Habari za Punde

Wananchi watakiwa kuimarisha mshikamano uliopo


 Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Alhajj Hemed Suleiman Abdulla akiwasalimia waumini wa Masjid AL- ITISWAM Shumba Mjini wilaya ya Micheweni Mkoa wa Kaskazini Pemba mara baada ya  Ibada ya Sala ya Ijumaa.

Na Ali Mohammed OMPR

Waislamu na Wananchi kwa ujumla wametakiwa kuimarisha mshikamano uliopo kwa maslahi ya Taifa .

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Alhajj Hemed Suleiman Abdulla ametoa kauli hiyo alipojumuika na Waumini katika Masjid AL- ITISWAM Shumba Mjini wilaya ya Micheweni Mkoa wa Kaskazini Pemba wakati wa Ibada ya Sala ya Ijumaa.

Ameeleza kuwa ni wajibu wa kila muislamu na mzanzibari kuimarisha umoja na mshikamano uliopo na kuweza kusaidiana kwa kila mwenye uwezo kwani kufanya hivyo kutaongeza mapenzi kwa wanashumba na wazanzibar kwa ujumla.

Alhajj Hemed amewataka waumini na wananchi kuendelea kuwasimamia na kuwasaidia watu wenye mahitaji maalum wakiwemo wajane, watu wenye ulemavu na watu wasiojiweza ili kujenga jamii yenye upendo na mshikamano baina yao kwa maslahi ya vizazi vya sasa na baadae.

Akizungumzia suala la madawa ya kulevya na udhalilishaji Alhaj hemed amesema waislamu na wazanzibar ni vyema kujitathmini  kwa kila hali ili kuweza kuyatokomeza matendo haya maovu hapa nchini.

Aidha Mhe. Hemed amewataka waumini haku kutoa mashirikiano pindi  yanapotokea masuala hayo ya udhalilishaji na madawa ya kulevya kijijini hapo kwenda kuripoti sehemu husika ili hatua ziweze kuchukuliwa.                                  

Sambamba na hayo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar amewataka walimu wa madrasa na waislamu kwa ujumla kuwa na utamaduni wa kuiombea dua nchi yetu pamoja na kumuombea Dua rais wa Zanzibar Dkt. Husein Mwinyi ili aweze kutimiza yale yote aliyoyaahidi kwa wananchi wake.

Kwa upande wake Imam wa Msikiti huo  Sheh. Omar Hija  amewataka Waumini kuwa na utamaduni wa kuwa na shukrani katika maisha ya kila siku ili kuweza kupata mafanikio katika maisha yao duniani na kesho akhera.

Amesema ni wajibu kwa kila muumini kuweza kushukuru neema zote alizopata kutoka kwa mwenyezi mungu ili kupata fadhila zake, pia Mtume Muhamad S.A.W amesema kuwa  “asiweza kumshukuru binadamu mwenzake basi hawezi kumshukuru mwenyezi mungu”.

 Baada ya kumaliza Ibada ya Swala ya Ijumaa Alhajj Hemed alipata fursa ya kuifariji familia ya Bwana. Ali Shapandu Sharif kufatia kifo cha baba yao Ali Sharif kilichotokea hivi karibuni pamoja na kumjulia hali Sheha wa Shehia ya Micheweni Bwana.DAWA JUMA MSHINDO nyumbani kwake Micheweni Mkoa wa Kaskazini Pemba.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.