Tanzania
na Zambia zimedhamiria kumaliza changamoto za kibiashara na usafirishaji
zinazowakabili wafanyabiashara ili kuruhusu biashara na usafirishaji wa bidhaa
ufanyike bila vikwazo baina ya nchi hizo.
Hayo
yamebainishwa katika hotuba ya ufunguzi iliyosomwa na Katibu Mkuu Wizara ya
Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Joseph Sokoine wakati
wa Mkutano wa Tume ya Kudumu ya Pamoja ya Ushirikiano (JPC) kati ya Tanzania na
Zambia ngazi ya Wataalam unaofanyika leo tarehe 12 Oktoba 2022 jijini Lusaka
Zambia.
Balozi
Sokoine aliwasisitiza watendaji kutumia
mkutano huo kuandaa mikakati ya pamoja itakayosaidia kuondoa vikwazo vya
kibiashara na kutengeneza mazingira wezeshi kwa sekta ya umma na binafsi ili
ziweze kufanya uwekezaji utakaoleta maendeleo endelevu kwa ajili ya maslahi
mapana ya kiuchumi kwa pande zote mbili.
“Tanzania
ina dhamira ya dhati ya kuimarisha ushirikiano wake wa kindugu na kihistoria na
Zambia ili kuendeleza jitihada zilizoasisiwa na waasisi wa mataifa yetu kwa
kuweka mfumo rasmi wa ushirikiano unaowezesha ufuatiliaji wa utekelezaji katika
masuala ya ushirikiano” alisema Balozi Sokoine.
Aidha,
alieleza kuwa ushirikiano imara na wenye mafanikio ni ule unaojengwa kwa mfumo
rasmi ambao unaruhusu kukutana na kufanya majadiliano ya mara kwa mara hivyo,
alieleza kuwa ana amini kupitia mkutano huu maeneo yote ya ushirikiano yenye
changamoto yatajadiliwa kwa kina kwa maslahi ya nchi zote mbili na wananchi
wake.
Naye
Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa Zambia, Bw.
Chembo Mbula alieleza kuwa ni muhimu majadiliano yakaangalia kwa kina maeneo
muhimu yatakayowezesha pande zote mbili kuwa na mchango katika maendeleo ya
mtangamano wa kikanda.
“Nchi
zetu zimepiga hatua kiuchumi na katika maendeleo ya jamii tangu kumalizika kwa
mkutano wa tisa wa Tume ya Pamoja ya Kudumu ya ushirikiano baina yetu, hivyo ni
vyema majadiliano yakaendana na uhalisia wa mabadilika hayo” alisema, Bw.
Mbula.
Pamoja
na mambo mengine mkutano huu utapitia na kujadili utekelezaji wa maazimio ya
Mkutano wa Tisa wa Tume ya Kudumu ya pamoja ya ushirikiano kati ya Tanzania na
Zambia uliofanyika tarehe 25 na 26 Februari 2016 jijini Dar es Salaam.
Mkutano
huo ulioanza tarehe 11 Oktoba 2022 kwa ngazi ya Wataalam, utafuatiwa mkutano wa
Makatibu Wakuu na utahitimishwa kwa
mkutano wa ngazi ya Mawaziri utakaofanyika tarehe 14 Oktoba 2022 jijini
humo.
-Mwisho-
Imetolewa na:
Kitengo cha
Mawasiliano ya Serikali.
No comments:
Post a Comment