Serikali ya mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kuimarisha mashirikiano yaliyopo baina ya Zanzibar na Kuwait kwa maslahi ya wananchi wa pande zote mbili.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla ameeleza hayo Ofisini kwake Vuga alipokutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Kuwait Nchini Tanzania Mhe.Mubarak Mohammed Alsehaijn.
Mhe hemed amesema mashirikiano kati ya Nchi hizo mbili ni ya muda mrefu sasa na tayari Kuwait wameshasaidia mambo mbali mbali ya kimaendeleo.
Aidha Mhe. Hemed ameeleza kuwa katika mazungumzo yao wamekubaliana mambo mbali mbali yakiwemo kuendeleza marekebisho ya hospitali ya rufaa ya Mnazi mmoja ambayo ni ushirikiano wanchi tofauti ikiwemo nchi ya Kuwait.
Amesema kuwa katika mzungumzo hayo wamekubaliana kuanzisha uwekezaji mwengine katika sekta ya elimu ili kuwasaidia wananchi wa Zanzibar katika kukuza sekta hio.
Sambamba na hayo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar amemshukuru Balozi huyo kwa mashirikiano ya karibu na Zanzibar na kuwataka wananchi kuenzi yale yote amabyo yanafanywa na nchi rafiki katika kupeleka mbele maendeleo yetu ikiwemo Kuwait.
Nae Balozi wa Kuwait nchini Tanzania Mhe.Mubarak Mohammed Alsehaijn amemuhakikisha Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kuwa nchi yake itaendelea kuimarisha uhusiano uliopo baina ya nchi hizo mbili.
Aidha Balozi Mubarak amemshukuru Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwa mashirikiano yaliyopo baina ya Kuwait na Tanzania na kuahidi kutafuta ufumbuzi kwa changamoto zote ambazo zinaweza kukwamisha baadhi ya miradi ambayo inayosimamiwa na nchi yao ili kuwaletea maendeleo wananchi wa Zanzibar.
Ali Moh’d
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais
12/09/2022
No comments:
Post a Comment