Habari za Punde

Taifa linakabiliwa na changamoto kubwa kwa baadhi ya watumishi wa umma waliopewa dhamana kukosa uadilifu

 

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk.Hussein Ali Mwinyi akizungumza na kuwasalimia Waumini wa Dini ya Kiislam baada ya kumalizika kwa Ibada ya Sala ya Ijumaa iliyofanyika  leo 2-9-2022 katika Mskiti wa Mabuluu Mlandege Wilaya ya Mjini Unguja

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi  Alhaj Dk. Hussein Ali Mwinyi amesema Taifa linakabiliwa na changamoto kubwa kwa baadhi ya watumishi wa umma waliopewa dhamana kukosa uadilifu na kusababisha mapato ya Serikali kuingia mifukoni mwao.

Alhaj Dk. Mwinyi amesema hayo katika salamu zake kwa waumini waliohudhuria Ibada ya sala ya ijumaa iliofanyika Msikiti Mabluu, Mkoa wa Mjini Magharibi.

Ameeleza kuwa taarifa ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ilitolewa hivi karibuni imebainisha kuwepo ubadhirifu mkubwa wa fedha za Serikali, hivyo akasema Serikali itachukua hatua thabiti kudhibiti ubadhirifu wa mali ya umma.

Aliwahimiza wafanyakazi, ikiwemo wale wanaokabidhiwa nyadhifa  kuwa waaminifu katika utekelezaji wa majukumu yao na kusisitiza azma ya Serikali ya kufanyakazi ya kuondosha madhila katika utumishi wa umma.

Aidha, aliitaka jamii kuendelea kuhimiza suala la kukabiliana na vitendo vya udhalilishaji wa kijinsia dhidi ya wanawake na watoto.

Alhaj Dk. Mwinyi alisisitiza umuhimu wa wananchi kudumisha amani na kusema anafarijika mno kusikia watu wote wanahubiri jambo hilo na kubainisha umuhimu wake katika maendeleo ya nchi kiuchumi na kijamii, “ .......... bila ya amani hakuna ibada”, alisema.

Aidha, alitumia nafasi hiyo kutoa shukrani zake za dhati kwa niaba ya Familia yake kwa  wananchi wote ambao kwa namna moja au nyengine wamemfariji kutokana na msiba wa kuondokewa na kaka yake Hassan Ali Mwinyi, aliefariki dunia Jumatano wiki hii katika Hospitali Kuu ya Mnazimmoja, Mkoa Mjini Magharibi.

Nae, Katibu Mtendaji Ofisi ya Mufti Mkuu wa Zanzibar Sheikh Khalid Ali Mfaume  alisema Rais Dk. Mwinyi ni mtu mwenye manufaa makubwa kwa wananchi wa Zanzibar kutokana na juhudi zake za kusimamia maendeleo ya kiuchumi na kijamii hapa nchini.

Mapema, Khatibu wa Sala hiyo ya ijumaa Sheikh Said Ali Saleh alisema amani ndio msingi wa  mambo yote na neema kubwa miongoni mwa neema zilizotoka kwa Mwenyezi Mungu .

Alisema katika kufanya ibada  imani pekee haitoshi ni lazima iambatane na vitendo.

“Msingi mzima wa Ibada unabebwa na kuwepo kwa amani, jambo ambalo liko mikononi mwa binadamu wenyewe”alisema.  

Imetayarishwa na Idaya ya Mawasiliano

Ikulu Zanzibar.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.