msingi za Wananchi wetu katika mwaka wa
fedha 2021/22. Mathalani, Serikali ilitumia jumla shilingi bilioni 7 zilitokana
na tozo ya miamala kwa ajili kujenga madarasa. Vilevile, Serikali ilitumia
jumla ya shilingi bilioni 143.7 kwa ajili ya ujenzi wa vituo vya afya ambapo
kati ya fedha hizo, shilingi bilioni 117 sawa na asilimia 81.4 ya fedha zote zilitokana
na tozo ya miamala. Kadhalika, Serikali ilitumia jumla ya shilingi bilioni
611.3 kwa ajili ya mikopo ya elimu ya juu na kati ya fedha hizo, shilingi
bilioni 221.3 zilitokana na tozo. Kwa upande wa TARURA, Serikali ilitumia jumla
ya shilingi bilioni 735.7 kwa ajili ya ujenzi wa barabara vijijini ambapo kati
ya kiasi hicho shilingi bilioni 13.5 zilitokana na tozo kwenye miamala na kiasi
kingine ni tozo kwenye mafuta.
Mheshimiwa
Spika, katika
mwaka wa fedha 2022/23, kulikuwa na mahitaji muhimu na ya lazima ambayo
yangekosa fedha kutokana na ufinyu wa bajeti. Baadhi ya masuala muhimu ambayo
yangeathiriwa kama tungefuta kabisa chanzo hiki ni:
a)
Tungeelekeza
fedha za mkopo wa ECF kwenye madarasa mwaka huu, tusingeweza kupeleka bilioni
954 kwenye kilimo zinazolenga kujenga miundombinu ya umwagiliaji, mbegu bora
pamoja na block farming. Serikali ilitumia busara ya kiuchumi kupeleka
fedha hizo kwenye sekta za uzalishaji ili kutengeneza ajira kwa vijana, na
fedha za kutoa huduma za jamii zitafutwe kutoka kwenye tozo;
b)
Tungeelekeza
fedha za mkopo wa ECF kwenye ujenzi wa VETA mwaka huu, tusingeweza kupeleka bilioni
145 kwenye mifugo, uvuvi na wamachinga zinazolenga kujenga na kununua boti za
uvuvi, kuchochea ukuaji wa sekta ya mifugo na kujenga miundombinu na mitaji kwa
wamachinga. Katika suala hili pia, Serikali ilitumia busara ya kiuchumi kupeleka
fedha hizo kwenye sekta za uzalishaji na
fedha za kutoa huduma za jamii zitafutwe kutoka kwenye tozo;
c)
Tungeelekeza
fedha za mkopo wa AfDB kwenye ujenzi wa madarasa na VETA mwaka huu, tusingeweza
kupeleka bilioni 150 kwenye ruzuku ya mbolea ili kuwasaidia wakulima wazalishe
chakula cha kutosha kwa ajili ya nchi yetu na kudhibiti mfumuko wa bei. Hapa
pia, Serikali ilitumia busara ya kiuchumi kupeleka fedha hizo kwenye sekta za
uzalishaji na fedha za kutoa huduma za
jamii zitafutwe kutoka kwenye tozo; na
d)
Tungeamua
kutotoa ruzuku ya shilingi bilioni 100 kwenye mafuta kila mwezi tungeweza kuelekeza
fedha hizo kujenga madarasa yote, VETA na mengineyo. Hata hivyo, tungeweza kuwa
na mfumuko wa bei ambao ungeleta athari kubwa kwenye uchumi ikiwemo kupanda kwa
gharama za maisha ambazo zisingehimilika hususan kwa wananchi wa kawaida.
Mheshimiwa
Spika, Hivyo,
Serikali ilitarajia kukusanya takriban shilingi bilioni 500 kutokana na tozo ya
miamala ya simu na benki na kuzielekeza katika;
a)
Ujenzi wa
madarasa 8,000 nchi nzima ambapo mahitaji ya madarasa bado yanakadiriwa kuwa
17,000;
b)
Kujenga
vyuo vya VETA 72 kwenye Wilaya
zisizo na vyuo vya ufundi nchini;
c)
Kutekeleza
mpango wa elimu bila ada kwa kidato cha tano na sita; na
d)
Kuendelea na ujenzi wa zahanati na vituo vya
afya na vifaa tiba katika maeneo ambayo bado hayana huduma hizo. Nawasihi
Watanzania wote kuunga mkono juhudi hizi njema za Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, mama yetu, Samia Suluhu Hassan.
Marekebisho
ya Sheria ya Fedha ya Mwaka 2022
Mheshimiwa
Spika, kama unavyofahamu,
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Sheria ya Fedha ya Mwaka
2021 ilifanya marekebisho kwenye Sheria ya Malipo ya Taifa, Sura ya 437 (The
National Payment System Act, Cap 437) kwa kuanzisha tozo ya miamala ya kutuma
na kutoa fedha ambapo Kanuni ya Sheria husika (The National Payment System (Electronic
Money Transaction Levy Regulations 2021)) ilianzishwa na kuainisha tozo kwenye miamala ya kielektroniki ya kutuma
na kutoa fedha kwa njia ya simu. Vilevile, kupitia Sheria ya Fedha ya Mwaka
2022, Kanuni za Malipo ya Taifa (The National Payment
System (Electronic Money Transaction Levy) Regulations 2021) zilifanyiwa
marekebisho kwa lengo la kuongeza wigo wa tozo hiyo kwa miamala yote ya
kielektroniki. Marekebisho hayo yalihusisha miamala ifuatayo ya kielektroniki ambayo inalalamikiwa;
a) Kuhamisha fedha kutoka akaunti ya Benki ya mtumiaji kwenda mitandao ya simu;
b) Kuhamisha fedha kutoka akaunti ya Benki ya mtumiaji kwenda akaunti nyingine ya mtumiaji ndani ya benki husika;
c) Kuhamisha fedha kutoka akaunti ya
benki ya mtumiaji kwenda akaunti ya benki nyingine;
d) Uhamishaji wa Fedha
kimataifa;
e) Kutoa fedha taslimu kutoka akaunti
ya simu ya mtumiaji au akaunti ya benki kwa mkusanyaji, wakala wa mkusanyaji au
mashine ya kuhesabu fedha kielektroniki.
Mheshimiwa
Spika, Kuongezwa kwa wigo wa utozaji wa tozo
za miamala kumepelekea malalamiko hasi kutoka kwa wadau. Wapo waliodhania
gharama zote hizo zimeletwa na Serikali ili hali gharama za kutuma au kutoa
fedha zimejumuisha gharama za taasisi husika na nyongeza kidogo ya Serikali.
Kwa mfano unapotoa TZS 15,000 ni TZS 2,443, Gharama ya Benki ya Tangu zamani ni
TZS 2,200 na tozo ya Serikali yaani gharama mpya ni TZS 243, na kwenye kutuma zaidi
ya milioni tatu kielektoniki (T.T)
gharama ilikuwa TZS 14,000 ambapo gharama za Mabenki tangu zamani ni TZS 10,000
na tozo ya Serikali ni TZS 4,000.
Mheshimiwa Spika, Kufuatia malalamiko hayo,
Kamati Kuu ya Chama Cha Mapinduzi chini ya Mwenyekiti wake Mheshimiwa Samia Suluhu
Hassan kiliielekeza Serikali kupitia upya tozo za miamala na kuzingatia maoni ya
wananchi. Wizara ya Fedha na Mipango kupitia wataalam wake wa Bajeti na wataalam
wa Sera wakiwashirikisha wadau wamefanyia kazi maelekezo ya Chama na Maelekezo ya
Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kupitia
upya tozo hizo.
Mheshimiwa
Spika, naomba kusisitiza hapa wataalam wa Wizara ya Fedha na Mipango
wanaohusika na maswala ya Bajeti na Sera wamefanya mapitio haya wakiwa Ofisini
kama Sehemu ya Majukumu yao ya Kila siku tofauti na taarifa zilizozungushwa
kuwa kuna tume ya watu 200 imeundwa na inatumia mabilioni ya fedha. Napenda kuwasilisha taarifa kuwa tumefanya mapitio kama ifuatavyo: Kupunguza mzigo wa tozo kwa jamii, Kuchochea matumizi
ya miamala kwa njia ya fedha taslimu (cash); Kurahisisha utozaji, na Kuzuia utozaji
wa tozo husika mara mbili kwa kuwa utozaji wake kwa sasa unahusisha pande zote mbili
yaani mtoaji na mpokeaji.
Marekebisho
Yatakayofanyika
Mheshimiwa
Spika, marekebisho
yatakayofanyika ni kama ifuatavyo;
a)
Kufuta
tozo ya kuhamisha fedha kutoka benki kwenda mitandao ya simu (pande zote);
b)
Kufuta
tozo ya kuhamisha fedha ndani ya benki moja (pande zote);
c)
Kufuta tozo
ya kuhamisha fedha kutoka benki moja kwenda benki nyingine (pande zote);
d)
Wafanyabiashara
(merchants) hawatahusishwa kama ilivyo kwenye kanuni za sasa;
e)
Kusamehe
tozo ya miamala kwenye utoaji wa fedha taslimu kupitia wakala wa benki na ATM kwa
miamala yenye thamani isiyozidi shilingi 30,000; na
f)
Kupunguza
gharama ya miamala kwa asilimia 10 hadi asilimia 50 kufuatana na kundi la
miamala. Ikumbukwe kuwa tozo hizo ambapo viwango vya tozo vilishushwa kwa
asilimia 30 kutoka kiwango cha juu cha shilingi 10,000 hadi kiwango cha juu cha
shilingi 7,000, viwango ambavyo vilianza kutumika tarehe 07 Septemba, 2021.
Kadhalika, Mheshimiwa Rais alisisitiza kupunguzwa zaidi tozo ambapo Wizara ya Fedha
ilipunguza tozo zaidi kwa kushusha tena kiwango cha juu kutoka 7,000 hadi
4,000.
Mheshimiwa Spika, marekebisho haya yataanza kutumika tarehe 1 Oktoba 2022.
Mheshimiwa Spika, Sambamba na hatua hiyo, Serikali inafuta utaratibu wa kodi ya
zuio inayotokana na pango kukusanywa na mpangaji na badala yake jukumu hilo
linarejeshwa kwa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwa
utaratibu utakao bainishwa kwenye kanuni. Napenda kusisitiza kuwa kodi ya
zuio ya pango siyo ya mpangaji bali inapaswa kulipwa na mpangishaji ambaye
ndiye anapokea mapato kutokana na uwekezaji au biashara ya kupangisha.
Utaratibu huo umekuwa ukitumika kwa muda mrefu kwenye nyumba za biashara na
nyumba zinazopangishwa kwenye makampuni au mashirika yanayofunga ritani za
kodi.
HITIMISHO
Mheshimiwa Spika,
mwisho lakini sio kwa umhimu nisisitize mambo mawili:
1) Ni
dhahiri kwamba punguzo hili litapunguza mapato ya Serikali, naelekeza fedha hizi zifidiwe kutokana na kubana matumizi
mengineyo ndani ya Serikali ambayo
hayataathiri utekelezaji wa majukumu ya Msingi ya mafungu husika.
Namwelekeza Mlipaji Mkuu
wa Serikali kukaa na Maafisa Masuuli wote kuyaangalia upya mafungu ya matumizi Mengineyo
ili miradi ya maendeleo yote isiathirike kwa hatua hii. Tukate kwenye chai,
vitafunwa, misafara kwenye safari za ndani na nje kwa maafisa wa Wizara zetu kama Mhe Rais alivyoelekeza,
tukate Mafunzo, Semina,
Matamasha, Warsha, makundi yanayokwenda
kukagua mradi ule ule kwa nyakati tofauti au makundi yanayokwenda eneo lilelile
kila mtu na gari lake (Mfano, Wilaya ile ile kila Afisa na gari peke yake, Mkoa
ule ule kila Kiongozi na gari pekee yake).
Mheshimiwa Spika, Naomba
kuwasilisha.
Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba Madelu
(Mb.)
Waziri wa
Fedha na Mipango,
No comments:
Post a Comment